JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI LIMEWAOMBA WANANCHI KUTOA TAARIFA MAPEMA MAJANGA YA MOTO YANAPOTOKEA.
Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Msemaji wa Jeshi hilo Puyo Nzalayaimisi akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu maadhimisho ya siku ya Wazimamoto duniani leo Mei 4, 2025.
*Laadhimisha siku ya Wazimamoto moto duniani,huku likisisitiza kushirikiana na Jamii.
Na Mussa Augustine.
Wananchi wametakiwa kutoa taarifa mapema pindi majanga ya moto yanapotokea ili kuwezesha Jeshi la zimamoto na Uokoaji kufika mapema na kuweza kudhibiti majanga hayo.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Kamishna wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Msemaji wa Jeshi hilo Puyo Nzalayaimisi wakati akizungumza na Waandishi wa habari katika maadhimisho ya siku ya Wazimamoto duniani inayofanyika Mei 4, kila Mwaka.
Aidha amesema kuwa inapotokea mripuko wa moto wananchi wengi hukimbilia kutoa mali zao za ndani bila kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la zimamoto na Uokoaji hali ambayo inasababisha Jeshi hilo kuchelewa kutoa msaada wa Uokoaji.
Katika hatua nyingine Naibu Kamishna huyo amesema kuwa malengo ya maadhimisho hayo ni kutoa heshima kwa wazima moto waliopoteza Maisha wakiwa kazini, pamoja na kutambua mchango wa wazima moto waliopo hai katika jamii.
Aidha Nzalayaimisi amesema malengo mengine ya maadhimisho hayo ni kuelimisha umma kuhusu majukumu ya Jeshi la Zimamoto na hatua za tahadhari, kujenga mshikamano wa Kimataifa kati ya vyombo vya zimamoto na uokoaji pamoja na kutoa motisha kwa wazimamoto kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa moyo wa uzalendo.
Aidha amesema kwa mwaka huu wa 2025 Jeshi la zimamoto na Uokoaji limefanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni sehemu ya maadhimidho hayo muhimu.
" Tumefanya usafi wa Mazingira katika Hospitali ya Mkoa wa Njombe na Kituo cha afya Msamala Ruvuma, tumetoa msaada wa kibinadamu katika gereza la Mkoa wa Lindi, tumetoa elimu kwa umma kuhusu kinga na tahadhari dhidi ya moto katika shule, masoko, vituo vya mabasi, mikusanyiko ya watu na kupitia vyombo vya habari, pamoja na kupandishwa vyuo kwa baadhi ya maafisa na askari waliotimiza wajibu wao kwa weledi wa kujitolea." amesema.
Nakuongeza kuwa"Tunamshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji katika kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi".
Naibu Kamishna huyo wa Jeshi la zimamoto na Uokoaji na Msemaji wa Jeshi hilo amesisitiza kua siku ya Wazimamoto Duniani si tu siku ya kumbukumbu bali ni mwito wa mshikamano, uzalendo, na kuthamini thamani ya maisha ya binadamu,hivyo ni kuwaenzi mashujaa wao kwa ujasiri wao wa kila siku na kuendelea kushirikiana kuhakikisha jamii inakua salama dhidi ya majanga.
No comments
Post a Comment