GAVANA WA BENKI KUU APINGANA NA RAIS MAGUFULI,NI KUHUSU KUHIFADHI FEDHA KWENYE MABENKI,SOMA HAPO KUJUA
Sakata la Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweka
fedha katika akaunti maalumu kwenye benki za biashara limechukua sura mpya
baada ya Gavana wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu kusema si kosa
kisheria.
Profesa Ndulu, ambaye ni mmoja wa wajumbe wa Bodi ya
TRA iliyovunjwa na Rais John Magufuli Jumapili iliyopita, alisema mjini Arusa
jana kuwa hakuna hasara kiuchumi kuweka fedha kwenye akaunti maalum isipokuwa
hilo suala lilikuwa na hali nyingine.
Japokuwa Profesa Ndulu hakutaka kufafanua zaidi kwa
maelezo lilichomekewa tu katika mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea hali
ya uchumi, alisema hali hiyo ndiyo suala lililozungumzwa na siyo kusema “fixed
deposit account” ni mbaya.
“Kwani amesema fixed account zote ni
mbaya, pamoja na za watu binafsi? Ndo hivyo sasa. Nilijua mtachomekea hilo kwa
hiyo nilikuwa tayari,” alisema mhadhiri huyo wa zamani wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Profesa Ndulu alisema hayo alipokuwa akijibu maswali
ya waandishi wa habari walipotaka kujua athari za kiuchumi kwa taasisi za umma
kuweka fedha kwenye akaunti maalumu tena benki binafsi.
Kauli hii ya Profesa Ndulu imekuja siku moja baada
ya Rais Magufuli kueleza kilichochangia kuchukua uamuzi wa kutengua uteuzi wa
Mwenyekiti wa Bodi, Bernard Mchomvu na pia kuivunja bodi yake iliyokuwa na
wajumbe tisa. Kati ya wajumbe hao tisa, watano wanaingia kwa mujibu wa sheria
na wanne ni wa kuteuliwa.
Wajumbe wanaoingia kwenye Bodi kwa mujibu wa sheria
ni Gavana wa BoT, Profesa Beno Ndulu; Kamishna Mkuu wa TRA, Alphayo Kidata;
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha wa Jamhuri ya Muungano, Doto James; Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha Zanzibar, Khamis Mussa Khamis; na Katibu Mkuu Mipango. Bodi
hiyo ilivunjwa Jumapili iliyopita.
Rais Magufuli alisema juzi kuwa Bodi ya TRA
iliyokuwa na watendaji hao wakuu wa idara na taasisi za Serikali ilifanya
dhambi ya kuidhinisha uamuzi wa menejimenti kuweka mabilioni ya shilingi katika
benki za binafsi.
“Juzi hapa tumekuta Sh26 bilioni
zilizokuwa zimetolewa TRA kwa ajili ya matumizi ya TRA zikapelekwa kwenye
mabenki matatu kama ‘fixed deposit account’ na bodi ikapitisha. Ndiyo maana
nilipozipata hizo hela; hela nikazichukua na bodi kwaheri,”
alisema Rais Magufuli alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu
Huria cha Tanzania (OUT) yaliyofanyika mjini Kibaha mkoani Pwani ambako jumla
ya watu 4038 walihitimu shahada mbalimbali
Ukwasi wa mabenki
Katika hatua nyingine Profesa Ndulu amesema ukwasi
wa fedha katika mabenki umeshuka ikilinganishwa na kipindi cha nyuma hatua
inayotatiza utoaji wa mikopo ya muda mrefu kwa ajili ya uwekezaji nchini.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mara baada
ya kufungwa mkutano wa 18 wa taasisi za fedha uliofanyika kwa siku mbili jijini
Arusha alisema hali hiyo inafanyiwa kazi na wadau wa taasisi hizo ili kuja na
mbinu kufanya kuwa endelevu kwani uchumi unategemea uwekezaji unaotegemea
mikopo ya muda mrefu.
Profesa Ndulu alisema BoT itahakikisha inaziwezesha
benki kuendelea na jukumu lao la kutoa mikopo pia kuwa wabunifu wa kutafuta
pesa kwa ajli ya amana badala ya kutegemea Serikali pekee.
“Benki zinaweza kukusanya amana kwa
kiwango kikubwa lakini kama nilivyosema jana (juzi) kuwa katika kila Sh60 kati
ya Sh100 zipo kwenye mikono ya watu badala ya kuwekwa akiba benki hivyo ni
muhimu zikawekwa mbinu ya kuzipata kwa ajili ya kuwawezesha wawekezaji
kuzitumia kwenye uzalishaji,” alisema.
Alisema katika kufanikisha mpango huo lazima kuvutia
mitaji kutoka nje kwani hakuna nchi yoyote duniani inayoweza kupiga hatua kwa
kutegemea fedha za maendeleo na uwekezaji zitokane na mapato ya ndani pekee
akitolea mfano wa China kuwa ni mfano uchumi wake kutegemea mitaji inayotoka
nje ya nchi hiyo.
Katika hatua nyingine Profesa Ndulu alisema
amekubaliana na wadau wa sekta ya fedha kuongeza nguvu katika kutoa mikopo na
kuboresha mifumo ya taarifa kwa wale wanaotaka mikopo kwa ajili ya kilimo
katika mnyororo mzima wa thamani kuanzia uzalishaji hadi kufika kwenye soko.
Profesa Ndulu alisema Tanzania imekaa vizuri
kijiografia kufanya biashara na nchi zisizo na bahari zikiwemo Malawi, Uganda,
DRC na Zambia katika kuwezesha sekta ya fedha kusaidia eneo la usafirishaji,
bandari kufanya kazi na huduma kutolewa inavyotakiwa.
Mwenyekiti wa wenye mabenki ambaye ni Mkurugenzi
Mkuu wa Benki ya CRDB, Dk Charles Kimei amesema waendeshaji wa mabenki
wamenufaika na kuelewa mikakati na fursa za Serikali ambayo itawawezesha wao
kutoa fedha kwa wafanyabishara.
Alisema wao kama CRDB wameweza kukusanya amana za
Sh500 bilioni zinazokopeshwa kwa wafanyabiashara katika kipindi cha miaka
miwili iliyopita na kufungua matawi madogo madogo 100 nchi nzima.
Dk Kimei alisema serikali inapobanwa kifedha
kutokana na kutegemea mashirika ya umma inawapa fursa sekta binafsi kupanua
wigo wao kuwafikia wananchi wengi.