LIPUMBA AIPASUA CUF,SASA YAIBUKA MKUNDI MAKUBWA,SOMA HAPO KUJUA
NDANI ya Chama cha Wananchi (CUF) kuna makundi
mawili makuu, moja likimtaka Prof. Ibrahim Lipumba aliyekuwa Mwenyekiti wa
chama hicho na lingine likitaka atoswe, anaandika Happiness Lidwino.
Taarifa kutoka ndani ya chama
hicho zinaeleza kuwa, kundi linalotaka atoswe limedhamiria kuvunja katiba huku
kundi linalotaka arejeshwe kwenye nafasi hiyo limeapa kusimama na katiba ya
chama hicho.
Taarifa
zaidi zinaeleza kwamba, kundi linalotaka atoswe linafanya mkakati wa kuvunja
Katiba ya mwaka 1992 Toleo 2013 Ibara ya 117 inayoeleza kwamba, “… kama
hakuainisha tarehe ya kujiuzulu kwake basi mara baada ya katibu wa mamlaka
iliyomteua ama kumchagua kupokea barua hiyo na kumjibu.”
Taarifa
zinaeleza kuwa, maombi ya Prof. Lipumba kujiuzulu yalimfikia katibu wa mamlaka
ambaye ni Maalim Seif Shariff Hamad na kwamba, kwa mujibu wa ibara hiyo,
alipaswa kupeleka maombi hao katika Mkutano Mkuu wa chama hicho kuijadili barua
hiyo na baadaye kujibu baada ya Mkutano Mkuu kujadili jambo ambalo mpaka sasa
halijafanyika.
Prof.
Lipumba aliteuliwa kutwaa nafasi hiyo na Mkutano Mkuu mwaka 1999. Ibara hiyo
inaipa mamlaka mkutano huo kukubali ama kukataa kujiuzulu kwake.
“Kwa
mujibu wa Katiba ya CUF Prof. Lipumba bado ni mwenyekiti wa CUF. Uenyekiti wake
unakoma pale tu katibu wa mamlaka (baada ya Mkutano Mkuu) kuridhia maombi yake
ya kujiuzulu na kumjibu kwa barua, Prof. Lipumba mpaka sasa hajajibiwa,”
ameeleza mjumbe mmoja wa Mkutano Mkuu aliyeomba kuhifadhiwa jina lake na kuongeza;
“Watu
walidhibitiwa sana kwenye mapato ya chama ndio maana wanataka asirudi, hili
ndio linalosababisha hata kutaka kuvunja Katiba. Lakini cha kujiuliza kwanini
wanataka kukwepa ibara ya 117? Wanajua kwenye Mkutano Mkuu wajumbe hawawezi
kukubali.”
Kwa
mujibu wa taratibu za CUF, Baraza Kuu halina mamlaka ya kukubali ama kukataa.
“Mpaka
sasa katibu wa mamlaka halijaleta taarifa ama maombi ya kujiuzulu kwa Prof.
Lipumba, tunaisuburi ije na hakuna chochote kitakachofanyika mpaka utaratibu
huu ufuatwe. Hatopatikana mwenyekiti mwingine mpaka taarifa hiyo itufikie,”
amesema.
Mvutano
wa CUF umedhihiri juzi kwenye kongamano lililoandaliwa na Kata ya Makurumla
Manispaa ya Kinondoni ambapo wajumbe waliibua hoja ya ukimya wa taarifa kuhusu
maombi ya kujiuzulu ya Prof. Lipumba.
Katika
kongamano hilo, Mohamed Mgomvi, mmoja wa wanachama wa CUF alisema, upande wa
bara chama hicho kimebaki kwenye uyatima na kwamba hakuna mtu madhubuti
anayeweza kukiendesha kama Prof. Lipumba.
“Nashangaa
viongozi wetu mnasema habari zisizoeleweka juu ya kujiuzulu kwa Lipumba badala
ya kusema ukweli nini kinaendelea huko ndani, tangu alipoondoka Lipumba hakuna
maendeleo alafu mnasema tupo pamoja naye, haiingii akilini hata kidogo,”
alisema.
Maganga
Dachi, mwanachama wa CUF katika mkutano huo pia alisema, kwa mujibu wa Katiba
ya CUF, barua ya kujiuzulu inatakiwa ifike katika Mkutano Mkuu uliomchagua
jambo ambalo halijafanyika.
“Kwa
hatua hiyo chama kinavunja Katiba maana hadi leo hakuna kinachoendelea kama
hivyo suala la Lipumba, linatakiwa kuwasilishwa kwenye Mkutano Mkuu nasi
tunamtaka Lipumba arudi katika nafasi yake ili chama kiendelee na shughuli za
kimaendeleo,” alisema Dachi.
Ushawishi
ndani ya chama hicho unaendelea kufanywa na baadhi ya wanachama pia viongozi wa
chama hicho kumrejesha Prof. Lipumba kwenye nafasi hiyo.
Prof.
Lipumba alijiuzulu nafasi yake mwaka jana kwa madai ya kutoridhishwa na uamuzi
wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuridhia Edward
Lowassa kuepusha bendera ya umoja huo kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2015
kupitia Chadema.
Akizungumza
na MwanaHALISI Online leo
Sheweji Mketo, Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi na Mipango wa CUF amesema, kwa
mujibu wa Katiba ya CUF, Prof. Lipumba anayo nafasi ya kurejea kwenye nafasi
hiyo.
Mketo
amesema, Katiba ya chama inamruhusu mwanachama aliyejiuzulu uongozi kurudi
kuwania tena nafasi yoyote kwani kujiuzulu ni haki ya mwanachama.
Akijibu
hoja ya Prof. Lipumba kurejea kwenye nafasi hiyo amesema, “anaruhusiwa kurudi
kama kawaida, atajaza fomu za kuomba kuwania uongozi na atapigiwa kura na
baraza la chama kama wagombea wengine.”
Amesema
utaratibu wa chama hicho katika kumpata mwenyekiti ni kuitisha Mkutano Mkuu
ndani ya miezi sita ili kumchagua mwenyekiti mpya.
“Tatizo
ni kwamba, mpaka hadi sasa bado hatujafanya kikao kutokana na kukosa fedha
hivyo chama kimeongeza miezi mingine sita ambapo mkutano mkuu unatarajiwa
kufanyika Oktoba mwaka huu,” anasema.
Post Comment
Hakuna maoni
Chapisha Maoni