CHAMA CHA CUF CHAIINGIZA UKAWA MAJARIBU TENA,UCHAGUZI WA JIMBO WAANZA KULETA MASHAKA,LIPUMBA ATAJWA KUWA NI KIKWAZO,SOMA HAPO KUJUA
Mgogoro wa uongozi unaoendelea ndani ya chama cha
CUF huenda ukaathiri ushiriki wake kwenye uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika
Januari 27 baada ya pande zote mbili zinazosigana kujiandaa kuteua wagombea.
Mbali ya mgogoro huo kuhofiwa kukiathiri chama
pengine hadi kusababisha wagombea wake kuzuiwa, pia unaweza kuudhoofisha Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Habari kutoka ndani ya chama hicho zinasema upande
wa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa
vyama vya siasa uko kwenye maandalizi ilhali ule wa Katibu Mkuu, Seif Sharrif
Hamad unatarajiwa kukutana na watendaji wa chama kujadili ushiriki wao.
Profesa Lipumba aliyeiongoza CUF tangu mwaka 1995,
alijiuzulu kwa hiari uenyekiti wake Agosti 2015 lakini siku chache kabla ya CUF
kuitisha mkutano Agosti mwaka huu wa kujadili barua yake, aliandika barua ya
kutengua kujiuzulu na akarejea kazini.
Siku ya mkutano mkuu uliofanyika Ubungo Plaza,
wajumbe waliridhia kujiuzulu kwake lakini walipoingia kuchagua mrithi wake,
wafuasi wa Profesa Lipumba walivamia mkutano na kuuvuruga hali iliyosababisha
baadaye kusimamishwa kwake.
Alipoulizwa jana namna CUF yenye mgogoro
itakavyoshiriki uchaguzi wa madiwani katika kata 22 Bara na ubunge wa Jimbo la
Dimani, Zanzibar, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi CUF, Julius Mtatiro
alisema wapo katika mikakati kuhakikisha wanashiriki kikamilifu.
Mtatiro alisema muda wowote kuanzia sasa Katibu
Mkuu, Maalim Seif atakutana na watendaji wa chama kujadili kwa kina suala hilo
na kutoa maelekezo.
“Tutashiriki vizuri na niwaweke wazi Watanzania kuwa
shughuli za chama zinaendelea kama kawaida hivyo kamati za utendaji zitatimiza
wajibu wake wa kuwapitisha wagombea watakaojitosa kwenye kinyang’anyiro,”
alisema.
Kuhusu Profesa Lipumba, Mtatiro alisema, “Hatuwezi
kufanya kazi na mtu wa CCM kumsogeza karibu yetu ni kumleta atuharibie chama
jambo ambalo hatuwezi kuliruhusu. Ingekuwa lile suala la kujiuzulu aliteleza
tungemwelewa na kumsamehe lakini inavyoonekana yupo kwenye mipango yake katu
hatuwezi kumuweka karibu.”
Lakini Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CUF
anayemuunga mkono Lipumba, Abdul Kambaya alisema, “Tuna kikao leo (jana) upande
wa Bara chini ya Mwenyekiti Profesa Lipumba kujadili suala hilo la uchaguzi,
kuhusu upande wa Zanzibar sifahamu chochote.”
Akizungumzia uchaguzi huo mdogo, Naibu Katibu Mkuu
wa Chadema upande wa Zanzibar, Salum Mwalimu alisema Ukawa utakuwa bega kwa
bega na CUF katika uchaguzi huo kwani wanaitambua kuwa iko moja si mbili kama
inavyotengenezwa na watu wasiopenda maendeleo ya chama hicho.
“Tunatambua na kuheshimu uamuzi wa wanachama na
viongozi halali wa chama, CUF iko moja, kama kuna mtu anatengeneza propaganda
alifanya hivyo akiamini anakwenda kukiua chama ajue bado kinaendelea kusimama,”
alisema.
“Pale atakaposimamishwa mgombea kutoka chama hicho
Ukawa tutamuunga mkono na kumpigania kuhakikisha anashinda. Tunaamini pia nao
watafanya hivyo akisimamishwa mgombea wa Chadema, ”alisema Mwalimu
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi Juju Danda alisema
mgogoro wa CUF hautaleta changamoto yoyote kwenye Ukawa kwa kuwa wanamtambua
katibu mkuu. Alisema Ukawa unamtambua Maalim Seif na ndiye mtendaji mkuu wa
chama hivyo watakuwa tayari kushirikiana naye katika kila jambo.
Kuhusu mpasuko unaoendelea ndani ya chama hicho,
Danda alisema suala hilo waachiwe CUF wenyewe ndiyo watakaoamua. “Mtendaji Mkuu
wa chama ni katibu si Mwenyekiti, na kwa kuwa tupo pamoja na Maalim hatuoni
changamoto yoyote yeye ndiye anayesimamia uteuzi na tunategemea mambo
yatakwenda sawa,” alisema.
Katika hatua nyingine hatima ya Jaji Sekieti Kihiyo
anayesikilkiza kesi ya CUF kujitoa sasa itajulikana Desemba 14 atakapotoa
uamuzi wa maombi ya wadai kumtaka ajiondoe.
Jaji Kihiyo alipanga kutoa uamuzi wa maombi hayo
dhidi yake jana baada ya kumaliza kusikiliza hoja za pande zote katika kesi
hiyo, ambazo zilizua mvutano mkali baina ya mawakili wa wadai kwa upande mmoja
na mawakili wa wadaiwa pamoja na Jaji Kihiyo kwa upande mwingine.
Kesi hiyo imefunguliwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi
ya Wadhamnini wa CUF, dhidi ya Profesa Lipumba, Naibu Katibu Mkuu wa chana
hicho Bara, Magdalena Sakaya pamoja na wanachama wengine tisa waliosimamishwa
uanachama wa chama hicho.
Wengine ni Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi, ambaye ndiye mdaiwa wa kwanza katika kesi hiyo na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali (AG), ambaye ni mdaiwa wa pili.
Kesi hiyo ilitarajiwa kusikilizwa jana lakini kabla
ya kuendelea, kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai, Juma Nassoro aliieleza
mahakama kuwa wadai wameandika barua wakimtaka jaji ajiondoe kuendelea na kesi
hiyo kwa maelezo hawana imani naye.