OMBENI SEFUE AICHIA IKULU KISHINGO UPANDE,SOMA HAPO KUJUA
Baada ya kudumu Ikulu kwa takribani siku 127 zikiwamo 67 tangu aongezewe muda wa mwaka moja akiwa na Serikali ya Awamu ya Tano, Balozi Ombeni Sefue ameshukuru heshima aliyopewa na Rais John Magufuli kwa muda wote aliomsaidia kutekeleza majukumu yake ya ukatibu mkuu kiongozi na kueleza kuwa Serikali ya sasa ni ya mabadiliko.
Wakati Sefue akiondoka, mhandisi John Kijazi amepokea kijiti cha ukuu wa utumishi serikalini na kuahidi kuwa atafuatilia mazingira ya watumishi wote pamoja na mazingira yao, ili kurekebisha panapohitajika kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na tija kwa wananchi.
Akizungumza muda mfupi baada ya kuapishwa kwa mrithi wake, licha ya kumshukuru Rais, Balozi Sefue aliwataka watendaji wote serikalini kumpa ushirikiano wa kutosha Balozi Kijazi ili kuleta ufanisi kwenye huduma za umma.
“Namshukuru Rais kwa kuniamini kwa kipindi chote nilichodumu naye. Ni heshima kubwa kuwatumikia Watanzania pamoja naye. Nitampa ushirikiano wowote atakaouhitaji katibu mkuu kiongozi mpya kwenye utekelezaji wa majukumu yake,” alisema Sefue.
Rais Magufuli, ameahidi na mara zote amekuwa akisisitiza adhma yake ya kutumbua majipu kwa watumishi wote ambao hawaendani na kasi yake.
Tangu taarifa za mabadilio hayo zilipotangazwa jana, kumekuwepo na tetesi nyingi kuwa huenda Sefue naye ni jipu lilikuwepo ikulu, suala ambalo halikupata maelezo ya kutosha kutoka kwa balozi huyo.
Alipoulizwa juu ya tetesi hizo alijibu kwa ufupi: “Hii ni Serikali ya mabadiliko.”
Kwa upande wake Kijazi, alisema atafanya kazi kwa kuzingatia vipaumbele vya Rais huku akimshauri namna sahihi za kuboresha mazingira ya utumishi serikalini.
Akieleza juu ya majukumu yake mapya, alionyesha kuyatambua ipasavyo na kubainisha kuwa atashirikiana na Baraza la Mawaziri kwenye vikao vyao, bila kusahau kuzifuatilia wizara husika na kuona endapo kila kitu kinaenda kama inavyotakiwa.
“Nitakutana na mawaziri kwenye vikao vyao nitakavyoviandaa. Nitawasiliana na kuwafuatilia watendaji wa wizara husika juu ya masuala yatakayokuwa yamejitokeza ndani ya maeneo yao ya uwajibikaji. Kila mmoja atimize wajibu wake ili Taifa lisonge mbele,”alisema Kijazi.
Ili kuitendea haki hadhi ya utumishi wa umma, Kijazi ameahidi kuhakikisha kila kitu kinasimamiwa kwa ukaribu huku akitoa msisitizo kwenye vipaumbele vya Rais.
“Kwenye suala la mapato na rushwa, nitafuatilia kwa nguvu ili kuongeza uwajibikaji kwa watumishi wa Serikali,” alisisitiza Kijazi.
Balozi Kijazi aliteuliwa juzi kushika nafasi inayoachwa na Balozi Sefue. Kabla ya uteuzi huo, Kijazi alikuwa mwakilishi wa Tanzania kwa nchi za India, Singapore, Sri Lanka, Bangladesh na Nepal huku makazi yake yakiwa jijini New Delhi, India kuanzia mwaka 2007.
Katika wadhifa huo, alikuwa mkuu wa mabalozi wote wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi pamoja na mkuu wa mabalozi wa Afrika nchini India.
Kabla hajateuliwa kuwa mwakilishi wa nchi, Kijazi amekuwa mtumishi serikalini kwa nafasi mbalimbali ikiwamo Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi kuanzia mwaka 2002 mpaka 2006.
Kabla ya hapo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu kati ya mwaka 1996 hadi 2002.
Ndani ya Wizara ya Ujenzi, kabla hajawa katibu mkuu, alikuwa mhandisi mwandamizi wa ujenzi wa barabara kisha kupandishwa cheo na kuwa mkurugenzi wa barabara za mikoa.
Kumbukumbu za taaluma yake zinaonyesha kuwa alipata Sha hada yake ya kwanza ya Sayansi ya Uhandisi wa Umma mwaka 1982 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Shahada ya Uzamili katika Uhandisi wa Barabara kutoka Chuo Kikuu cha Birmingham, Uingereza mwaka 1992.
Jana wakati anaapishwa, saa 4:15 asubuhi, Kijazi alikuwa sambamba na mke wake, Fransiscar Kijazi na kwa pamoja wamejaliwa watoto watatu, David, Emmanuel na Richard.
Kwa heshima ya familia hiyo, baada ya kukamilisha protokali, Rais Magufuli alipiga picha ya pamoja na familia ya mteule huyo mpya atakayehudumu ikulu kuanzia sasa.
Hata hivyo kwa mara ya mwisho, Sefue aliendelea na kazi yake mpaka jana asubuhi na ndiye aliyemkabidhi Kijazi kitabu kitakatifu cha Biblia, Katiba na kiapo cha uongozi ambacho alisaini
Hakuna maoni
Chapisha Maoni