Zinazobamba

IDARA YA USALAMA WA TAIFA YAKINGIWA KIFUA BUNGENI,NI KUHUSU KASHFA YA UTEKAJI,SOMA HAPO KUJUA

Mazoea ya baadhi ya wabunge kuomba mwongozo wa kiti cha spika kuzima hoja za wabunge wenzao, jana uliibuka tena baada ya Mbunge wa Makambako, Deo Sanga kuomba mwongozo uliozima hoja ya kutaja majina ya wabunge 11 wanaodaiwa kutaka kutekwa.
Sanga aliomba mwongozo wa Spika kwa kutumia Kanuni 68 (7) pamoja na 64 A,B,C, alisema ndani ya Bunge yameongelewa mambo yanayohusu mahakama, usalama, mauaji na kutekwa.
“Nilikuwa nadhani kupitia kanuni hizi naomba mwongozo wako nini kazi ya Bunge mheshimiwa naibu spika,” alisema.
Mwongozo huo uliibuka baada ya Mbunge wa Viti Maalum CCM, Angelina Malembeka kuwataka wabunge waliosema kuna orodha ya wabunge 11 wanaotakiwa kutekwa kuwataja majina yao.
Hoja ya Malembeka ilimlenga Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ambaye siku za karibuni aliliambia Bunge kwamba ameambiwa na mmoja wa mawaziri kuwa kuna wabunge 11 watatekwa na Usalama wa Taifa.
Malembeka alitoa hoja hiyo wakati akichangia mjadala wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Tamisemi na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2017/18.
Hata hivyo, mwongozo wa spika ulioombwa na Sanga ulizima kiu ya Malembeka aliyetaka kumbana Bashe ataje majina ya wabunge hao 11, badala ya kutaja idadi pekee.
Akijibu mwongozo wa Sanga, Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliamua kupiga marufuku masuala ya Usalama wa Taifa kujadiliwa bungeni. 

Dk Tulia alisema wanaotaka kufanya hivyo wawasilishe hoja mahsusi kwa kufuata Kanuni za Kudumu za Bunge.
Awali, Malembeka alisema ni vizuri Usalama wa Taifa wakaongezwa fedha, mbinu mpya na vifaa ili kurahisisha utendaji wao wa kazi.
“Kutwa mtu anatuma ujumbe kwenye simu kwa rafiki yake eti nimetekwa nyara, waulizeni waliotekwa hiyo simu wamepata wapi ya kutumia huo ujumbe kuwa wametekwa?
“Kutekwa nyara si mchezo, waulizeni wenzenu waliotekwa
watawaambia si mchezo. Na hao wanaojifanya usalama feki naomba mheshimiwa waziri uwashughulikie kwa sababu sasa mtu akishakata ‘panki’ lake akavaa kaunda suti yake anatoa kitambulisho anasema mimi Usalama wa Taifa.
“Usalama wa Taifa mchezo! Mtu anajizungusha zungusha
anawatisha watu mtaani unasema Usalama wa Taifa sasa wale wanaojifanya Usalama wa Taifa na kuogopesha watu mtaani washughulikiwe,” alisema.