NCCR-MAGEUZI YAPITISHA MGOMBEA URAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA OKTOBA MWAKA HUU
*Yatangaza rasmi tarehe ya kuchukua fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi
Na Mussa Augustine
Chama Cha NCCR-Mageuzi kimesema kuwa zoezi la uchukuaji wa fomu za kugombea katika nafasi mbalimbali za Urais,Ubunge na Udiwani katika Uchaguzi Mkuu ujao,zitaanza kutolewa katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chama hicho kuanzia Mei 31 hadi Juni 15,2025.
Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 13,2025 na Katibu Mkuu wa Chama hicho Evaline Wilbard Munisi wakati akizungumza na Waandishi wa habari Jijini Dar es salaam huku akibainisha kuwa chama hicho kimempitisha Mwenyekiti Taifa wa Chama hicho Haji Ambari Khamis kuwa Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Makamu wake Joseph Roman Selasini kuwa Mgombea Mwenza.
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa NCCR-mageuzi ameongeza kuwa Mgombea Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na mgombea mwenza bado hawajapatikana hivyo chama hicho kinaendelea na mchakato wa kuwapata.
"Kupitia Kikao cha halmashauri Kuu Taifa ya chama hetu kilichofanyika Machi 30 ,20205 chama kimejipanga kushiriki kikamilifu kwa kusimamisha wagombea katika nafasi zote za Udiwani, Uwakilishi katika baraza la Mapinduzi Zanzibar, Ubunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania(JMT),Urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania" amesema Munisi
Nakuongeza kuwa " Tunaomba Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi kuendelea kutoa ushirikiano katika kufanya zoezi hilo la uchaguzi kuwa la Amani, huru na haki kama Rais alivyokwisha kutamka, tunaamini kwa kushirikiana,Elimu ya uraia itatolewa kwa wapiga kura, malalamiko yote ya hilo zoezi yatashughulikiwa kwa wakati muafaka nakwa haki. "
Aidha Katibu Mkuu huyo wa NCCR-mageuzi amewasihi wapiga kura kutumia haki yao ya kikatiba kushiriki kikamilifu hasa katika kupiga kura, ambapo takwimu zinaonesha kwamba tangu Mwaka 2000 katika uchaguzi mkuu ushiriki unakua chini hali inayochangiwa na Watanzania kukata tamaa.
"Tunawaomba Watanzania wote wanaoamini kwamba kwa kujali UTU wetu,haki msingi za kila Mtanzania zitapatikana,wajiunge na chama chetu,na pia tunaomba mwanachama yeyote anayetamani kugombea nafasi husika kujitathmini kwa kuzingatia sifa za kuwa na maadili ya kitanzania,kusimamia maslahi ya wengi dhidi ya wachache ndani na nje,pamoja na kusimamia na kutetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania."amesema
Nakuongeza kuwa" Tunawaomba Watanzania wote wenye kukubaliana na Itikadi yetu ya UTU na misingi yake na jenda yetu ya UZAWA ambapo sisi tunaamini kuwa uchumi wa Taifa letu ukiwa mikononi mwa Wazawa,basi Vijana Wetu watapata ajira lakini pia Wazawa kwa uzalendo wao watalipa Kodi zinazopaswa kulipwa kwa wakati,pia wanachama wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi zilizoainishwa".
No comments
Post a Comment