Zinazobamba

DOYO: AMANI NI NGUZO KUU YA MAENDELEO NA MAPINDUZI YA UCHUMI TANZANIA


Dar es Salaam 

Mgombea urais kupitia Chama cha National League for Democracy (NLD), Mhe. Doyo Hassan Doyo, na Katibu Mkuu wa chama hicho, amewataka Watanzania kudumisha amani kabla, na baada ya uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa lolote duniani.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika muendelezo wa kampeni za chama hicho zinazofanyika kwa mtindo wa “mobile kampeni”, Doyo alisema chama chake kimefanya kampeni za kistaarabu na kisayansi katika mikoa 26 mpaka sasa. Alisema kampeni hizo zimekuwa zikiwalenga wananchi moja kwa moja ili kuwapa sera na kuelewa changamoto zao bila kutweza utu wa mtu.

“Niwaombe sana, Watanzania wenzangu, mkapige kura kwa amani. Mkivunja amani, hakuna maendeleo yatakayopatikana. Amani ndiyo tunu ya taifa letu,” alisema Mhe. Doyo.

Doyo alifafanua kuwa amani ni sharti muhimu la maendeleo. Alisema pale ambapo amani ipo, ndipo serikali inaweza kutekeleza kwa ufanisi ahadi zake kwa wananchi, ikiwemo kuboresha huduma za jamii, kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Amani huleta utulivu wa kisiasa, hujenga imani kwa wawekezaji, na huipa serikali uwezo wa kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo bila vikwazo. Doyo alisema serikali isiyo na amani haiwezi kusimamia elimu bora, huduma za afya, wala uchumi imara.

“Amani huleta matumaini na nguvu ya kufanya kazi. Serikali itakayojengwa juu ya misingi ya amani itakuwa na uwezo wa kuwatumikia wananchi kwa haki na ufanisi mkubwa,” aliongeza Doyo.

Mhe. Doyo alisisitiza kuwa serikali atakayoiongoza itakuwa ya kuwakomboa Watanzania kiuchumi na kijamii, kwa kuweka mazingira bora ya vijana kujiajiri, kujitegemea na kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Tunataka kuona kijana ana ajiriwa, anajiajiri na kuacha utegemezi. Serikali itakayojengwa juu ya amani itakuwa na nguvu ya kweli ya kuleta mageuzi ya kiuchumi na kijamii,” alisema Doyo.

Akizungumza kuhusu Ilani ya Uchaguzi ya NLD, Doyo alisema chama chake kimeweka mkazo katika kumwezesha kijana wa Kitanzania kujitegemea, kukuza ujasiriamali na kujenga mazingira ya ajira. Alibainisha pia kuwa serikali yao itaweka kipaumbele katika kuboresha huduma za jamii kama elimu, afya na miundombinu, huku ikipunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini ili fedha hizo zielekezwe kwenye sekta zenye manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi.

“Hospitali hazina dawa, barabara hazijakamilika tangu uhuru. Tunataka serikali inayoweka kipaumbele katika maendeleo ya watu, si anasa,” alisisitiza Doyo.

Katika mkutano huo, Doyo alimnadi mgombea ubunge wa NLD Jimbo la Ubungo, Bi. Gradiness Msuya, akisema jimbo hilo limebaki nyuma kimaendeleo kutokana na miundombinu mibovu, shule zisizo na madawati na barabara zisizopitika. Aliwaomba wananchi wa jimbo hilo wamchague mbunge anayetokana na Chama cha NLD.

Kwa upande wake, Bi. Msuya aliwataka wananchi wa Ubungo kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani na busara, ili kuleta mabadiliko ya kweli na maendeleo ya jimbo hilo.

“Niwaombe tarehe 29 Oktoba msifanye makosa. Tukiungana tutaleta mageuzi katika nchi yetu, lakini pia tuijenge Ubungo yetu,” alisema Bi. Msuya.

Bi. Msuya aliwaomba kura wananchi wa Jimbo la Ubungo, huku akiwahidi kushirikiana nao kusukuma maendeleo ya jimbo hilo kwa vitendo.

Naye Meneja kampeni wa Chama cha NLD, Ndugu Pogora Ibrahim Pogola, alieleza kuwa chama hicho kimetumia mbinu mpya za “mobile kampeni” katika uchaguzi huu, mbinu iliyolenga kuwafikia wananchi, badala ya kutumia mikutano mikubwa yenye gharama kubwa, ikizingatiwa kuwa wananchi wengi wanaishi maisha ya kipato cha chini. 

“Tunafanya kampeni za kisayansi. Hatuleti wasanii wala kubeba wananchi kwa magari. Tunawafuata wananchi walipo ili tusikilize matatizo yao na kuwaeleza sera zinazotokana na ilani yetu moja kwa moja,” alisema Pogola.

Ameongeza kuwa Ilani ya NLD inalenga kupunguza maslahi makubwa ya wabunge na kuelekeza fedha hizo katika kuongeza mishahara ya walimu, madaktari na watumishi wa umma.

“Chama chetu kimekuja na ilani bora, inayolenga maendeleo ya watu. Tukipiga kura kwa amani, mkituchagua NLD, sera za chama chetu zote zinatekelezeka kwa ufanisi,” alihitimisha Pogola.

Msafara wa kampeni za chama cha NLD unaelekea Mtwara na Zanzibar katika muendelezo wa kuwataka wananchi kuchagua viongozi waadilifu wanaotokana na chama cha NLD katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29.

No comments