TFDA yaunda kikosi kusaka ukweli mchele plastiki Dar
MAMLAKA
ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imeunda kikosi maalum ili kupata
ukweli juu ya mchele unaodaiwa kutengenezwa kwa kutumia plastiki baada
ya picha kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa umeanza kutumiwa na
baadhi ya mamalishe jijini Dar es Salaaam.
Baada
ya picha hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, ikielezea mchele huo
kutumiwa na mamalishe kariakoo jijini Dar es Salaam, baadhi ya wananchi
hususan wanaopata huduma ya chakula kwa mama lishe hao, walianza
kuingiwa na hofu.
Mkurugenzi
Mkuu wa (TFDA), Hiiti Sillo,jana alisema mamlaka imeanza kufuatilia
suala hilo na kwamba imeunda timu maalum ili kubaini ukweli wa suala
hilo.
Aidha,
alisema taarifa za awali walizipata kupitia mtandano wa kijamii na Juni
8, mwaka huu, walitoa taarifa ya ufafanuzi kuwa hapakuwa na mchele wa
aina hiyo ingawa wanaendelea kufuatilia.
“Mchele
ambao upo na ambao TFDA tunautambua ni wa Basmati ambao huitwa Sunrice.
Huu wa kutengenezwa kwa plastiki tunaendelea kufuatilia kama taarifa
hizo ni za kweli au la,” alisema.
Alisema
timu hiyo imeanza kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini kama ni kweli
mchele huo uko sokoni. Aliwataka wenye taarifa za ziada kuhusu mchele
huo wawapelekee ili kurahisisha uchunguzi.
“Tunaomba
wenye taarifa za wapi mchele huu unauzwa, waliotumia watuletee au
wapeleke taarifa serikali za mitaa wanakotoka, polisi au kwenye ofisi
zozote za serikali ili tuweze kufuatilia jambo hili kwa urahisi,”
alisema.
Mkurugenzi
huyo alikiri kwamba mamlaka yake imepata taarifa juu ya mchele huo
ingawa hadi sasa haijadhibitisha kama kweli umeshaingia nchini.
“Tayari
nimeshatoa maelekezo kwenye kanda zetu za TFDA zikiwamo Mwanza, Arusha,
Mbeya kuanza kufuatilia na ninavyozungumza ni kwamba ukaguzi
unaendelea. Kama taarifa hizi ni za kweli tunamwomba huyu aliyetuma
‘clip’ (picha) hii kwenye mitandao ya kijamii ajitokeze ili atusaidie ni
wapi alikula mchele huu maana clip inaonyesha mkono tu,” alisema.
Katika
‘clip’ hiyo, kijana huyo anaeleza kuhusu chakula hicho (wali)
walioletewa na mama lishe huko Kariakoo huku akifinyanga tonge na
kuonyesha tofauti yake na ule wa kawaida.
Sillo
alisema taarifa mbaya zinazohusu chakula zinagusa watu na maisha yao
kwa ujumla ndiyo maana wanamwomba mtu huyo awape ushirikiano ili wawajue
wauzaji na wasambazaji.
“Wito
wangu kwa watu wanaponunua kitu chochote wadai risiti hii itasaidia
matatizo kama haya yanapojitokeza inakuwa rahisi kumkamata mhusika,”
alisema.
Kuibuka
kwa taarifa juu ya kuwapo mchele wa plastiki, kumezua taharuki na gumzo
kwa wakazi wa Dar es Salaam ambao asilimia kubwa ndicho chakula chao na
wengi hula kwa mama lishe.