Zinazobamba

TANZANIA KUWA KITUO CHA MFANO KATIKA HUDUMA ZA HALI YA HEWA AFRIKA.

DODOMA.

Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mikakati madhubuti ya kuifanya Tanzania kuwa kinara wa huduma za hali ya hewa barani Afrika kupitia uwekezaji mkubwa katika miundombinu na teknolojia.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza leo Jumanne, Januari 21, 2025, katika hafla ya uzinduzi wa mradi wa Systematic Observation Financing Facility (SOFF) iliyofanyika katika Ukumbi wa Midland Inn View, Dodoma, alisema hatua hizi ni sehemu ya juhudi za Serikali kuboresha maisha ya wananchi na kuimarisha sekta muhimu zinazotegemea hali ya hewa.

Akifafanua kuhusu uwekezaji unaofanywa, Mheshimiwa Majaliwa alisema kuwa rada saba za hali ya hewa zimeagizwa kwa ajili ya kuhakikisha utabiri sahihi, huku Chuo cha Taifa cha Hali ya Hewa kikipanuliwa ili kutoa mafunzo ya kisasa kwa wataalamu. Pia, vifaa vinavyotumia zebaki vimeanza kuondolewa, kufuatia masharti ya Mkataba wa Minamata.

“Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kununua vituo 11 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe, ambavyo vitakuwa sehemu ya mtandao wa kimataifa wa kukusanya na kubadilishana data,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alieleza kuwa Tanzania imechangia zaidi ya dola za Marekani milioni nne kwa njia ya huduma zisizo za kifedha ili kufanikisha utekelezaji wa mradi wa SOFF. Mradi huu unalenga kuimarisha ubadilishanaji wa data za hali ya hewa duniani na kuhakikisha tahadhari za hali mbaya ya hewa zinapatikana kwa wakati na usahihi.Waziri Mkuu alisisitiza kuwa sekta kama kilimo, ufugaji, nishati, maji, afya, na usafirishaji zinategemea kwa kiasi kikubwa utabiri wa hali ya hewa. “Uwekezaji huu unaenda kusaidia nchi yetu kuwa tayari kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa sekta zetu za uchumi,” alisema.

Kwa mujibu wa Mheshimiwa Majaliwa, uzinduzi wa mradi wa SOFF unaleta fursa mpya kwa Tanzania, ikiwemo upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa, kuboresha maamuzi ya kisera, na kusaidia ustawi wa jamii.

Kwa uwekezaji huu, Tanzania inalenga kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma bora za hali ya hewa, siyo tu Afrika Mashariki, bali pia katika ngazi ya kimataifa

Hakuna maoni