TRA YAPONGEZA WAALIMU NA WANAFUNZI KWA KUSHIRIKI KIKAMILIFU SHINDANO LA VILABU VYA KODI
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Nchini Tanzania TRA Bw. Charles Kichere akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi katika mamlaka Mapato nchini Tanzania TRA Bw. Richard Kayombo wakati wa shindano la Vilabu vya Kodi lililofanyika kwenye Chuo cha Kodi Mwenge jijini Dar es salaam leo.
Baadhi ya majaji wa shindano hilo wakiedelea na kazi yao ya kupata washindi wa shindano hilo.
Baadhi ya washiriki kutoka shule ya sekondari ya Saint Joseph jijini Dar es salaam.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) Bw. Charles Kichere ametoa pongezi nyingi katika hotuba yake kwa waalimu , wanafunzi na Wakuu wa Idara mbali mbali za Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na wadau wote kwa kazi nzuri ya kushiriki kwenye mashindano ya vilabu vya kodi kwa shule za Sekondari za mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Amesema kuwa ni matumaini yake kuwa wanafunzi wamejiandaa vizuri na kwa kiwango cha hali ya juu katika uelewa wa masuala ya kodi na ni kutokana na jitihada zao ndiyo maana leo wapo tayari kwa shindano. “Tunatarajia shindano hili litafanikiwa mbali ya kuwa mlikuwa na majukumu mengine yakimasomo” amesema Kamishna Kichere.
Kamishna Kichere ameyasema hayo leo wakati wa mashindano ya vilabu vya kodi katika shule mbalimbali mkoani Dar es salaam na Pwani yaliyofanyika Mwenge kwenye Chuo cha Kodi jijini Dar es salaam na kushirikisha shule mbalimbali katika mashindano hayo.
Ameongeza kuwa Inafahamika bila kificho kuwa hakuna jambo lolote linaloanzishwa na kufanikiwa bila kuwa na walimu. Katika mashindano yanayofanyika walimu wamefanya kazi kubwa sana ya kuwaunganisha na kuwaandaa wanafunzi na shule zao. Hongereni sana kwa kazi kubwa na nzuri mliyoifanya. Ni mchango wenu pia katika kujenga Taifa letu.
Aidha Kamishna Kichere amewashukuru sana wanachama wa vilabu vya kodi kwa kuwa mstari wa mbele katika kujiandaa na mashindano hayo ambayo yanategemewa kuleta tija katika masuala mazima ya kodi hapo baadaye
Amewaomba walimu kuendelea kutoa msaada katika kuendeleza vilabu hivi kwani kwa kufanya hivyo utakuwa ni mchango wao mkubwa wa kusambaza elimu ya kodi kwa taifa. TRA inaahidi kuendelea kutoa msaada na ushirikiano katika vilabu vya kodi vilivyoanzishwa na kuendelea kufungua vilabu vingine katika shule nyingi zaidi za sekondari nchini.
Amemaliza kwa kuwakumbusha waalimu na wanafunzi wanaoshiriki katika mashindano haya kuwa waliyojifunza ni vyema wakayafanyia kazi na kuwapatia wengine elimu hiyo kwa manufaa ya Taifa letu. TRA itatoa kila ushirikiano kwa shule zote ambazo zitaonyesha uhitaji wa kupata elimu ya kodi wakati wote itakapohitajika.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Elimu kwa Mlipa Kodi katika mamlaka Mapato nchini Tanzania (TRA) Bw. Richard Kayombo amewapongeza walimu na wanafunzi hao kwa kazi nzuri waliyoifanya mpaka kufikia siku ya mashindano hayo yaani leo.
Bw. Kayombo amesema Vilabu vya kodi ni mkusanyiko wa wanafunzi wenye nia ya kukuza ufahamu na uelewe wa masuala mbalimbali yanayohusu kodi katika shule za sekondari vinalenga hapa nchini ikiwa ni pamoja na Kuandaa vijana waweze kutimiza wajibu wao pindi watakapoanza kupata mapato.
Ameongeza kwamba lengo kubwa ni Kukuza ufahamu wa masuala mbalimbali ya kodi kwa vijana, Kuandaa wataalamu wa kodi wa baadae, Kuwafanya wanachama waelewe umuhimu wa kudai risiti wanunuapo bidhaa au huduma, Kuwajengea uzalendo vijana wawe na utamaduni wa kulipa kodi kwa wakati.
Ameongeza kuwa serikali inatumia kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi ikiwa ni pamoja na Kumjengea mwanafunzi uwezo wa kufikiri, kujiamaini na kuchambua kwa ufasaha masuala mbalimbali yanayohusu kodi .
Mamlaka ya Mapato Tanzania imekuwa ikifanya mashindano haya kila mwaka tangu mwaka 2008, ambapo katika shindano la mwaka huu wanafunzi watashindana juu ya masuala mbalimbali kuhusu kodi na ukusanyaji wa risiti.
Serikali ya awamu ya tano imeweka kipaumbele katika kuhakikisha kuwa mapato ya serikali yanakusanywa kwa ufanisi na weledi hivyo basi katika shindano hilo Mamlaka ya Mapato (TRA) inatarajia kupata washindi waliokusanya risiti nyingi katika manunuzi mbalimbali yaliyofanyika toka kwa wafanyabiashara katika Mikoa Dar es Salaam na Pwani, kama kauli mbiu yetu inavyosema” Ukiuza Toa Risiti na Ukinunua Dai Risiti”.
Kayombo ameongeza kuwa katika shughuli yoyote haikosi kuwa na changamoto na changamoto ambazo tunakabiliana nazo kama TRA ni Ufinyu wa bajeti kwa ajili ya Kutoa elimu ya kodi kwa wanachama wote ili waweze kuelewa sheria za kodi zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania pamoja na Kuandaa makongamano na midahalo ambayo itawezesha wanafunzi kukutana na kubadilishana mawazo kwa ufanisi mkubwa .