Zinazobamba

TZLPGA INATOA ELIMU KWA JAMII KUIUNGA MKONO SERIKALI MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

        Mkurugenzi Mkuu TZLPGA Bw.Amos Jackson 

Na Mussa Augustine.

Chama cha waagizaji na wasambazaji wa gesi ya mitungi chini(TZLPGA) kinaendelea na utoaji wa elimu kwa wananchi ili watumie nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la Serikali ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa Novemba 8,2024 na Mkurugenzi Mkuu wa Chama hicho Amos Jackson wakati akizungumza na Waandishi wa habari ofisini kwake  Jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa Elimu kuhusu matumizi ya nishati safi itokanayo na gesi asilia imekua changamoto kubwa kutokana na wananchi wengi bado wanatumia Nishati chafu(mkaa na kuni) ambayo inaathiri afya zao pamoja na kusababisha uharibifu wa Mazingira.

Aidha amesema kuwa changamoto nyingine ni gharama ya mitungi ya gesi,ambapo watu wengi wamekua wakitumia sababu hiyo kama sababu ya kutotumia nishati safi itokanayo na gesi asilia kwa madai kuwa hawana uwezo wa kutumia gesi.

" Hii gesi tunaitoa nje ya nchi,tunainunua kwa gharama ya bei ya soko la Dunia,kwa maana hiyo kuna gharama ambazo hatuwezi kudhibiti wenyewe,hivyo kuna gharama ambazo tuna uwezo nazo,zingine hatuna uwezo nazo kama vile gharama ya kuinunua nje ya nchi" amesema

Nakuongeza kuwa"hizi gharama za kununua gesi nje zinachangia kati ya asilimia 50 hadi 55 ya bei ya mwisho ambayo mtu analipia hii gesi ya kupikia,
kwa mfano kama mtungi mdogo wa kilo sita unauzwa shilingi elfu ishirini na tano( 25,000),maana yake kati ya shilingi elfu kumi(10,000) hadi elfu kumi na tano( (15,000) ni gharama ya kununua gesi nje ya nchi,hapa hatuwezi kufanya kitu kwenye hiyo,inayobaki elfu kumi(10,000)ni gharama ya kupokelea gesi bandarini ,kuhifadhi kwenye miundombinu pamoja na kuisafirisha kumfikia mtumiaji pamoja na tozo mbalimbali zinazotozwa na Serikali hasa maeneo ya bandari"
     
Jackson amesema kuwa Serikali imefanya kazi kubwa ya kuondoa kodi kwenye gesi nakwamba tozo zilizopo kwa sasa Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea na mchakato wake wa kuweza kuziondoa ili nishati hiyo iweze kuwa na gharama nafuu zaidi.

Aidha Mkurugenzi huyo wa TZLPGA ameendelea kufafanua kuwa gharama zingine zimekua zikitokana na kukosekana kwa ubora wa vifaa ambavyo mtumiaji anatumia kwenye mtungi,ambapo vimekua vikikaa kwa muda mfupi vinaharibika.

"Kwa mfano kuna zile bana ambazo zinatumika kwenye mitungi midogo zinauzwa elfu mbili(2000) hadi elfu mbili mia tano(2500)mtu anatumia baada ya mwezi kinaharibika,mbali na kutumia gharama kubwa lakini kinaweza kumletea hatari gesi kuvuja au kuripuka moto" amesema 

Nakuongeza kuwa" Sisi kama Chama tumeanza kufanya kazi na shirika letu la viwango( TBS) hivi karibuni tutakua na mkutano wa kushirikisha wale wote wanaoagiza hivi vifaa tuwafundishe namna yakufanya hiyo biashara vizuri ili waagize vifaa vyenye ubora mzuri.

Aidha amesema kua eneo hilo wameliangalia kwa undani ili kuhakikisha vifaa vinavyotumika kwenye gesi viwe na ubora nakwamba jitihada hizo wanazifanya kwa kushirikiana na TBS,EWURA pamoja na Zimamoto.

Aidha ameongeza kuwa kuna baadhi ya mawakala wamekua wakijaza mitungi kiuhalifu akitolea mfano mitungi ya kilo 6 inajazwa kilo 4 nakuuzwa kwa gharama ileile ya kilo 6, hali hiyo inawafanya watumiaji kulalamika kuwa gesi imeisha haraka,nakusema kuwa changamoto hiyo wanaifanyia kazi pamoja na mamlaka husika ikiwemo Wakala wa vipimo(MWA),pamoja na EWURA kwa ajili ya kuhakikisha kila wakala wa usambazaji wa gesi anakua na mzani wa kupimia gesi hiyo.

"Juzi tu hapa Dar es salaam tumekamata watu wanne na Arusha wawili ambao wamejaza mitungi kiuhalifu,tunataka kila wakala wa gesi awe na mzani kwenye eneo lake la Biashara ili mteja akifika pale wanaipima gesi anajiridhisha ujazo uliopo ndipo anachukua kwenda kuitumia"amesema Jackson 

Akizungumzia fursa zinazopatikana kwenye mnyororo wa usambazaji wa Nishati hiyo Mkurugenzi Mkuu huyo wa TZLPGA amesema kuwa kuna fursa mbalimbali ikiwemo uwekezaji katika miundombinu ya upokeaji wa gesi bandarini,matenki ya kuhifadhi gesi pamoja na kuisafirisha kwa watumiaji maeneo mbalimbali nchini.

"Kuna fursa ya kuwekeza kwenye miundombinu ya kupokelea gesi kwenye bandari ya Dar es salaam na bandari ya Tanga,miundombinu iliyopo kwa sasa haina uwezo wa kupokea meli kubwa,pia matenki ya kuhifadhia gesi( terminal's)bado tunahitaji wawekezaji zaidi,pia kuwekeza kwenye Viwanda vya kutengeneza mitungi,pamoja magari ya kuisafirisha mitungi hiyo kwenda kwa watumiaji maeneo mbalimbali" amesema.




Hakuna maoni