MAUZA UZA TUPU USAFIRI WA MABASI YAENDAYO KASI,SOMA HAPO KUJUA
IKIWA ni siku tano kupita baada ya mabasi ya mwendo
kasi kuanza kusafirisha abiria katika Jiji la Dar es Salaam, hali ya vituo
vyake inatisha, anaandika Happiness Lidwino.
Baadhi ya vituo hivyo vinatoa
harufu kali, vimeenea mikojo, kinyesi na takataka ngumu ambapo Halmashauri ya
Jiji la Dar es Salaam na manispaa husika vimedai kutohusika na usafi wake.
Miongoni
mwa vituo alivyotembelea mwandishi wa habari hii ni pamoja na Moroco
(Kinondoni), Kinondoni B, Manyanya na Kimara Baruti ambapo vituo hivyo vimekuwa
na hali inayotia shaka usalama wa abiria wanaotumia vituo hivyo kusubiri
usafiri.
Gatson
Makwembe, Msemaji wa Jiji alipoulizwa kuhusu ufuatiliaji wa usafi kwenye vituo
hivyo baada ya hali kuwa mbaya, amedai jiji halihusiki.
“Mimi
siwezi kuzungumzia suala hilo kwani sisi halituhusu labda uwatafute Dart au
Msemaji wa Manispaa ya Kinondoni,” amesema Makwembe.
Sebastian
Mhowera, Ofisa Uhusiano wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni alipoulizwa,
alidai kazi ya Manispaa ya Kinondoni ni kusimamia usafi wa barabarani pekee.
“Sisi
kazi yetu ni kusimamia usafi barabarani ndani ya manspaa hii na sio uchafu
uliopo ndani ya vituo vya mabasi ya UDA. Siwezi kuzungumzia uchafu uliopo kwenye
nyumba ya jirani,” amesema.
Alipotafutwa
William Gatambi, Msemaji wa Kampuni ya Dart inayosimamia UDA hakupatikana
kujibu aliye na dhamana ya kufanya usafi kwenye vituo hivyo.
Hali
ya wasiwasi inaendelea kutawala kwa wananchi kutokana na vituo hivyo kuwa na
hali mbaya, kukosa ulinzi na hata kugeuka kuwa maeneo ya vibaka, mateja na
watoto wa mitaani kupata hifadhi ya usingizi.
Kituo
cha Kimara Baruti kimekuwa na mlundikano mkubwa wa watu, harufu mbaya
inayotokana na kinyesi, mkojo huku mwingine ukiwa umefungwa kwenye chupa za
maji na kutupwa hovyo. Uchafu wa kituo hicho unafanana na vituo vingine.
John
Mgonja, mmoja wa abiria aliyekuwa akisubiri usafiri katika Kituo cha Moroco
ameeleza kushangazwa na huduma mbovu za vituo hivyo.
“Kwanini
vituo havina ulinzi, hakuna maji, sakafu chafu, taka ngumu kila mahali na
harufu mbaya mpaka imekuwa kero.
“Sijui
sisi tuna tatizo gani, hivi haya mambo yote hayakuwa kwenye mpango wao. Wao
wanachojua ni kukusanya fedha kwa ajili ya nauli tu?” amehoji Mgonja.
Amesema,
watu wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa, kama amebanwa na haja na vyoo vipo
kwake anaona ni bora kikudhi haja yake kwanza mengine mbele kwa mbele.
“Sasa
kama umefika hapa na umebanwa kwanini usijisaidie, lakini hata kama utaacha
vyoo vichafu nani atakukamata? Hakuna mlinzi na hakuna usalama wowote,”
amesema.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni