Zinazobamba

JAJI LUBUVA AZIDI INGIWA UWOGA KUHUSU ZANZIBAR,SOMA HAPO KUJUA


Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC)
Jaji Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC)
HALI ya hofu visiwani Zanzibar kuhusu marudio ya uchaguzi imeendelea kukata mioyo ya baadhi ya watendaji wa serikali akiwemo Jaji Mstaafu, Damian Lubuva ambaye ni Mwenyekiti wa Taifa wa Tume ya Uchaguzi (NEC). Anaandika Dany Tibason.
Licha ya Tume ya Uchaguzi Zaznibar (ZEC) kutangazwa kwa tarehe ya marudio ya uchaguzi kuwa 20 Machi mwaka huu, Jaji Lubuva amesisitiza kuwepo kwa ulazima wa vyama vikubwa kukaa meza moja na kufikia mwafaka.
Jaji Lubuva amasema hayo leo Dodoma mbele ya waandishi baada ya kufungua mkutano wa tathimini wa asasi za kiraia kuhusu elimu ya mpiga kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Amedai mgogoro wa Zanzibar unaweza kutatuliwa na ZEC pekee na si kiongozi mwingine na kuongeza Rais wa Jamhuri ya Tanzania na Rais wa Zanzibar hawana uwezo wa kutatua mgogoro huo.
Ikiwa tayari Chama cha Wananchi (CUF) kimetengaza kususia uchaguzi huo, Jaji Lubuva ameonesha haja ya kuwepo kwa mazungumzo na chama hicho ili kukaa meza moja na kuangalia namna ya kutatua mgogoro huo.
Alipobanwa na wanahabari kwamba, kuna madhara gani kwa CUF kususia uchaguzi Zanzibar, Jaji Lubuva alijinasua kwa kusema, ‘ipo haja ya vyama hivyo kukaa pamoja na kuafikiana ili kuweza kuunda uongozi wa umoja wa kitaifa.’
Amesisitiza kwamba, suala la uchaguzi na malumbano yanayoendelea visiwani Zanzibar yanaweza kutatuliwa na ZEC pekee.
Hata hivyo, wakati akifungua mkutano huo Jaji Lubuva aliwataka wanasiasa walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu uliopita wajipange kwa ajili ya uchaguzi wa 2020 na si kuzungumza maneno ambayo hayana tija kwa taifa.
“Uchaguzi umeisha wanasiasa msiwapotoshe wananchi, walioshinda wameshinda na walioshindwa wameshindwa sasa tujipange kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Wanaotoa hukumu kwenye uchaguzi ni wananchi wenyewe sio Tume kwani wananchi kwa utashi wao huchagua wanayemtaka,” asema Jaji Lubuva.
Amesema katika Uchaguzi Mkuu uliopita NEC haikuwa na chama wala haikupendelea chama chochote bali ilifanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu za nchi.
‘’Hatukupendelea mtu wala chama, watumishi wa tume walifanya kazi kwa kufuata kanuni na taratibu na katika hili niwapongeze wafanyakazi wote wa Tume popote walipo,’’amesema.
Amesema “hakuna hata mgombea mmoja aliyekwenda tume kuonesha ushahidi kuwa aliibiwa kura, kama ulishinda na kuibiwa kura, ushahidi uko wapi mbona hukuleta? Lakini bado unaongelea kuwa uliibiwa kura” alihoji Jaji Lubuva.
Amesema mwaka 2010 watu milioni 20 walijitokeza kujiandikisha lakini waliopiga kura ni milioni nane.
Pia mwaka 2015 jumla ya watu waliojiandikisha walikuwa milioni 22 lakini waliopiga kura ni milioni 15.

Hakuna maoni