TUMIENI MATOKEO YA TAFITI ZA KISAYANSI KATIKA UTEKELEZAJI WA MIPANGO YA KITAIFA” WAZIRI MKUU
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa amewataka Idara na Taasisi za utafiti na elimu ya juu ziendelee kufanya tafiti za kisayansi ili kutafuta suluhisho za changamoto zenye mwingiliano wa afya ya binadamu, afya ya wanyama, na afya ya mazingira. Aidha, Idara na Taasisi za Serikali zitumie matokeo ya tafiti hizo katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Kitaifa.
Akizungumza wakati akifungua Mkutano wa Afya Moja leo Novemba 4, 2024 Jijini Arusha Waziri Mkuu amesema Taasisi zote zinazohusika na masuala mtambuka katika afya ya jamii, wanyama na mazingira zitenge fedha na kuweka katika mipango ya taasisi hizo afua za kuthibiti magonjwa ya kizoonotiki, usugu wa vimelea dhidi ya dawa, magonjwa yasiyoambukiza, mabadiliko ya tabia nchi, na usalama wa chakula.
“Wizara za kisekta, na Mamlaka za Serikali za Mitaa, andaeni mipango kazi na taratibu za usimamizi kwa ajili ya utekezaji wa mbinu ya Afya Moja kwa kuzingatia miongozo iliyopo ambayo imeweka bayana majukumu ya wadau wote aidha Mamlaka za Serikali za Mitaa fanyeni vikao vya mara kwa mara, kufanya tathmini ya utekelezaji wa pamoja wa afua mbalimbali, kwa kufanya hivyo changamoto zitajulikana mapema na kupatiwa ufumbuzi”.Alisema Waziri Mkuu
Aidha Waziri Mkuu amesema tafiti zinaonesha kuwa, duniani kote takribani visa bilioni moja vya ugonjwa pamoja na mamilioni ya vifo hutokea kila mwaka kutokana na magonjwa yanayotoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu aidha, zaidi ya asilimia 75 ya vimelea vipya 30 vya magonjwa vilivyogunduliwa katika miongo mitatu iliyopita, vimetoka kwa wanyama.
“kwa mujibu wa taarifa na takwimu zilizopo, Taifa la Tanzania kama mataifa mengine duniani limekuwa likikumbwa na magonjwa hayo, Kama mtakumbuka, mnamo mwaka 2017 wataalam wetu kutoka sekta mbalimbali waliainisha magonjwa ya zoonotiki yanayopewa kipaumbele hapa nchi kwetu ambayo ni kichaa cha mbwa; kimeta; malale; brusela; homa ya bonde la ufa; homa ya mafua; na magonjwa yanayosababishwa na virusi vya ebola na Marburg”Alieleza Waziri Mkuu
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Mheshimiwa Ummy Nderiananga akieleza kuhusu mkutano huo amesema, Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuratibu shughuli za Serikali ikiwemo la menejimenti ya maafa ambapo katika hatua hii Dhana ya Afya Moja inaendelea kupewa kipaumbele hususani kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwani suala hilo linagusa sekta nyingi.
“Kwa kuwa utekelezaji wa Afya Moja unahisisha wadau mbalimbali ndani nan je ya nchi, na huu mkutano ni moja ya mkakati wa kuimarisha ushirikiano pamoja na kutoa elimu ya kujiandaa na kukabiliana na majanga ya afya moja yenye athari kwa binadamu, Wanyama na mfumo wa kiikolojia,”alisema Nderiananga
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kwamba matatizo mengi yanayoathiri afya ya binadamu kwa kiwango cha zaidi ya asilimia 60 huanzia kwa wanyama, mimea pamoja na mazingira, hivyo dhana ya Afya Moja ndiyo njia pekee ya kukabiliana nayo na kuyadhibiti matatizo hayo.
“Katika kufanikisha dhana ya afya moja Wizara yangu iko tayari na itaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na sekta zenye dhamana ya afya ya Binadamu, Afya ya Mimea pamoja na Mazingira katika kutekeleza dhana hii. Washirika wa maendeleo wamekuwa wakishiriki na sisi bega kwa bega katika kukuza uelewa na ushiriki kwenye dhana hii,”alisema mhe. Ulega
Akizitaja faida zilizopatikana tangu kuanza utekelezaji wa dhana hiyo katika sekta ya mifugo amesema ni pamoja na ; kutumia Dhana hiyo kuunganisha Sekta zote katika kukabiliana na mlipuko wa Homa ya Bonde la Ufa mwaka 2007, kukabiliana na magonjwa ya Kizoonotiki; mojawapo ukiwa ni Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti na Kutokomeza Kichaa cha Mbwa. Mkakati huu utaiwezesha Tanzania kunufaika kwa kupata chanjo dhidi ya kichaa cha mbwa kutoka benki ya chanjo ya Shirika la Afya ya Wanyama Duniani (WOAH) ikiwa nchi ya tatu Afrika kunufaika na mpango huu.
“….Pia imesaidia Kukabiliana na matukio mbalimbali ya mlipuko wa ugonjwa wa Kimeta. Mfano mmojawapo ni ule uliotokea kwenye mifugo na baadae kusambaa kwa binadamu katika Halmashauri ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe mwaka 2022,”aliongezea.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni