Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mhandisi Kapuulya Musomba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uunganishwaji na usambazaji wa gesi asilia leo Jijini Dar es Salaam.
KATIKA kuhakikisha wananchi wananufaika na Gesi
nchini,Shirika la Maendeleo ya Petrori nchini (TPDC) kwa kushirikiana na Sekta binafsi wanatarajia
kutekeleza miradi mbalimbali ya usambazaji wa gesi asilia katika Mikoa ya Dar
es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na baadhi ya mikoa mingine itakayoidhinishwa.
Akizungumza
na waandishi wa habari leo habari Ofisini kwake leo Jijini Dar es Salaam Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC Mhandisi Kapuulya amesema kuwa miradi hiyo imeanza
kwa kupitia upya taarifa ya awali ya upembuzi yakinifu wa mradi wa ujenzi
wa mtandao wa bomba la kusambazia gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam,
ambapo mnamo mwezi machi 22, 2017 TPDC ilikaribisha jumla ya makampuni 9 ambayo
yalikidhi vigezo vya kimanunuzi kwa ajili ya kazi hiyo.
“Napenda kuutaarifu umma kuwa TPDC inatarajia kutekeleza
miradi mbaimbali ya usambazaji wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam,
Bagamoyo na Mkuranga Mkoani Pwani, Lindi na Mtwara pamoja na baadhi ya mikoa
mingine,” alisema Mhandisi Muyomba.
Aliongeza
kuwa lengo la kupitia upya taarifa za awali ni kuboresha zaidi taarifa za
kifedha, mahitaji ya kiufundi na utambuzi wa njia za kupitisha bomba na ugawaji
wa kanda za usambazaji.
Aidha
alisema kuwa ili kuharakisha usambazaji wa gesi, TPDC inakaribisha na
kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uendelezaji wa miundombinu
itakayowezesha usambazaji wa gesi asilia katika Jiji la Dar es Salaam mara tu
mapitio ya upembuzi yakinifu utakapomalizika.
Mtandao huo
unakadiriwa kuwa na urefu wa takribani kilomita 65 ambao utahudumia, kwa
kuanzia, nyumba 30,000, viwanda na vituo vya kushindilia gesi asilia pamoja na
vituo vya kujazia gesi hiyo.
Katika hatua
nyingine Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa hadi sasa TPDC imefanikiwa
kukiunganisha na mtandao wa gesi asilia Kiwanda kimoja cha kutengeneza Vigae
cha Goodwill kilichopo Mkuranga, Mkoani Pwani huku likiendelea na majadiliano
na viwanda vingine vitatu kwa ajili ya kuunganishwa na mtandao huo.
Kwa mujibu
wa Sheria ya Mafuta ya Mwaka 2015 TPDC inatambuliwa kuwa Shirika rasmi la taifa
linalojiendesha kibiashara, ambapo sheria hii inaipa mamlaka TPDC kuruhusu
makampuni mbalimbali kuendesha shughuli za sekta, zitakazokuwa zainadhibitiwa
kwa utaratibu maalum chini ya usimamizi wa Mdhibiti anayetoa leseni.