ASKALI WA JWTZ WAPANDISHWA MAHAKAMANI KWA MAUAJI,SOMA HAPO KUJUA
ASKARI tisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), wamefikishwa mahakamani wakituhumiwa kwa mauaji ya mkazi mmoja wa Kata ya Chemchem Manispaa ya Tabora.
Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Samson Kabigi, alisoma mashtaka dhidi ya watuhumiwa hao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, Agatha Chigulu.
Alidai kuwa askari hao wote wa Kikosi cha 823 Msange, walitenda kosa hilo Septemba 10, mwaka huu.
Inadaiwa kuwa askari hao waliwashambulia wananchi mjini Tabora baada ya mkesha wa Fiesta.
Askari hao ni MT 109535 Koplo Msafiri Kitwima (26) na MT 92697 Private Thobias Salum (30) wakazi wa Kata ya Chem Chem, MT 114612 Private Shomary Hemed (24), MT 114685 Private Yusuph Muluthary (25) na MT 114110 Private Rajab Mbasa (24).
Wengine ni MT 114142 Private Selestine Machemba (24), MT 114125 Private Said Rashid (27), MT 114118 Private Rogasian Shayo (24) na MT 114684 Private Yustin Mwingira (24), ambao wote ni wakazi wa Kikosi cha 823 Msange.
Mwendesha Mashtaka Kabigi, alidai washtakiwa wote kwa pamoja Septemba 10, mwaka huu saa 9.00 mchana walimuua Omary Shaban.
Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa vile shauri lao litasikilizwa na Mahakama Kuu. Walirudishwa makabusu hadi Oktoba 5, mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa tena.