WIZARA YA NISHATI YAENDELEA KUTOA ELIMU KUHUSU MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA
*📌 Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wanufaika na mafunzo*
*📌 Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034*
Wizara ya Nishati imeendesha mafunzo ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma
Mafunzo haya ni mwendelezo wa jitihada za Wizara ya Nishati katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024–2034, ambao unalenga kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia. Akizungumza katika mafunzo hayo, Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Anitha Ringia, ameipongeza Wizara ya Katiba na Sheria kwa kutambua umuhimu wa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kualika wataalam wa Wizara ya Nishati kutoa elimu husika kwa Watumishi wa wizara hiyo.
Mha. Ringia amesisitiza kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia si tu yanachangia kulinda afya za watumiaji, bali pia ni njia muhimu ya kuhifadhi mazingira na kupunguza uchafuzi wa hewa.“Matumizi yasiyo salama ya nishati ya kupikia yana madhara makubwa kwa afya na mazingira. Kila mtumishi na Mtanzania kwa ujumla anatakiwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutumia nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya taifa letu”. Amesema Mha. Ringia
Awali wakati akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Mbaraka Stambuli, alisema chimbuko la kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa kinara katika kusisitiza matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira.“Tunapaswa kutumia fursa ya mafunzo haya kubadilisha maisha yetu ya kila siku majumbani, ili kusaidia nchi kufikia malengo iliyojiwekea katika mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia”. Amesema Bw. Stambuli.
Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuboresha maisha yao na kuchangia katika utunzaji wa mazingira.Mafunzo hayo pia yalihusiha wataalam kutoka SESCOM na Positive Cooker ambao walitoa elimu kuhusu majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo.

No comments
Post a Comment