JECHA WA ZEC AZIDI KIPASUA CHAMA CHA ADC,UNDUMI LA KUILI WA HAMAD RASHIDI WAKIMALIZA ,SOMA HAPO KUJUA
Mwenyekiti wa ADC-Taifa, Said Miraji. |
MGOGORO wa
kushiriki ama kutoshiriki uchaguzi wa marudio visiwani Zanzibar unatokota ndani
ya Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), anaandika Happyness Lidwino.
Taarifa zilizopatikana ndani ya chama hicho
zinaeleza kwamba, kumeibuka makundi mawili makubwa ya viongozi.
Kundi la kwanza linahoji sababu za kukubali kuingia kwenye
marudio ya uchaguzi huo uliotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar
(ZEC), Jecha Salim Jecha kufanyika tarehe 20 Machi mwaka huu.
Kundi la pili linaloonekana kubebwa na aliyekuwa mgombea urais
wa chama hicho, Hamad Rashid likitaka kushiriki uchaguzi huo bila kujali
kufutwa kwa uchaguzi wa awali kulizingatia sheria ama la.
Jecha alifuta uchaguzi huo tarehe 28 Oktoba mwaka jana kwa madai
ya kuwepo kwa kasoro, hata hivyo tayari vyama 10 kati ya 14 vimegoma kushiriki
uchaguzi huo kwa madai ya kutoona sababu ya kurudiwa.
Hata hivyo, kinachoonekana kuvuruga zaidi chama hicho ni kuwepo
kwa taarifa za mmoja wa viongozi wa chama hicho kurubuniwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) ili kushawishi kukubali kuingia kwenye uchaguzi huo kwa ahadi
kupewa bahshishi.
Mtandao huu ulimtafuta Said Miraji, Mwenyekiti wa ADC-Taifa
kujua ukweli wa taarifa hizo, awali alipopokea simu na kujibu “nipo kwenye
kikao, nitafute baada ya saa moja.”
Alipopigiwa kwa mara ya pili akionesha kuwa na haraka, alikiri
kuwepo kwa mgogoro ndani ya chama hicho na kwamba, anaandaa taarifa kwa ajili
ya kupeleka katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Hakusema ni taarifa ipi.
“Niko busy (nimebanwa) sana kwanza chama changu mpaka sasa bado
kipo kwenye utata, kwa sasa siwezi kukujibu.
“Na hapa kuna maelezo naandaa, yanatakiwa kupelekwa kwa msajili
wa vyama vya siasa sasa hivi, simu yako nimepokea kwa kukuheshimu tu,” amesema
Miraji.
Ndani ya chama hicho, Miraji amekuwa akishutumiana vikali na
Hamad kwa madai kwamba, anatumika na CCM katika kuhakikisha chama hicho
kinashiriki uchaguzi.
Mmoja wa viongozi wa chama hicho aliyetaka jina lake kutoandikwa
amesema “viongozi wanatofautiana na kinachoonekana hapa kuna fedha imetumika.
Upo ushawishi unaoendelea tena kwa kutumia fedha ili chama kishiriki uchaguzi
lakini wanaosema hivyo hawaelezi sababu za kushiriki uchaguzi huo.”
Chanzo hicho kimeeleza kuwa, “wanaosimamia msimamo huo
wanashindwa kutoa sababu za msingi ili kuhalalisha hoja yao. Kinachoonekana ni
kwamba wengine wana kisasi na CUF hivyo wamekuwa wepesi kutumika, lakini bado
tunapambana kugomea uchaguzi. Ngoja tuweke mambo sawa.”
Hamad aliyejiunga na ADC tarehe 23 Julai mwaka jana baada ya
kufukuzwa na Chama cha Wananchi (CUF) kwa tuhuma za usaliti, pia amekuwa
akihusishwa na ubadhirifu wa fedha ndani ya chama hicho.
Hamad na Miraji wote walikuwa wanachama wa CUF ambapo kila mmoja
aliondoka kwa sababu zake na kukutana kwenye chama hicho ambacho inadaiwa
kwamba, Hamad alikuwa na mkono wake katika kuanzishwa kwake.
Miraji amekuwa akiongoza harakati za kumng’oa Hamad ndani ya
chama hicho kwa madai bila kufanya hivyo, ADC haitakuwa salama.
Mpaka sasa, ushiriki wa vyama vya ADC na Chama Cha Kijamii (CCK)
kwenye uchaguzi huo upo njiapanda kutokana na wagombea wake kutangaza kushiriki
licha ya vyama vyao kuwa na msimamo tofauti. Vyama ambavyo vimetangaza
kushiriki marudio hayo hadi sasa ni CCM, Tadea, TLP, Sau na AFP.
Kwa kipindi cha miezi miwili iliyopita, Zanzibar imeendelea kuwa
kwenye mgogoro wa kisiasa baada ya CUF ambayo ni moja ya chama kinachounda
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kususia marudio ya uchaguzi baada ya ule wa
awali kufutwa na ZEC.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni