KIINGEREZA KIBOVU CHA RAIS MAGUFULI CHAIBUA JIPU LA MIAKA 50,SOMA HAPO KUJUA
KATI ya mambo mawili
yaliyofanywa na Rais John Magufuli wiki iliyopita, moja lilinifurahisha;
jingine lilinisikitisha. Nitaanza na lililonifurahisha, anaandika
Ansbert Ngurumo.
Rais Magufuli, akiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, alitumia Kiswahili kuhutubia marais wenzake na washiriki
wengine, katika ukumbi wa hoteli ya Ngurdoto, mkoani Arusha.
Alinifurahisha jinsi
alivyotumia fursa hiyo kusisitiza masuala nyeti ambayo, ama angependa
yasimamiwe au yalimkera na aliagiza yasahihishwe.
Rais alisisitiza mambo
kadhaa. Kwanza, alizungumzia haja ya nchi wanachama kuvumiliana, kwani kila
moja ina matatizo yake.
Pili, alisisitiza
umuhimu wa sekretarieti kubana matumizi. Akasema wanatumikia nchi maskini, kwa
ajili ya wananchi maskini; hivyo wanapaswa kufanya kazi wakijielekeza kuokoa
fedha ili kuelekeza nguvu katika huduma.
Alitoa mfano wa
gharama za ukumbi waliotumia kwa ajili ya mkutano huo, katika Hoteli ya
Ngurdoto, akisema hesabu zinaonesha kila mshiriki amelipiwa dola 45.
Akasema kama mkutano
huo ungefanyikia katika Ukumbi wa Mikutano wa Kituo cha Kimataifa cha Arusha
(AICC), kila mjumbe angelipiwa dola 30.
Akatoa mfano kwamba
dola 15 ambazo zingeokolewa zingeweza kusaidia ununuzi wa madawati au kuchangia
gharama za usuluhishi wa mgogoro wa Burundi.
Mambo haya yatakuwa
yamemjengea Rais Magufuli taswira chanya mbele ya wenzake na jamii ya
kimataifa.
Hata wananchi wake
waweza kuwa walijisikia vizuri kwamba rais wao amethubutu kukumbusha wenzake
masuala muhimu waliyopuuza kwa muda mrefu.
Na amefanya hivyo
mapema kabisa mwa kipindi cha uenyekiti wake. Ameweka mweleleko mpya
unaosisitiza utumishi badala ya utawala.
Hata hivyo, licha ya
uzuri wa hoja zake, kuna moja ambalo lilionekana kukera wengi, wakiwamo
wasaidizi wake wa karibu.
Nilibahatika
kuzungumza na baadhi ya wasaidizi wake. Wengine walisema kwa uwazi; wengine
wakakwepa kuzungumza kwa uwazi.
Baadhi ya wasaidizi wa
rais, viongozi wa serikali, na wananchi wasomi makini, wameonekana kuchukizwa
na jinsi Rais Magufuli alivyotupia maneno ya Kiingereza, hapa na pale katika
hotuba yake.
Zipo sababu za mtu
kuonekana amechukia. Mambo mazuri niliyozungumzia hapo juu yangeweza
kusisitizwa vizuri tu kwa Kiswahili bila kuchomeka Kiingereza.
Au kama mzungumzaji
aliamua kuchomeka Kiingereza, basi alipaswa achomeke Kiingereza sanifu.
Yafuatayo ni baadhi ya
maneno ya Kiingereza aliyochomeka Rais Magufuli, ambayo hayakupendeza
wasikilizaji. Ninaweka hapa mifano mitatu:
“…We are supposed to
look each other as one family.”
“Kila siku they come
with a special proposals. And that proposals is always positive proposals. Not
negative proposals…”
Count on me. I don’t know to whom interest…”
Hotuba ya Rais
Magufuli imeibua maneno mengi kutoka kwa watani wake wa kijamii na wa kisiasa.
Nimesikia mmoja
akisema, “…sasa naelewa kwanini rais hakuhudhuria hafla ya mabalozi aliyoandaa
mwenyewe Ikulu mwezi uliopita.”
Mwingine akisema,
“…kumbe ndiyo maana mgombea urais wa UKAWA alipoambiwa mdahalo akasema angeshiriki
kama ungeandaliwa kwa Kiingereza.”
Mwingine akidiriki
kulinganisha Kiingereza cha Jacob Zuma, Rais wa Afrika Kusini, (ambaye hakukwea
madarasa na kutafuna karatasi za vitabu vingi); na kile cha Dk. Magufuli,
mwenye shahada ya tatu – ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mzazi mmoja jijini Dar
es Salaam amesema Kiingereza cha Magufuli kimesababisha ugomvi kati yake na
mtoto wake.
Mzazi huyo
hakufurahishwa na kitendo cha mtoto wake cha kuchambua makosa ya kisarufi
katika “Kiingereza cha rais.”
Hoja yangu ni ipi?
Rais kujua au kutojua Kiingereza? Hapana! CCM ina kigezo cha mgombea urais kuwa
angalau na digrii moja. Hicho ndicho walitumia “kumzuia” Augustine Mrema.
Sasa huyu mwenye
shahada anatarajiwa walau ajue vema lugha mbili kuu, kikiwemo Kiingereza.
Tuangalie hoja zifuatazo:
Kwanza, kwa kuwa rais
amejifunza lugha hiyo na atakuwa ameitumia kujifunzia masomo mengine hadi
kupata digrii ya uzamivu, anapaswa – siyo tu kuielewa bali hata kuiheshimu – na
kuitumia inavyopasa.
Pili, rais hakuwa na
sababu ya kutumia maneno ya Kiingereza. Kama alikuwa ameamua kuchanganya
Kiswahili na Kiingereza, angetumia Kiingereza sanifu.
Tatu, rais kukosea
maneno ya kawaida na kuzungumza Kiingereza “ndivyo-sivyo,” amekuwa mfano mbaya
kwa watoto wanaojifunza lugha hiyo, huku wakigombezwa na walimu wao kwa makosa
ambayo hata rais anafanya.
Nne, washauri wa rais
wamwandalie hotuba. Katika mazingira haya ndipo uzuri wa hotuba zilizoandikwa
unapoonekana. Angeweza kusema maneno haya kwa kuyasoma. Yawezekana hata
Kiingereza kingenyoshwa, kama angetaka kiwemo.
Tano, kwamba mwalimu
wa zamani wa kemia katika shule ya sekondari, ambaye sasa ni msomi wa ngazi ya
shahada ya uzamivu katika kemia, anapokosea vitu vidogo lakini muhimu kama
hivi, hatoi mfano mzuri kwa watoto wetu ambao wanagombezwa na walimu na wazazi
kila wanapokosea Kiingereza kama alivyofanya.
Sita, rais ajenge
utamaduni wa kusikiliza washauri wake Ikulu – kama alikuwa hajajenga tabia
hiyo. Ni kwa njia hiyo aweza kuepuka makosa ya aina inayojadiliwa. Akubali
kusoma hotuba alizoandika au alizoandikiwa na washauri wake.
Saba, ujengwe
utaratibu wa kudumu kwa viongozi wetu kuenzi Kiswahili na kukitumia katika
mikutano ya kitaifa na kimataifa, ndani na nje ya nchi. Kiswahili kimeshakua.
Kama Tanzania tunajiita kitovu cha Kiswahili, tuoneshe kwa vitendo kwamba
tunaweza kuipa dunia lugha ya kazi.
Nakumbuka miaka kadhaa
iliyopita, katika mkutano wa viongozi wa Umoja wa Afrika, wakati Benjamin Mkapa
akiwa rais, alihutubia viongozi wenzake kwa Kiingereza sanifu.
Ilipofika zamu ya Joachim
Chissano, aliyekuwa rais wa Msumbiji, akahutubia kwa Kiswahili mwanzo hadi
mwisho. Tulimsema Rais Mkapa kwamba alikuwa amenyang’anywa fursa adhimu ya
kumiliki Kiswahili na kuonyesha kuwa Tanzania ndiyo kisima cha Kiswahili.
Tangu mwaka 2005,
Kiswahili ni moja ya lugha rasmi za Umoja wa Afrika, kikiwa lugha pekee yenye
asili ya bara hili.
Tunatambua kuwa
viongozi wetu wengi wanajua Kiswahili kuliko Kiingereza.
Ni vema basi watumie
lugha yao kuliko lugha ya kigeni inayowapa shida katika kuwasiliana na wenzao.
Mwaka 2007 nilialikwa
kutoa mhadhara katika Kongamano la Highway Africa, lifanyikalo kila mwaka
katika Chuo Kikuu cha Rhodes, Grahamstown, Afrika Kusini. Mada yangu ilihusu
jinsi ya kublogu kwa Kiswahili.
Katika utafiti wangu,
niligundua kuwa Kiswahili kimekua kuliko wengi wetu wanavyofahamu. Niliwaeleza
wasikilizaji kutoka nchi zote za Afrika kwamba Kiswahili ni moja ya lugha
zinazokua kwa kasi duniani.
Katika Afrika pekee
kilikuwa na wazungumzaji zaidi ya milioni 100. Katika Afrika Kusini mwa Sahara,
Kiswahili ni lugha inayozungumzwa kuliko lugha nyingine zote.
Katika maeneo kadhaa
ya Afrika, Kiswahili kinatumika Tanzania, Kenya, Uganda, Somalia, Kongo (DRC),
Burundi, Rwanda, Msumbiji, Zambia, Malawi, Sudan, Comoro na Malagasy.
Vyuo vikuu zaidi ya
100 duniani vina programu ya kufundisha Kiswahili. Vituo kadhaa vya redio vya
nchi mbalimbali duniani vina idhaa ya Kiswahili.
Mifano michache ni
BBC, Uingereza; Radio Deutsche Welle, Ujerumani; Nippon Hoso Kyokai (NHK),
Japan; Voice of America (VoA), Marekani; Radio China, China; Radio Cairo,
Misri; Radio Moscow International, Urusi; Radio Sudan, Sudan; Channel Africa ya
Shirika la Utangazaji la Afrika Kusini (SABC), Radio France International
(RFI), Ufaransa; na Radio India, India.
Nilipokuwa Uingereza, moja
ya kazi nilizofanya ili kuongeza kipato ni kuwa mfasili wa kazi za Kiswahili
kwenda Kiingereza kwa ajili ya kampuni kadhaa zilizokuwa na mikataba na vyuo
kadhaa vya Marekani katika kukuza Kiswahili.
Kilichonisikitisha ni
kwamba katika mradi huu, tulikuwa wafasili zaidi ya 20 wa Kiswahili kutoka nchi
mbalimbali; lakini mimi ndiye pekee niliyekuwa Mtanzania. Wengine walitoka
Kenya, Afrika Kusini, Canada na Congo.
Wanaosafiri kwa ndege
za KQ – Shirika la Ndege le Kenya – wamekuwa wanasikia Kiswahili chenye lafudhi
na msamiati wa Kenya kwenye matangazo yao. Hata kwenye mitandao, Kiswahili
ambacho kinaonekana kurasimishwa ni cha Kenya, si cha Tanzania.
Sisi tumetumia nguvu
nyingi kung’ang’ania Kiingereza, ambacho watu wetu hawawezi kuzungumza vizuri
kwa kuwa hawakupata msingi mzuri wa kufunzwa lugha hiyo; ingawa imetumika kama
lugha ya kufundishia masomo mengine tangu sekondari hadi chuo kikuu.
Ndiyo, Kiswahili ni
lugha ya taifa tangu 1961. Watanzania wengi wanazungumza Kiswahili. Vyombo
vyetu vya habari vingi, vinaandika au kurusha taarifa za habari na matangazo
kwa Kiswahili.
Tuna BAKITA, Baraza la
Kiswahili la Taifa. Tuna TUKI, Taasisi ya Ukuzaji wa Kiswahili ya Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, ambayo nasikia imekua na kujitanua zaidi.
Tuna miradi mingi ya
kukuza Kiswahili. Lakini tumejifanya wanyonge wa kuenzi Kiswahili. Wakenya sasa
wanaelekea kupora lugha yetu. Tusipostuka, kuna wakati tutajikuta tunakwenda
Kenya kujifunza Kiswahili.
Natambua kuwa mjadala
juu ya lugha ya kufundishia katika shule zetu haujaisha. Wapo wanaotaka
Kiingereza kiendelee kutumika kufundishia watoto wetu. Wengine wanasema
Kiswahili kitumike.
Hoja hiyo itajadiliwa
siku nyingine. Lakini lililo wazi ni kwamba, lolote tutakaloamua halitakuwa na
uzito, halitatekelezeka, iwapo litakosa msukumo wa kisiasa.
Kwa sasa, hatuna
mwingine wa kubeba jukumu hili, bali Rais Magufuli. Alibebe kwa kuazimia na
kuonyesha kwa vitendo kuwa popote atakapokuwa, atahutubia kwa Kiswahili ili
kukidhi matakwa haya na kuepusha adha niliyotaja hapo awali.
Hatua hii itasaidia
kuongeza ajira. Watahitajika wafasili. Yeye azungumze, wengine watafsiri, dunia
isikilize.
Kwetu, au kwa yeyote
anayejua lugha hiyo, Kiswahili ni hazina. Ni soko la ajira. Ni mtaji. Lakini
hakijaweza kutumika kiuchumi kuboresha maisha ya wananchi kwa sababu viongozi
wanakipuuza.
Inasikitisha zaidi
kwamba marais wetu wameshindwa kukuza Kiswahili katika ngazi ya kimataifa.
Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, alikuwa mwandishi na mzungumzaji mahiri wa Kiswahili
na Kiingereza. Lakini alitumia Kiingereza kila alipohutubia jamii ya kimataifa.
Marais Ali Hassan
Mwinyi, na Benjamin Mkapa nao walifuata nyayo za Mwalimu Nyerere. Walihutubia
kwa kusoma hotuba walizoandika au walizoandikiwa na wasaidizi wao – kwa
Kiingereza sanifu.
Mara moja tu, Rais
Jakaya Kikwete, alianza kwa kuhutubia mkutano wa Umoja wa Afrika kwa Kiswahili.
Baadaye naye alitawaliwa na Kiingereza.
Hata hivyo, tofauti ya
marais hao wanne na Rais Magufuli ni uwezo wao wa kumudu lugha hiyo. Hili ndilo
limesababisha mitandao ya kijamii kujadili sana “Kiingereza kibovu cha
Magufuli” na kusahau maudhui ya hotuba yake.
Na huu ndio msukumo wa
ushauri wangu kwa Rais Magufuli. Atutangulie katika mradi mpya wa kukuza na
kueneza Kiswahili duniani.
Kwa kutekeleza mradi
huu, Rais Magufuli atakuwa ametumbua jipu lililoshindikana kwa miaka 55.
Asishindwe.
Uchambuzi huu
umechapishwa kwa mara ya kwanza katika gazeti la MwanaHALISI toleo Na. 329 la
Jumatatu, Machi 7, 2016.
·
·
145
·
·
·
·
Hakuna maoni
Chapisha Maoni