Zinazobamba

PROF.MBARAWA AMETOA WITO KWA WAWEKEZAJI KUTOKA JAPANI KUJA KUWEKEZA KATIKA MAENEO YA BANDARI NA RELI

Na Mussa Augustine.

Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amewaomba wawekezaji katika Sekta ya Uchukuzi  kutoka Nchi ya Japani kuja kuwekeza Nchini Tanzania kwenye Miradi ya kimkakati ikiwemo maeneo ya Bandari na Reli ambayo yana manufaa kwa nchi zote mbili.

 Rai hiyo ameitoa Januari 8,2024 Jijini Dar es Salaam wakati alipokua akifungua Mkutano wa kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya Uchukuzi ambapo wamekutana wadau mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Miundombinu ya Japani Afrika (JAIDA), Shirika la Reli Tanzania  (TRC) pamoja na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).

 Prof Mbarawa amesema kwamba, mahusiano kati ya Sekta Binafsi na Serikali (PPP) yameendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora ikiwemo utendaji wa ufanisi wa bandari hapa nchini na kuwavutia wawekezaji toka sehemu mbalimbali duniani.

 Aidha, Waziri huyo wa Uchukuzi ametaja maeneo yanayohitaji uwekezaji kuwa ni pamoja na ujenzi wa kituo cha kuhifadhi makasha katika bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa barabara ya reli ya Isaka-Lusumo-Kigali yenye urefu wa kilomita 495.

 Kadhalika  amebainisha  sababu zilizopelekea kuongezeka kwa Meli nchini Tanzania kuwa  ni pamoja na uwezeshaji toka Serikalini, ongezeko la kina cha lango la Bandari hadi mita 15.5 ambacho kinatosha kuhudumia Meli gatini

 Nae Waziri wa Ardhi, Miundombinu, Usafiri na Utalii kutoka Serikali ya Japan, Mhe. Konosuke Kokuba, amesema kuwa wataendelea kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo kwa kuendelea kujenga miundombinu yenye ubora katika miradi yote inayoendelea na ile ambayo inatarajiwa kutekelezwa.

 Amesema kuwa, kutokana ongezeko la watu katika nchi zinazokuwa zinahitaji teknolojia za kisasa katika ujenzi wa miundombinu nchini ili ziweze kutosheleza mahitaji.

 Haya yanajiri ikiwa ni siku chache tu zilizopita ambapo Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yasushi Misawa alitembelea Bandari ya Dar es Salaam kuendeleza uhusiano wa kibiashara baina ya nchi yake na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania – TPA.

 Kando ya Mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania(TPA) Plasduce Mbossa amesema kuwa Kwasasa Mamlaka hiyo imejipanga kutoa huduma za bandari kwa ufanisi mkubwa

 “Miaka mitatu iliyopita huduma za bandari zinazidi kuwa za ufanisi mkubwa licha ya kuwepo kwa changamoto ya upanuzi wa gati,lakini kwa uwekezaji wa kampuni ya DP World  ambao unaanza hivi karibuni tunauhakikia kuwa ufanisi utazidi kuwa mkubwa”amesema

 

Hakuna maoni