UVCCM YAWASISITIZA VIJANA KUJITOKEZA KWENYE ZOEZI LA UBORESHAJI WA DAFTARI LA WAPIGA KURA AWAMU YA PILI
Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM Taifa, Bi. Jessica Mshama.
Na Mwandishi Wetu.
Katika muktadha wa kuimarisha Demokrasia nchini, Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki kikamilifu katika zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili, ambalo litaanza Mei 1 hadi Julai 4, 2025.
Ujumbe huo umetolewa ili kuhakikisha vijana, ambao ni asilimia kubwa ya Watanzania, wanatimiza haki yao ya msingi ya kupiga kura na kuchagua viongozi wanaowakilisha maslahi yao.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 29, 2025 jijini Dar es Salaam, Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi wa UVCCM Taifa, Bi. Jessica Mshama, ametoa wito kwa vijana wote kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo muhimu kama lilivyotangazwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, zoezi la uboreshaji wa Daftari litaendeshwa kwa awamu tatu. Mzunguko wa kwanza utahusisha mikoa 15 kuanzia Mei 1 hadi 7, ukiwemo Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe.
Mzunguko wa pili utafanyika Mei 8 hadi 15, ukihusisha mikoa 16, ikiwemo Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, na mikoa yote ya Zanzibar. Mzunguko wa tatu utafanyika Mei 16 hadi 22 katika vituo vya magereza 130 Tanzania Bara na vyuo vya mafunzo 10 Zanzibar.
Bi. Mshama amesema jumla ya vituo 7,869 vitatumika katika zoezi hilo, ambapo Tanzania Bara kutakuwa na vituo 7,659 na Zanzibar vituo 210. Ametoa kumbusho kwamba kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya 2022, vijana wanachukua asilimia 34.5 ya Watanzania wote, hivyo kuwa nguzo muhimu ya mwelekeo wa Taifa.
“Hii inamaanisha vijana ndio wenye nguvu ya kubadilisha Taifa. Kila kijana mwenye umri wa miaka 18 au anayefikisha miaka hiyo ifikapo siku ya uchaguzi mkuu 2025, anatakiwa kujiandikisha au kuboresha taarifa zake,” amesema.Aidha, amewahimiza vijana waliopoteza kadi zao, waliobadili makazi au walioharibikiwa na kadi kurekebisha taarifa zao ili waweze kushiriki uchaguzi. “Kuboresha taarifa ni hatua ya kwanza ya kidemokrasia na uzalendo,” aliongeza.
UVCCM pia imetoa onyo kali kwa wale wanaotaka kuwatumia vijana kwa nia ovu ikiwemo kuvuruga mchakato wa kidemokrasia. “Tanzania ni nchi ya sheria na katiba. Kila kijana ana haki ya kushiriki kwa amani, uhuru na utulivu,” alisema Mshama.
Bi. Mshama amewataka vijana kuwa wazalendo, kutokubali kupotoshwa, na kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi hili kwa ajili ya mustakabali bora wa taifa.
Alisisitiza umuhimu wa kulinda amani kama msingi wa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Katika upande wa maendeleo, amewataka vijana kumuunga mkono Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo, akibainisha kuwa zaidi ya ajira milioni 8 zimezalishwa kati ya Novemba 2020 hadi Februari 2025 kupitia miradi mikubwa ya kimkakati na sekta ya elimu na afya.
Pia alieleza kuwa kupitia mikopo ya asilimia 10 kutoka halmashauri zote nchini, zaidi ya Shilingi bilioni 250 zimekwenda kwa vikundi vya vijana kufanikisha miradi ya uzalishaji mali hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2024.
Akihitimisha hotuba yake, Bi. Mshama ametoa wito kwa vijana kuendelea kuwa wazalendo, kutumia fursa zilizopo na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kama njia ya kujenga Tanzania yenye maendeleo endelevu na amani ya kudumu.
Post Comment
No comments
Post a Comment