SERIKALI YA MAGUFULI YASITISHA TENA AJIRA,SOMA HAPO KUJUA

WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi,
Profesa Joyce Ndalichako, ametoa masharti mapya ya ajira za ualimu nchini, huku
akisema Serikali haitaajiri walimu wa masomo ya sanaa (arts) kwa kuwa wapo wa
kutosha.
Akizungumza mjini Dodoma jana wakati akifungua
mkutano mkuu wa mwaka wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA),
Profesa Ndalichako, alisema Serikali kwa sasa haiwezi kuajiri walimu wa masomo
hayo kwa kuwa inataka kuajiri walimu wa masomo ya sayansi na hisabati ambao
idadi yao ni ndogo.
“Pamoja na uamuzi huo mpya, ajira za
walimu wapya wa masomo ya sayansi nazo zimebadilika kwani wale wote waliohitimu
ualimu wa sayansi na hisabati, wanatakiwa watume vyeti vyao kabla ya kupangiwa
kituo cha kazi.
“Kuhusu wale walimu wa ‘arts’, kule tuna
walimu wa ziada ambao tutajaribu kuwapanga kutokana na shule, kwani wengi
walikuwa wamepangwa shule moja. Kwahiyo, tutaangalia utaratibu wa kuwapanga
kulingana na mahitaji,’’ alisema Profesa Ndalichako.
Akizungumzia suala la ubora wa elimu nchini, Profesa
Ndalichako aliwataka walimu wakuu hao kuhakikisha wanasimamia ubora wa elimu
kwa kuwa wao ndio wanaowaandaa wanafunzi kabla hawajaenda vyuoni.
“Vilevile pelekeni takwimu sahihi za
wanafunzi waliopo katika shule zenu kuisaidia Serikali katika kupanga bajeti
ili iweze kutoa fedha sahihi.
“Hapa kuna kimbembe, yaani wakati
mwingine huwa najifanya nimepoteza takwimu ya shule fulani, nikiziomba na
kutumiwa, zinakuwa ni tofauti na zile za mwanzo.
“Hili nawaomba mkalisimamie ili iwe
rahisi kwetu kupanga bajeti yenye tija,’’ alisema.
Kuhusu ujenzi wa maabara katika shule za sekondari,
waziri huyo alisema kwamba kutokana na nyingi kukamilika, Serikali itatoa vifaa
vya maabara kuanzia Januari mwakani baada ya kuwa vimeingia nchini kutoka
vilikoagizwa.
Awali, akisoma risala ya walimu hao, Rais wa
TAHOSSA, Bonus Nyimbo, aliiomba Serikali itoe waraka wa kupiga marufuku
matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni kwa kuwa zimekuwa zikichangia kushuka
kwa ufaulu kwa baadhi ya wanafunzi.
“Ili kuboresha elimu, tunaiomba Serikali
itoe waraka wa kupiga marufuku matumizi ya simu kwa wanafunzi kwani simu nyingi
tunazozikamata tunakuta mule hakuna taaluma,’’ alisema
Nyimbo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Global Education
Link, Abdulmalik Molel, ambaye pia kampuni yake ilipewa tuzo ya heshima katika
kuendeleza elimu nchini, alisema ni jukumu la kila mmoja kutimiza wajibu wake
ili kuiendeleza elimu ya Tanzania.
“Kila mmoja anapaswa kutimiza wajibu,
wazazi, walezi na walimu, waambieni wanafunzi wasiwe na ‘expectation’
(matarajio) makubwa kwani wanapokuwa na matarajio hayo, wakienda vyuo vikuu
wanakuwa wasumbufu,” alisema.
Wakati hayo yakiendelea, juzi taarifa ilitolewa
jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Ufundi, Maimuna Tarishi, ikisema kwamba, walimu wahitimu wa masomo ya sayansi
na hisabati waliohitimu shahada na astashahada mwaka 2015, wanatakiwa
kuwasilisha nakala za vyeti vya elimu ya sekondari vya kidato cha nne na sita
na taaluma ya ualimu kwa uhakiki.
Pamoja na hayo, hivi karibuni Serikali ilitangaza
kusitisha ajira zote nchini ili kukabiliana na wimbi la watumishi hewa.
Sambamba na uamuzi huo, nyongeza za mishahara kwa
watumishi wa Serikali nazo zilisimamishwa ili kukabiliana na watumishi hao hewa
ambao walikuwa wakiingizia hasara Serikali.