UWINDAJI WA KITALII KUIINGIZIA TANZANIA BIL.2.5
Na Happiness Shayo- Dar es Salaam
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajia kuingiza jumla ya Dola za Kimarekani 968,000 sawa na shilingi za kitanzania bilioni 2.5 kama ada ya vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa mwaka pamoja na mapato mengine.
Hayo yamesemwa leo Februari 21,2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) wakati wa hafla ya kukabidhi vyeti vya umiliki wa Vitalu vya Uwindaji wa Kitalii kwa wawekezaji wanne (4), iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Ninayo furaha kukabidhi vyeti hivi kwa wawekezaji ambao ni K&F Wild Expedition Ltd kwa Kilwa Open Area Nakiu, Michel Mantheakis Safaris Ltd kwa Muhesi GR, Out of Africa Ltd kwa Lwafi Nkamba, Royal Conservation Ltd kwa Pori la Akiba la Pololeti na Selous MT2 kwa Neon Investment Ltd chini ya Uwekezaji Mahiri kwenye Maeneo ya Wanyamapori (Special Wildlife Investment Concession Areas-SWICA)” amesisitiza Mhe. Chana. Amefafanua kuwa utoaji wa vyeti hivyo kwa wawekezaji hao wapya unaendana na utekelezaji wa Ilani ya CCM, kutokana na ukweli kwamba hiyo inahalalisha umuhimu wa tasnia ya uwindaji kwa uchumi wa nchi na kusisitiza kuwa Utalii wa Uwindaji huchangia manufaa ya moja kwa moja kwa jamii kupitia ajira na maendeleo ya jamii.
Mhe. Chana ametumia fursa hiyo kuwakaribisha wawekezaji wengine kutoka China na duniani kuwekeza katika Sekta ya Utalii nchini Tanzania huku akimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Mpango wa kuitangaza Tanzania katika kiwango cha kimataifa kupitia filamu za “Amazing Tanzania” na “Tanzania, The Royal Tour”.“Napenda kuwahakikishia wadau wote wa uwindaji kwamba dhamira ya Serikali ni kuendelea kuweka na kudumisha mazingira wezeshi ya biashara zao bila kuathiri uhifadhi na ustawi wa watu wetu” amesema Mhe. Chana.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA, Meja Jenerali Mstaafu Hamis Rajabu Semfuko alisema kuwa TAWA imekuwa ikitumia mikakati ya kimasoko kuvutia wawekezaji kutoka duniani kote ikiwa ni pamoja na matumizi ya mnada wa kielektroniki wa vitalu vya uwindaji ambapo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kupata wawekezaji kutoka China katika sekta ya uwindaji.
"TAWA imejipanga vyema ili kufikia soko la kimataifa na soko la ndani la utalii sambamba na kuangalia uwezekano wa masoko ya mapya ya utalii kama China, Urusi na Brazili” amesema Meja Semfuko.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa Uhifadhi, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA),Mlage Kabange, alifafanua kuwa katika jitihada za kuvutia wawekezaji na watalii zaidi, TAWA itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji.
“Hivi sasa tumejenga kilomita 453.2 za mitandao ya barabara kwa kiwango cha changarawe katika maeneo ya kimkakati sawa na asilimia 40 ya lengo letu ambalo ni kilomita 1,127 ifikapo mwaka 2026, tumejenga miundombinu ya utalii 33 ikijumuisha Banda, kambi na maeneo ya picnic ambayo ni 117% ya maeneo yaliyolengwa ya Utalii. Vilevile, sasa tuko katika asilimia 23 ya lengo letu la kujenga vituo 22 vya kukusanyia mapato kama ilivyotarajiwa ifikapo mwaka 2026. Miundombinu hii ya utalii ililenga kuweka mazingira mazuri ya kuboresha ufikiaji wa vivutio vyetu vya utalii na kukuza utalii na mapato ya Serikali” alisema Bw. Kabange.
Hafla hiyo imehudhuriwa na Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Allexander Lobora, Mwenyekiti wa Kamati ya Ugawaji Vitalu vya Uwindaji na Mjumbe wa Bodi ya TAWA, Prof. Japhary Kideghesho, Wajumbe wa Bodi ya TAWA, Wawakilishi kutoka Timu ya Majadiliano ya Serikali, Katibu wa Chama cha TAHOA, Suleiman Masato na wadau mbalimbali wa Sekta ya Utalii.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni