Zinazobamba

KAMUPUNI YA USAFIRI WA MTANDAO"IZZE RIDE"YAZINDULIWA DAR.

*Yalenga kuleta Mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri mtandao Nchini Tanzania.

Na Mussa Augustine.

Kampuni ya usafiri wa mtandao ya IZZE Ride imezinduliwa rasmi leo Machi 18,2026 jijini Dar es Salaam,ikiwa na lengo la kuleta mapinduzi makubwa katika sekta ya usafiri wa teksi mtandao nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo,Mkurugenzi Mtendaji wa IZZE Ride, Fredrick Silaa,amesema jukwaa hilo ni matokeo ya utafiti wa mwaka mmoja uliofanywa na kampuni ya kidijitali ya Kitanzania ya Esteban,kwa lengo la kutatua changamoto za usafiri na kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi.

Amesema IZZE Ride inalenga si tu kuwaunganisha madereva na abiria, bali pia kutoa mfumo wa kisasa wa usimamizi wa magari,kuongeza usalama,na kuboresha ustawi wa madereva kupitia huduma mbalimbali za kijamii na kifedha.

“IZZE Ride ni zaidi ya teksi mtandao,ni jukwaa linalowajumuisha wadau wote wa sekta hii kwa kuhakikisha usalama,uwazi na fursa za kiuchumi kwa madereva na abiria,” amesema Silaa.

Katika uzinduzi huo,kampuni hiyo imeeleza kuwa madereva watakaojiunga na jukwaa hilo watanufaika na huduma ya bima ya afya,usajili wa hifadhi ya jamii kupitia Mfuko wa Taifa wa hifadhi ya Jamii(NSSF),pamoja na mfumo maalum wa kidijitali wa kufuatilia matumizi ya magari na matengenezo yake.

Aidha,IZZE Ride imeingia ubia na CRDB Benki kupitia huduma ya“Lipa Hapa”, hatua itakayowezesha malipo ya papo kwa papo kwa kutumia simu au kadi za benki,huku madereva wakipokea mapato yao moja kwa moja kwenye akaunti zao za benki.

Kwa mujibu wa Silaa jukwaa hilo pia linazingatia kikamilifu sheria na kanuni zinazosimamiwa na Mamlaka ya kudhibiti vyombo vya usafiri majini na ardhini(LATRA),kuhakikisha huduma zake zinakuwa salama na zenye viwango vinavyokubalika kisheria.

Uzinduzi wa IZZE Ride unakuja wakati mahitaji ya huduma za teksi mtandao yakiongezeka kwa kasi katika miji mikubwa kama Dar es Salaam, Arusha na Mwanza,hali inayochochewa na ukuaji wa teknolojia na ongezeko la watumiaji wa simu janja.

Aidha Silaa amesema kuwa usajili kwa madereva utakuwa bure,huku mchakato wake ukihitaji nyaraka muhimu ikiwemo leseni ya udereva,usajili wa gari na kibali cha LATRA.

"IZZE Ride imebeba kaulimbiu ya “Ya Kwetu,Ki Vyetu”,ikiwa na dhamira ya kujenga suluhisho la kiafrika kwa changamoto za Kiafrika,hasa katika eneo la ujumuishaji wa kifedha na ajira kwa vijana."amesisitiza Silaa
Kwa upande wake  Mkuu wa kitengo cha huduma za kibenki kidigitali kutoka Benki ya CRDB,Catherine Rutenge amesema kuwa Benki hiyo imejipambanua katika kuhakikisha kwamba Watanzania wengi wanashiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na fedha(Financial inclusion).

"CRDB tunafanya kazi na wadau wengi ambao wao wanaenda kutatua matatizo  mbalimbali yaliyopo kwenye jamii zetu kwa Kila siku, kwahiyo kuna vitu ambavyo tunafanya Moja kwa moja na kuna vitu ambavyo tunampata partners ambao wana malengo makubwa yakufikia jamii ya kitanzania"amesema.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo maafisa wa benki, wafanyakazi wa kampuni hiyo pamoja na waandishi wa habari.

No comments