Zinazobamba

DC HAPI AMALIZA MGOGORO ULIOWASHINDA WENGI KINONDONI,SOMA HAPO KUJUA


Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Ally Salum Hapi amefanya maamuzi magumu leo Jijini Dar es Salaam Kata ya Kunduchi Mjimwema baada ya kuumaliza mgogoro ulikuwepo kati ya wachimbaji wa kokoto na wananchi wapatao 3000 wa eneo hilo, mgogoro ambao umedumu kwa muda wa zaidi ya miaka 20.
DC Hapi ameagiza wananchi wa eneo hilo kuendelea kukaa maeneo hayo baada ya leseni ya uchimbaji kokoto eneo hilo kufutwa kutokana na uharibifu wa miundombinu.
"Hatuwezi kuhatarisha maisha ya wananchi 3000, tutawapeleka wapi, kwani wao siyo wanakinondoni, kwani wao siyo watanzania" Alisema DC Hapi.
DC Hapi ametoa maagizo kwa watendaji kuhakikisha kuwa wananchi hao wanamilikishwa maeneo hayo kwao kufuata taratibu na sheria ambapo itabidi maeneo hayo yapimwe na wananchi hao wawe wavumilivu maana kuna baadhi ya maeneo yatatengwa kwa huduma za kijamii, ikiwemo vituo vya Afya, Polisi na barabara.
Hata hivyo DC Hapi amewatoa hofu wananchi wa maeneo hayo kuhusu kulipia gharama za upimaji wa ardhi ambazo itabidi wachangie, huku akieleza kuwa wataiandikia barua mamlaka ya chuo cha Ardhi ili waweze kutoa baadhi ya wanafunzi ambao watafanya upimaji katika eneo hilo bure na kuwaondolea wananchi gharama za ziada.
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamini Sitta amesisitiza kuwa serikali itakuwa bega kwa bega na wananchi wanyonge kuhakikisha haki yao haipotei, huku Diwani wa Kata hiyo akihimiza ushirikiano katika shughuli za maendeleo kwani maendeleo hayana chama, hvyo ni vyema kuondoa itikadi.
Wananchi wa maeneo hayo wameonesha kuridhishwa na uamuzi huo wa serikali na kuhaidi kutoa ushirikiano wa hali na mali, huku wakimpongeza Rais Magufuli kwa serikali yake kujali maslahi ya wanyonge.