SHEIKH JALALA: TUMUENZI MTUME MUHAMMAD(S.A.W) KWA KUKITHIRISHA MATENDO YA UPENDO, AMANI
| Kiongozi Mkuu wa Waislamu dhehebu la Shia Ithnasheriya Sheikh Hemed Jalala akielezea sherehe za Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) Kwa Waandishi wa habari |
Kiongozi Mkuu wa Waislamu dhehebu la Shia Ithnasheriya Sheikh Hemed Jalala ametoa wito kwa Waislamu na wasio Waislamu kufuata nyendo za Mtume Muhamadi kwa kukithirisha matendo ya upendo na Amani kwani njia hiyo inatawafanya watu kuwa kitu kimoja.
Amesema wakati huu jamii ya Kiislamu ikienda kusherehekea mazazi ya Mtume Muhammad, Jumatatu ya Tarehe 12, 2016, watu wanapaswa wafahamu kuwa mtume maisha yake yote alifunza jamii kuhusu kupendana, kuhurumiana.
Amesema matendo ya Mtume yalijikita zaidi kuhakikisha jamii inajawa na upendo, amani, jambo ambalo watu wengi walimpenda hata wale ambao walikuwa na mtizamo tofauti juu ya itikadi ya dini waliweza kumpenda Mtume na kuamua kuweka amana zao katika Nyumba yake.
"Mtume Muhammad aliaminika na kupewa sifa ya Mkweli na kuaminika, alikuwa akisema kweli tupu jambo hilo liliwafurusha umma wengi na wengine kuona ndio sehemu salama ya kuweka amana zao..." Alisema Jalala.
"Mtume Muhammad alihimiza kwa nguvu zake zote, umoja, utulivu, maelewano na amani, mambo hayo kwa sasa yanahitajika sana katika jamii. Tunapaswa kuyaenzi mambo hayo kwa nguvu zetu zote kama watanzania kwani Nchi yetu pia Imejaliwa kuwa na amani."
Mtume Muhammad (S.A.W)alizaliwa tarehe 17 mwezi wa Rabiul awwal, mwaka wa tembo sawa na mwaka 571 H.D, sawa na Tarehe 20,April mwaka 571 H.D. Alizaliwa katika mji wa Makkatul Mukarramah(Makka) ulioko katika Nchi ya Saudi Arabia. Mama yake ni Amina binti Wahabi bin Abdul Manafi na baba yake ni Abdallah bin Abdul Mutwalib bin Hashim Bin Abdul Manaf.