MBUNGE KUBENEA AMLIPUA WAZIRI NAPE,SOMA HAPO KUJUA
SAED Kubenea, Mbunge wa Jimbo la Ubungo na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers, wachapishaji wa
magazeti ya MwanaHALISI, MSETO na MAWIO amesema Muswada wa Upatikanaji wa
Habari utakaowasilishwa Bungeni wiki ijayo ‘utaua’ vyombo vya habari, anaandika Charles William.
Muswada huo unaojulikana kama
Sheria ya Huduma za Habari – The Media Services ACT (2016), unatarajia kusomwa
kwa mara ya pili na iwapo utapitishwa, utakuwa mbadala wa Sheria ya Magazeti ya
mwaka 1976 ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na wanahabari kwa miongo mitano
sasa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara eneo la
Manzese, Bakhresa jijini Dar es Salaam, Kubenea amesema muswada huo si tu
utaviathiri vyombo vya habari bali pia utazima sauti za wananchi.
“Muswada huu ni kitanzi cha uhuru wa kupokea na
kusambaza habari unaotajwa katika Ibara ya 18 ya Katiba ya Tanzania, sisi kama
wabunge wa upinzani tutaupinga kwa nguvu zote.
Muswada unasema Ofisa wa Polisi yaani IGP anaweza
kuamuru mtambo uliochapisha gazeti lililofanya kosa au kurusha matangazo
yatakayoonekana maudhui yake yamekiuka sheria uchukuliwa na kutaifishwa hata
kama mtambo huo si mali ya mkosaji,” amesema.
Kubenea pia amepinga suala la kuanzishwa kwa Bodi
Huru ya wandishi wa habari ambayo wajumbe wake watateuliwa na waziri wa Habari,
Vijana, Sanaa na Michezo na kusema bodi hiyo haiwezi kuwa huru na badala yake
itakuwa ikifanya kazi ya kuminya uhuru wa habari.
“Kwanini Bodi ya Wahandisi haiundwi na waziri wa
miundombinu? Kwanini Bodi ya Madaktari au Wafamasia haiundwi na waziri wa afya?
kwanini Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), hakiundwi na waziri wa Katiba
na Sheria lakini Bodi inayoitwa Huru ya waandishi wa habari itaundwa na Nape?”
amesema.
Ameongeza kuwa bodi itakayoundwa na Nape kwa mujibu
wa muswada huo ndiyo itakayokuwa ikitoa leseni kwa waandishi wa habari na
kwamba itakuwa na mamlaka ya kuamua nani apewe leseni hiyo, nani asipewe na
nani anyang’anywe jambo litakaloweza kuleta athari kubwa kuliko hata sheria za
sasa.
“Watakaoathirika si wanahabari tu kwasababu muswada
unasema mtu atakayetengeneza au kueneza taarifa za uongo au uzushi unaoweza
kuwatia hofu wananchi akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua Sh. 10
milioni mpaka Sh. 20 milioni au kifungo cha miaka minne mpaka sita,”
amesisitiza.