Zinazobamba

CHAMA CHA ADC CHAMUANGIKIA RAIS MAGUFULI,SOMA HAPO KUJUA

Katibu mkuu wa chama cha ADC Bw. Doyo Hassani Doyo akiongea na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es salaam na kulia kwake ni Bi. Queen Cathbert Sindiga ambae ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho na kushoto Afisa Mahusiano  Bw. Yahaya Chande
CHAMA cha Alliance For Democratic Change (ADC), kimemuomba Rais John Magufuli kuviachia vyama vya siasa vya upinzani kufanya shughuli za kisiasa kwa kuwa ni takwa la kisheria.

Kauli hiyo ilitolewa leo jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Taifa wa chama hicho Doyo Doyo  wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema serikali kuendelea kuzuia shughuli za kisiasa ni tishio kwa vyama kama ADC huenda vikafa.

“Hali ya kisiasa sio nzuri sana, kuna hali ya kutopata uhuru wa kufanya siasa hasa katika upande wa vyama vya upinzani katika nchi yetu, kwa mfano kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa, makongamano na kadhalika,”
“ADC inamuomba mh. Rais Magufuli atuachie tufanye mikutano kwani jambo hili ni takwa la kisheria,” amesema Doyo.
Aidha alibainisha chama hicho kupata mshangao juu ya mgogoro wa Chama cha Wananchi CUF kushindwa kutafutiwa ufumbuzi wa haraka hali inayofanya wanachama wao kukata tamaa.
Amesema kuwa wao wanachukizwa na hali hiyo kwani kuendelea kwa mgogoro huo kwa muda mrefu ni kuondoa afya ya upinzani katika macho ya watanzania, hivyo kuwaomba Maalim Seif Sharif Hamad na Profesa Ibrahim Lipumba wakae pamoja ili kumaliza tofauti zao.

Kwa upande chama hicho kilieleza kushtushwa na matamko mbalimbali ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuingilia mgogoro huo wa CUF hadi kupanga njama za kibabe kwenda kumuondoa kwa nguvu Pfofesa Lipumba.
Doyo aliwataka Chadema kuacha mara moja kuingilia mgogoro usiowahusu ambapo alisema kwamba kitendo cha wao kuingilia mgogoro huo ni mkakati wa kisiasa 
unaofanywa na chama hicho ili kujitengenezea hati miliki ya kisiasa nchini, lakini pia kinaweza kuhatarisha amani.
Akizungumzia kuhusu hali ya nchi alisema kuwa hawalizishwi kutokana na taarifa za mauaji yanayoendelea Kibiti mkoani Pwani kutia dowa Taifa ambapo aliiomba serikali kujipanga upwa na kuweka mkakati madhubuti ya kukabiliana na wahalifu.
Aidha alimpongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake anazofanya kuzuia rasilimali za nchi hasa kwa kitendo cha kuwasilisha miswada kwa hati ya dharura bungeni ili kufanyiwa marekebisho ya sheria.