Zinazobamba

LATRA CCC YATOA TAHADHARI KIPINDI HIKI CHA MWISHO WA MWAKA.



Na Mussa Augustine.

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini(LATRA CCC) limetoa rai kwa Madereva wanaosafirisha abiria katika msimu huu wa sikuu kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara yatokanayo na ajali zinazoepukika.


Pia kuhakikisha vyombo vya usafiri vyenye hitilafu havitumiki kutoa huduma za usafiri kwa kuhakikisha ukaguzi unafanyikia kwa weledi mkubwa.

Rai hiyo imetolewa leo Desemba 19,2024 Jijini Dar es salaam na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bw.Daud Daudi wakati akizungumza na Waandishi wa habari kwa ajili ya kuelezea mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa safari za mwisho wa mwaka.

Aidha ameiomba Mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini ( LATRA) pamoja na Jeshi la Polisi usalama barabarani, kuongeza nguvu na kutilia mkazo ufuatiliaji wa usalama wa vyombo vya usafiri na ufuatiliaji wa sheria za usalama barabarani kwa madereva wawapo safarini.

" Mamlaka hizi(LATRA na Jeshi la Polisi usalama barabarani)zihakikishe huduma inayotolewa inalingana na madaraja yaliyochaguliwa na abiria,pia kufanya uhakiki endelevu wa vigezo vya vyombo vya usafiri ikiwemo suala la bima ya Chombo husika" amesema Bw.Daud.

Nakuongeza kuwa "Abiria watoe ushirikiano kwa watoa huduma ili kuwawezesha kupatiwa huduma zenye viwango vizuri,na wanapotoa taarifa kwa mamlaka za usimamiaji wa huduma za usafiri ardhini, taarifa hizo ziwe za uhakika ili zisije zikasababisha usumbufu usio wa lazima.

Aidha amewaomba pia abiria kuendelea kupata taarifa muhimu wawapo safarini au kufuatilia mienendo ya vyombo vya usafiri( Mabasi) kupitia tovuti ya pis.latra.go.tz ambapo taarifa mbalimbali zinapatikana,ikiwemo kuonyesha, eneo gari lilipo,mwendo kasi wa gari,muda wa kutegemewa kufika kwenye kituo cha basi.

Aidha ameendelea kusema kuwa watoa huduma wategemee kuwepo ongezeko kubwa la abiria ambao wengi wao sio wale ambao wamekua wakiwahudumia kwa siku za nyuma hivyo wawapatie uhirikiano,na kujitahidi kuendelea kutoa huduma kwa uadilifu kwa kuzingatia matakwa ya leseni zao na kuendelea kukuza majina yao kibiashara kwa kundi hilo kubwa la wasafiri.

Akizungumzia wajibu wa abiria Mtendaji huyo wa LATRA CCC  amesema kuwa abiria ana wajibu wa kutoa taarifa sahihi pale anapopatiwa huduma ambayo haikidhi viwango vya mkataba wake na mtoa huduma( TICKET).
Wajibu mwingine ni kukata tiketi mtandaoni mapema na kuwa na uthibitisho wake kwenye chombo cha kielektroniki au kuchapisha nakala,kuhakiki taarifa zilizopo kwenye tiketi kama majina kamili ya abiria,muda wa usafiri,jina la mtoa huduma,namba ya usajili ya chombo cha usafiri.

Pia kuuliza matumizi sahihi ya huduma mbalimbali zinazopatikana wakati awapo safarini katika chombo,kutunza Mazingira ndani na nje ya chombo cha usafiri.

Katika hatua nyingine Mtendaji huyo wa LATRA CCC amesema kuwa usafiri kwa njia ya Reli umeendelea kupitia shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa huduma za Treni za kawaida ( MGR) na Treni za Umeme (SGR).

"Kufuatia mategemeo ya kuongezeka kwa uhitaji wa usafiri kuelekea sehemu mbalimbali za Nchi ,shirika la Reli Tanzania limeongeza safari za treni kuelekea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha,kuanzia Desemba 9 ,2024 ambapo ni kutoka safari mbili kwa wiki hadi tatu yaani Jumatatu,Jumatano na Ijumaa" amesema Bw.Daudi

Hata hivyo ametoa wito kwa abiria wanaosafiri maeneo hayo kutumia fursa ya usafiri huo mbadala wakati wa msimu huu wa mapumziko ya sikuu za mwisho wa mwaka 2024.


Hakuna maoni