DINI YA KIISLAMU INATOA KIPAUMBELE KWA WANAWAKE: SHEIKH JALALA
Na Mwandishi wetu,
IMEELEZWA kuwa dini ya Kiislamu inamtizama mwanamke kama ni mtu muhimu katika kuchangia
maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla na kwamba wanaodhani Uislamu haujampendelea Mwanamke hawaufahamu vizuri Uislamu.
Hayo yameelezwa na Kiongozi wa dini ya kiislamu, dhehebu la Shia ithnasheria, Shehe Hemed Jalala
wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya Kuzaliwa kwa Mjukuu wa Mtume Muhammad(Rehma na Amani ziwe juu yake), Bi. Fatma, aliyezaliwa mwaka wa 615 AD
Katika Maadhimisho hayo,Sheikh Jalala amesema siku hiyo ni muhimu wanapomuenzi mwanamke aliyefanya mambo
makubwa katika dini ikiwa ni pamoja na kuhubiri habari njema.
Amesema kuwa zamani wanawake hawakuruhusiwa kuingia kwenye nyumba za
ibada lakini Mtume kwa kuonyesha umuhimu wa mwanamke alimruhusu Bi Fatma kusimama mbele za msikiti na kutoa khutba kama anavyofanya Mwanaume.
Alifafanua kuwa mwanamke amekamilika kama alivyo mwanaume kwani ndiye
anatengeneza umma, watu na wanaume wanaoleta maendeleo katika jamii na
kusisitiza kuwa penye maendeleo ya mwanaume nyuma yake yupo mwanamke.
"Kumekuwa na maneno kuwa uislamu una aina fulani ya dhuluma kwa
mwanamke, la hasha anapatiwa haki zake zote anazostahili ikiwemo haki
ya kuzungumza mbele ya watu kufuata misingi ya dini. Bi Fatma alienda
kwenye msikiti na kutoa hutuba mbele za watu," alisema
Aliongeza kuwa mwanamke anayo haki ya kurithi, haki ya kuongoza, haki ya
kufanya kazi mbalimbali kwa kuzingatia maslahi na heshima yake kwa
misingi ya dini na sheria