Zinazobamba

MGOMO WA TUNDU LISSU MAHAKAMANI WAANZA KUTIKISWA,SOMA HAPO KUJUA

SIKU moja baada ya Baraza la Uongozi la Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kuitisha mgomo wa siku mbili kwa wanachama wake nchini wa kutohudhuria katika Mahakama pamoja na Mabaraza ya aina zote, Mkurugenzi Mtendaji wa Smile Stars Attorneys na Mwanachama wa TLS Leonard Manyama amelaani kitendo hicho na kuutaka viongozi wao kutolitumia Baraza kwa maslahi yao kisiasa.



Jana BARAZA la Uongozi la TLS kupitia Rais wao Tundu Lissu liliwataka Mawakili wote wanachama wa chama hicho kususia kuhudhuria katika Mahakama pamoja na Mabaraza ya aina zote kati ya kesho na kesho kutwa ( Agosti 29 hadi 30 mwaka huu).

Lissu alisema lengo la mgomo huo ni kuunga mkono mawakili wa IMMMA Advocates waliounguliwa na Ofisi zao kwa mlipuko wa mabomu ili kuonyesha kutokubaliana kwao na vitendo vya kihalifu vya kuwashambulia mawakili hao.

Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo leo jijini Dar es Salaam akizungumza na waandishi wa habari, Manyama amewataka wanachama wasikubali chama hicho kutumiwa kisiasa na kiharakati.

“Kitendo kile kimefanywa na wahalifu wenye nia ovu ambao vyombo vya dola vitawashughulikia, kufanya mgomo ni kuumiza wanachi wengine wasio na hatia kwa sababu tu ya kikundi kidogo cha wahalifu,” amesema Manyama.

Aidha amesema badala ya kufanya mgomo huo wanatakiwa kuacha vyombo vya dola kufanya uchunguzi ili kubaini wahalifu hao huku akieleza kuwa itakuwa ni kitendo cha ajabu kama mawakili watatekeleza agizo hilo wakati vyombo hivyo vikendelea na uchunguzi.

Ameendelea kusema kuwa uhalifu huo uneweza kutokea mahali popote ambapo alitoa mfano kwa tukio la uhalifu lililowahi kutokea  katika Mahakama  Kuu Kanda ya Dar es Salaam lakini hakuna tamko la jinsi hiyo lililotolewa na TLS huku tukio hilo pia likiwa na viashiria vya kuingilia uhuru wa Mahakama na mawakili.

Amesesitiza kwa kuwataka Mawakili kuachana na mgomo huo ili kutoathiri wananchi walio wengi wanaohitaji msaada wao wa kisheria. Amewataka wananchi wenye ushahidi wa tukio hilo la shambulio kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili kuwakamata watekelezaji wa shambulio hilo.

Aidha amelitaka Baraza la Uongozi wa TLS kuacha kutoa matamko ambayo yanaweza kujenga uadui baina ya wanachi na serikali kwani kwa kauli zile zianafanya wananchi kuamini kuwa vyombo vya dola ndiyo vilivyohusika.

Jana Rais Lissu alisema kuwa waliotekeleza ni kikundi cha watu ambao walikuwa wamevalia sale za Jeshi la Polisi ambapo Manyama amefafanua kuwa hata majambazi wanaweza kuvaa sale hizo ili kufanya uhalifu kwa urahisi.