Zinazobamba

AFRIKA TUNAYAPA KIPAUMBLE MATUMIZI YA NISHATI SAFI ILI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI-DKT.BITEKO

 DAR ES SALAAM.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Afrika inahamasisha matumizi ya nishati safi licha ya kuwa na mchango mdogo kwenye uchafuzi wa mazingira. Ameyasema hayo Machi 4, 2025, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa awali wa Kongamano la Petroli la EAC (EAPCE’25) jijini Dar es Salaam.

Dkt. Biteko amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili mipango ya matumizi ya nishati safi, hasa katika sekta ya kupikia na usafiri (CNG), ili kupunguza athari za tabianchi. Amesisitiza kuwa Afrika inahitaji sera thabiti na sheria madhubuti kufanikisha mabadiliko haya.

Aidha, amebainisha kuwa hadi sasa asilimia 81 ya kaya nchini Tanzania zinatumia kuni na mkaa kwa kupikia, hali inayosababisha uharibifu mkubwa wa misitu. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034) unaolenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo 2034.

Kuhusu usafiri, Dkt. Biteko amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) kwa magari.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga, amesema mkutano huo unaweka msingi wa Kongamano Kuu la EAPCE’25 litakaloanza Machi 5, 2025, na kuleta pamoja wadau wa sekta ya mafuta na gesi. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, ameongeza kuwa mkutano huo utajadili njia bora za kuhama kutoka nishati chafu kwenda nishati safi, ikiwa ni sehemu ya mpango wa dunia kufanikisha hili ifikapo mwaka 2050–2060.

Hakuna maoni