HOMA YA UCHAGUZI YAREJEA TENA,NEC YATANGAZA RASMI TAREHE NA SEHEMU ZA UCHAGUZI,SOMA HAPO KUJUA
Na Eliphace Marwa – MAELEZO
TUME ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza ratiba ya
uchukuaji wa fomu za kujaza nafasi zilizo wazi ya Mbunge na Madiwani katika
maeneo mbalimbali hapa nchini.
Imesema kuwa inatarajia kuendesha Uchaguzi Mdogo
katika Jimbo la Dimani , Mkoa wa Mjini Magharibi ,Tanzania Zanzibar kufuatia
kifo cha Mbunge wa Jimbo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari
iliyotolewa Jana jijini Dar es salaam na
Tume hiyo, hatua hiyo itanatokana na vifungu vya 37(1)(b) na 46(2) vya sheria
ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na Vifungu vya 13(3) na 48(2) vya Sheria ya
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Sura 292.
Aidha ,Tume hiyo pia itaendesha Uchaguzi Mdogo wa
kujaza nafasi za wazi za Udiwani katika kata 22 kwenye baadhi ya Halmashauri za
Tanzania Bara zilizokuwa wazi kutokana na sababu mbalimbali.
Imezitaja Kata hizo Ng’hambi ya Halmashauri ya
Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Ihumwa ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma,
Kiwanja cha Ndege ya Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Igombavanu na Ikweha
za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa pamoja na Ngarenanyuki
iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Meru Mkoani Arusha.
Kata nyingine ni Kijichi ya Halmashauri ya Manispaa
ya Temeke Mkoani Dar es Salaam, Kata ya Kinampundu ya Halmashauri ya Wilaya ya
Mkalama Mkoani Singida, Isegehe ya Halmashauri ya Mji wa Kahama Mkoani
Shinyanga, Kasansa Halmashauri ya Wilaya ya Mpimbwe Mkoani Katavi, Malya na
Kahumulo Mkoani Mwanza, Maguu na Tanga Mkoani Ruvuma pamoja na Kata ya Kimwani
Mkoani Kagera.
Imeongeza kuwa Kata nyingine ni pamoja na Nkome
Mkoani Geita, Kata ya Lembeni Mkoani Kilimanjaro, Mkoma ya Mkoani Mara, Duru ya
Mkoani Manyara, Mwamtani ya Mkoani Simiyu, Misugusugu ya Mkoani Pwani pamoja na
Mateves ya Mkoani Arusha.
Tume hiyo imesema kuwa zoezi la kutoa fomu za uteuzi
litaanza Desemba 10 hadi 22 na kufuatia kwa zoezi la uteuzi wa wagombea siku ya
tarehe 22 mwezi Desemba na Desemba 23 hadi Januari 21 mwakani itakuwa ni
kipindi cha kampeni ambapo Januari 22 mwakani itakuwa siku ya kupiga kura.