Zinazobamba

KAMATI YA WATAALAM NISHATI SAFI YA KUPIKIA WAJADILI UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Na Mwandishi Wetu.

Kamati ya wataalam iliyoundwa na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara na Taasisi mbalimbali kwa ajili ya kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Nishati safi ya Kupikia kitaifa imekutana kujadili utekelezaji wa mkakati huo wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania  wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034.

Kikao kazi hicho kimefanyika katika Ofisi za Wakala wa Nishati Vijijini  ( REA )jijini Dodoma Februari 5,2025 ambapo Maafisa Waandamizi hao wamepitia taarifa mbalimbali za utekelezaji na kutoa mapendekezo yaliyolenga kuboresha nyaraka hizo kabla ya kuziwasilisha katika Kamati ya Makatibu Wakuu.

Matumizi ya Nishati safi ya Kupikia ni Ajenda ya Kitaifa inayohakikisha wananchi wanaondokana na matumizi ya nishati isiyo safi  ikiwemo kuni na mkaa.

Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho,  Bw. Omari Ilyas ambaye ni Mkurugenzi Msaidizi Uratibu wa Shughuli za Serikali  kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu amesisitiza utekelezaji wa mkakati huo usiwe na kikwazo hivyo bajeti  za utekelezaji wa mkakati wa  nishati safi ya kupikia zinapaswa kutengwa.

" Wizara na taasisi zote kwa kushirikiana na wadau mbalimbali  wanatakiwa kutekeleza mkakati huu kwa kiwango kikubwa na bajeti zitengwe ili utekelezaji wa mkakati uwe na tija." Amesema IlyasKamati hiyo pia ilipokea wasilisho na kufanya maboresho ya rasimu ya mwongozo wa uratibu wa utekelezaji wa Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia iliyoainisha majukumu ya wadau wote ili kufanikisha uratibu husika kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.



Hakuna maoni