Zinazobamba

DPP MVUNGI ATETA NA MAAFISA BAJETI WA WIZARA NA TAASISI*


Na Saidi Lufune – Morogoro

Mkurugenzi wa Sera na Maendeleo wa Wizara ya Maliasili na Utalii Abdallah Mvungi amewataka wakuu wa seksheni za mipango na maafisa bajeti wa wizara na Taasisi kuzingatia vipaumbele vya Dira ya Maendeleo ya Taifa wakati wa uandaaji wa Randama  ya mwaka wa fedha 2025/2026 ili kufikia malengo  ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan

Mvungi amesema hayo Mkoani Morogoro Februari 19, 2025 akifungua kikao kazi cha uandaaji wa Randama ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2025/ 2026 ambapo amewataka kuhakikisha kuwa mipango na bajeti  ya Wizara inazingatia vipaumbele vya taifa na inaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) pamoja na Ilani ya Chama Tawala.

“Maandalizi ya Randama ni fursa adhimu ya kutathmini utekelezaji wa bajeti ya mwaka uliopita, kubaini changamoto zilizojitokeza, na kuweka mikakati thabiti ya kuboresha utekelezaji wa bajeti ijayo. Hivyo tunapaswa kuhakikisha kuwa tunapanga bajeti inayojibu mahitaji ya wananchi, inayoakisi hali halisi ya kiuchumi, na yenye kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya nchi yetu.” Amesema Mvungi

Aidha, Mvungi amesema kikao hicho ni hatua  muhimu katika kufanya uchambuzi wa kina wa vipaumbele vya sekta mbalimbali kulingana na rasilimali zilizopo, kuleta ushirikiano wa karibu kati ya Wizara, Idara, na Taasisi katika kupanga na kuweka bajeti inayotekelezeka,kuongezeka kwa ubunifu katika uandaaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha ufanisi na tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.

“Ninawasihi wote tushiriki kwa umakini na uwajibikaji mkubwa ili tuweze kuandaa bajeti bora, inayojibu mahitaji ya wananchi, na inayotekelezeka kwa ufanisi kwa uondoa changamoto za wananchi katika maeneo yao” Amesema Mvungi

Kikao hicho cha siku saba pamoja na mambo mengine kitapitia maoni na ushauri wa kamati ya kudumu ya Ardhi Maliasili na Utalii, kuandaa shughuli zilizotekelezwa na Wizara Julai 2024 hadi Februari 2025, mafanikio changamoto na mikakati ya utatuzi yake sambamba na kuandaa shughuli zitazotarajiwa kutekelezwa mwaka wa fedha 2025/2026

Hakuna maoni