CCM:Jussa ni Ian Smith wa Zanzibar
Chama Cha Mapinduzi(CCM) kimesema Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Ismail Jussa Ladhu, kifikra na kiitikadi ni sawa na aliyekuwa kiongozi wa kibaraka Ian Smith mpambe wa sera za Wakoloni huko South Rhodesia (Zimbabwe)
CCM kimemtaja ni kibaraka mkongwe kutokana na ushamba wa kubeza maendeleo yanayoletwa na viongozi wa Afrika akishabikia ukoloni.
Hayo yametamkwa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo , Mbeto Khamis Mbeto, aliyemwita Jussa ni kibaraka kama alivyokuwa smithi au Mtawala wa zamani wa Zaire, Mobutu Seseseko.
Mobutu na Smith walikuwa viongozi wasaliti dhidi ya maendeleo ya Afrika na kuwa mashabiki wakubwa wa sera na misimamo ya kikoloni.
Mbeto alisema Jussa amekuwa mstari wa mbele kuponda juhudi za SMZ chini ya Rais Hussein Ali Mwinyi za ujenzi wa shule za ghorofa, bila aibu hudai majengo hayo hayana maana kwa maendeleo ya Zanzibar.
Mara kadhaa Jussa amekuwa akijinasibu yeye amesoma kwenye maghorofa machache yalioojengwa na utawala wa kifalme.
Alisema Jussa alipaswa kusifu baada ya kuona watoto wa Wakulima na Wakwezi, sasa wakisoma shule zilizo bora, kinyume chake, amekuwa akidai majengo hayo si chochote kwa maendeleo ya Zanzibari.
"Jussa ni kibaraka mpya miongoni mwa vibaraka wachache waliobaki Afrika. Ni Ian Smith mpya na kikwazo kwa maendeleo ya Zanzibar pia akifanana kifkra na Rais wa zamani huko Zaire Mobutu Seseseko " Alisema Mbeto
Aidha Katibu huyo Mwenezi alisema kinadharia na kiuhalisia , Makamu huyo Mwenyekiti ACT Wazalendo ,bado anatamani sera za ukandamizaji chini ya ukoloni uliowanyima elimu watoto wa kiafrika.
' Jussa acha kujivunia shule chache za ghorofa zilizoachwa na Wakoloni .Ni aibu kwako na kwa ACT Wazalendo .Matamshi yako yanazidi kukinyima kura ACT kutokana na ulimi wako kuwa mchafu " Alisisitiza
Mbeto alisema wakati Jussa akijigamba kuwepo kwa shule chache za ghorofa ndani ya Mji Mkongwe, huko Kisiwapanza,Fundo, Muwambe , Makunduchi, Paje , Donge na Mtambwe , wakoloni toka Mwaka 1804 hadi 1964 , hawakujenga shule za ghorofa.
'Mazuri yanayofanyika sasa ni baada ya Mapinduzi Matukufu Mwaka 1964.
Watoto wa kina Pandu, Jecha, Makame na Simai wanapata elimu bora . Hivi sasa huko Kojani Tumbatu, Kisiwapanza na Kiwani watoto wa Wakulima na Wavuvi wanasoma katika shule za ghorofa za SMZ " Alisema
Hakuna maoni
Chapisha Maoni