Zinazobamba

WATU WASIOJULIKANA WAWATISHA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU ,WAIBUKA KUILIMA TAMKO KALI SERIKALI YA JPM,SOMA HAPO KUJUA


Pichani ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Herren Kijo Bisimba akizungumza leo na waandishi wa habari.

NA KAROLI  VINSENT
MASHIRIKA  ya utetezi wa haki za binadamu nchini  wamesema kwa sasa nchini pamekuwa sio sehemu salama kama wanavyodai viongozi kutokana na kuongezeka matukio ya utekaji, kushambuliwa kwa wanasiasa pamoja na kutokea mauaji ya raia wasiokuwa na hatia.


Pia, Mashirika hayo yamesema kama jitihada za makusudi zisipofanywa na serikali ikiwemo kuunda tume maalum ya kuchunguza na kubaini ni watu gani wanaofanya matukio hayo ili yaweze kutokomezwa basi hali ya amani tuliokuwa nayo ipo Shakani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dk Herren Kijo Bisimba wakati akisoma tamko la kuzungumzia hali ya nchi, tamko hilo ambalo limetolewa na mashirika 102 nchini ambayo ni ya kutetea haki za binadamu.

Amesema kwa kipindi cha miaka miwili  tangu Rais John Magufuli aingie madarakani kumetokea matukio kadhaa ya ukiukwaji za misingi ya utawala bora na haki za binaadamu ambayo yamesababishwa na vitendo vya mauaji, utekaji na manyanyaso kwa watetezi wa haki za binadamu, viongozi wa kisiasa pamoja na kuuliwa kwa wananchi wasio na hatia.

"Matukio haya hapa nchini yameendelea kuleta hofu baina ya wananchi kuhusu hali ya usalama nchini, "Amesema.

         TUKIO LA KUSHAMBULIWA TUNDU LISSU.

Watetezi hao wameonyesha masikitiko makubwa kwa kitendo cha kupigwa risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye alipigwa risasi mwishoni mwa wiki iliyopita  mkoani Dodoma alipokua Bungeni na kupelekea kukimbulizwa kwa matibabu, Nairobi nchini Kenya.

Akizungumza  kwa Uchungu, Kijo- Bisimba  amesema kitendo hicho ni cha kinyama kuwahi kutokea nchini hasa kwa kiongozi na mtetezi wa haki za binadamu.

"Lissu  amekuwa mwanaharakati wa muda mrefu wa utetezi wa haki za binadamu na rasilimali za nchi pamoja na mambo mengi. Anastahili heshima kubwa katika ulinzi wa haki za binadamu na utawala bora kitaifa na kimataifa"amesema Kijo-Bisimba .

Amesema Lissu amefanya kazi kubwa hapa nchini ikiwemo kufichua jinsi ambavyo madini ya nchi yaliyovyokuwa yakiporwa kupitia mikataba mibovu ya madini pamoja na sheria mbovu za madini huku akiwasemea bila uoga wowote  wachimbaji wadogo walioporwa migodi yao na kampuni za madini  wakisaidiwa na vyombo  vya dola.

"Hata baada ya kuchaguliwa kuwa mbunge  amekuwa mtetezi imara wa utawala bora ambapo jitihada zake ambazo amekuwa akizifanya serikali ya awamu ya tano imezichukua na kufanyia marekebisho sheria za madini na petroli , hivyo  mtu  huyu badala kumlipa kwa kumpiga risasi alipaswa kukumbatiwa kama hazina  kubwa katika siasa, utetezi, sheria na rasilimali madini  hapa nchini. "amesema.

KUONGEZEKA KWA MATUKIO  YA KUTISHIA RAIA.

Watetezi hao wamesema kwa kipindi cha miaka miwili kumeongezeka  kwa matukio ya raia kutekwa  na hata wengine kuuliwa jambo ambalo watetezi  hao  wanadai kuwa matendo hayo yanaondoa sifa ya Tanzania kuwa nchi ya amani.

Akitaja  baadhi ya matukio  hayo Kijo-Bisimba amesema ni tukio la kutekwa na kuuliwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoa wa Geita Alphonce  Mawazo ambaye alifanyiwa unyama huo na watu wasiojulikana. Pia kutekwa kwa Salma Said mwandishi wa Mwananchi Communication Limited na mwandishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujerumani ( Deutsche Welle)  katika mazingira ya kutatanisha.

Matukio mengine ni kupotea kwa Benard Saanane maarufu kama Ben Saanane,  kuokotwa kwa miili saba huko Bagamoyo eneo la mto Ruvu,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam  Paul Makonda akiwa na watu wanaodhaniwa kuwa askari kuvamia kituo cha Televisheni cha "Clouds Media Group" wakiwa na silaha za moto, Nape Nnauye kutishiwa kupigwa risasi kwa bastola na Msanii Roma Mkatoliki pamoja na Rapa Moni Central Zone ambao walitekwa na watu wasiojulikana.

MAPENDEKEZO

Kufuatia matukio hayo yanayotishia usalama wa raia nchini watetezi hao wametoa mapendekezo 11. Baadhi ya mapendekezo hayo ni kutaka uchunguzi wa kina ufanyike kupitia tume huru itakayoundwa na bunge pamoja na vyombo vya kimataifa ili kupata taarifa sahihi za watu waliofanya jaribio la kumuua Lissu.

Watu waliotajwa au kuonekana waziwazi katika vyombo vya habari hasa waliomshambulia Nape Nnauye, waliovamia kituo cha Televisheni cha Clouds Media na walio vamia mkutano wa CUF wafikishwe mahakamani haraka iwezekanavyo kujibu tuhuma zinazowakabili.

Serikali inapaswa kuzingatia misingi ya kimataifa ya haki za binadamu kama ilivyoainishwa katika Mikataba ya Umoja wa Mataifa ambayo Tanzania ni mwanachama.

Aidha tasnia ya sheria iachwe huru katika kufanya kazi zake na kupatiwa ulinzi kwa mujibu wa sheria, mahakama, kama mhimili muhimu katika usimamizi wa haki,  ina wajibu wa kuhakikisha kwamba maofisa wote wanaofanya kazi chini ya mhimili huo wanakuwa salama na wanalindwa kwa mujibu wa sheria katika kutekeleza majukumu yao.