Zinazobamba

Serikali yawaonya waajiri kuhusu wafanyakazi wanaonyonyesha

Serikali imeonya waajiri wanaoweka vikwazo kwa wafanyakazi wao wanaonyonyesha watoto walio chini ya miezi sita.

Onyo hilo limetolewa leo Jumanne na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati anafungua maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani.

"Serikali ya awamu ya tano katika kuhakikisha watoto wanakuwa na afya bora, imeweka kanuni inayompa nafasi ya saa mbili mama mwenye mtoto wa chini ya miezi sita kumnyonyesha mwanaye," amesema Waziri Mwalimu.

Amesema kutokana na kanuni hiyo, waajiri wanapaswa kuwapa ushirikiano mzuri akina mama hao, kwa kuwa maziwa ya mama ndiyo msingi wa afya bora ya mtoto.

Waziri Mwalimu amebainisha kuwa ili mtoto aweze kuwa na afya bora, anapaswa kunyonya maziwa ya mama kwa miezi sita mfululizo bila kinywaji au chakula kingine chochote.

Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Chakula na Lishe, Dk Joycline Kaganda, amesema maadhimisho haya hufanywa kila mwaka kuanzia Agosti 1 hadi 7.

"Maadhimisho haya yanalenga kusisitiza umuhimu wa kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji wa maziwa ya mama,"amesema

Katika maadhimisho hayo, programu ya huduma ya taarifa za lishe kupitia simu za mkononi (M-Nutrition) imezinduliwa. Progrtamu hiyo inakusudia kuleta mabadiliko ya tabia kuhusu afya na lishe ya watoto, wanawake wajawazito  na wanyonyeshao.