NI BAJETI YA POSHO NA MISHAHARA TU,MIPANGO YAMAENDELEO YAPEWA PESA KIDUCHU,SOMA HAPA KUJUA
SAADA Mkuya- Waziri wa
Fedha na Uchumi, ametoa mwelekeo wa bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha
2015/2016, akisema itaweka kipaumbele katika kugharamia uchaguzi mkuu na
kukamilisha miradi inayoendelea na kuweka msukumo maalum kwenye miradi ya umeme
vijijini, maji vijijini na kuimarisha rasilimali watu. Anaandika
Pendo Omary … (endelea).
Akitoa mwelekeo huo leo jijini Dar es Salaam
mbele ya wabunge, Mkuya amesema jumla ya matumizi ya bajeti hiyo itakuwa ni Sh.
22.4 trilioni, likiwa ni ongezeko la asilimi 16 ya bajeti ya mwaka 2014/2015 ya
Sh. 19.6 trilioni.
“Serikali
itaendelea na juhudi za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuchukua
hatua mbalimbali za kisera na kiutawala kwa lengo la kuongeza mapato kwa
kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya mapato,” amesema Mkuya.
Amesema hatua hizo
ni;- Kusisitiza matumizi ya vifaa na mifumo ya kielektroniki ili kuongeza
ufanisi katika ukusanyaji na kudhibiti upotevu wa mapato;
Kuhakikisha kuwa
taasisi, wakala, mamlaka zinazojitegemea na mashirika ya umma yanakusanya
ipasavyo mapato yasiyo ya kodi ili kupunguza utegemezi kutoka serikali kuu na
kuwasilisha ziada kwenye mfumo mkuu wa serikali;
Kuendelea kuchukua
hatua za kudhibiti misamaha ya kodi; Kuboresha mazingira ya kufanya biashara
ili kuwezesha urasimishaji wa shughuli za biashara na kupanua wigo wa kodi;
Kupitia upya baadhi ya
viwango vya kodi, ada na tozo mbalimbali ili viendane na hali halisi ya utoaji
wa huduma husika;
Kuboresha mfumo wa
ukusanyaji wa kodi za majengo na kupitia upya viwango vya kodi ili zitozwe kwa
kuzingatia thamani ya jingo badala ya utaratibu wa sasa wa viwango sawa;
Kuendelea kutafuta
mikopo kutoka ndani na nje ya nchi kugharamia bajeti ya maendeleo kwa
kuzingatia uhimilivu wa deni la taifa.
Mkuya amesema kwa
kuzingatia sera za uchumi jumla pamoja na misingi na sera za bajeti kwa mwaka
2015/2016, sura ya bajeti inaonesha jumala ya Sh. 22,480.4 bilioni zinatarajiwa
kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.
“Jumla ya mapato ya
ndani yanatarajiwa kuwa Sh. 14,824.4 bilioni, sawa na asilimia 57.8 ya bajeti
yote. Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumala
ya Sh. 13,353.4 bilioni sawa na asilimia 90.1 ya mapato ya ndani,” Mkuya
amesema.
Aidha, mapato yasiyo
ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh. 949.2 bilioni na Sh.
521.9 bilioni. Serikali inategemea kukopa Sh. 5,767.8 bilioni kutoka vyanzo
vyenye masharti ya kibiashara.
Pia, washirika wa
maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh. 1,888.2 bilioni sawa na asilimia 8.4 tu ya
bajeti ikilinganishwa na asilimia 14.8 ya bajeti ya mwaka 2014/2015 ambazo
sehemu kubwa ni mikopo ya masharti nafuu.
“Kwa upande wa
matumizi, katika mwaka 2015/2016 serikali inapanga kutumia jumla ya Sh.
22,480.4 bilioni kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, Sh.
16,711.2 bilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh.
6,612 bilioni kwa ajili ya mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi,”
amesema Mkuya
Katika bajeti hiyo,
Sh. 2,600 bilioni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali
zinazoiva. Matumizi ya maendeleo yatakuwa Sh. 5,769.2 bilioni sawa na asilimia
25.9 ya bajeti yote ambapo kiasi cha Sh. 4,327.8 ni fedha za ndani sawa na
asilimia 75 ya fedha za maendeleo.
Mkuya amesema
“shabaha na misingi ya bajeti kwa mwaka 2015/2016 inalenga: kuongeza kasi ya
ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.2 mwaka 2015 kwa kutumia
takwimu zilizorekebishwa za mwaka wa kizio wa 2007”.
Aidha, kuendelea
kudhibiti kasi ya mfumko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa
tarakimu moja;
Kuongeza ukusanyaji wa
mapato ya ndani ikijumuisha mapato ya Halmashauri kufikia asilimia 15.7 ya pato
la taifa; kuongeza mapato yatokanayo na kodi kufikia asilimia 14.2 ya pato la
taifa;
“Matumizi ya serikali
yanatarajiwa kuwa asilimia 20.7 ya pato la taifa; Kupunguza nakisi ya bajeti
(ikijumuisha misaada) hadi kufikia asilimia 3.6; Kasi ya ukuaji wa ujazi wa
fedha kwa tafsiri pana zaidi kuwa asilimia 16 mwezi Juni 2016,” amesema Mkuya.
Ameongeza kuwa mikopo
kwa sekta binafsi itakuwa kwa asilimia 19.5 ya pato la taifa mwezi Juni 2016;
Kupunguza nakisi
katika urari wa malipo ya nje ya kawaida unaojumuisha urari wa biashara ya
bidhaa, huduma, mapato na vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida (current
account balance including transfers) kufikia asilimia 10.7;
Pia, kuwa na akiba ya
fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na
huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne.
“Changamoto katika
utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2014/2015 ni;- Kutokufikia malengo ya kukusanya
mapato ya kodi na yasiyo ya kodi kwa kiwango kinachotakiwa; Wafanyabiashara
kugomea matumizi ya mashine za kielektroniki za ulipaji kodi (EFD’s),”
ameongeza Mkuya.
Amezitaja changamoto
zingine ni;- “Mapato ya ndani na nje kutokupatikana kama ilivyokadiriwa; Sera
kulazimika kutoa fedha kwa mashirika ya umma ya biashara kama vile ATCL, TRL na
TAZARA na hivyo kuongeza gharama ambazo zimepaswa kulipwa na mashirika
yenyewe”.
Pia, mahitaji makubwa
ya kuboresha miundombinu hususan ya maji, reli, bandari, viwanja vya ndege na
barabara ili kukuza uchumi na kuongeza ajira na mchakato mrefu wa kupata mikopo
ya kibiashara.
“Mikakati ya
kukabiliana na changamoto hizo, serikali itaboresha na kuimarisha mifumo ya
ukusanyaji na usimamizi wa mapayo; Kuendelea kusisitiza matumizi kulipa kodi na
tozo mbalimbali kwa kutumia mitandao ya kielektroniki,” ameongeza Mkuya.
Mikakati mingine ni
kuhakikisha kwamba hakuna kuingia mikataba mipya ya miradi na huduma bila kuwa
na uthibitisho wa kuwepo kwa fedha; Kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji
kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa ubia kati ya sekta binafsi na sekta ya umma;
Kuimarisha mchakato wa
kutathiminiwa kwa uwezo wa serikali wa kukopesheka na hivyo kuingia kwenye soko
la fedha la kimataifa kukopa kwa masharti bora zaidi;
Kukamilisha uandaaji
wa kanuni za utekelezaji wa Sheria ya Bajeti na kuendelea kuimarisha mfumo wa
kieletroniki wa usimamizi wa malipo (IFMS).
Akizungumzia kuhusu
bajeti hiyo, Esther Bulaya, Mbunge wa viti maalum (CCM), amesema “zaidi ya
asilimia 60 ya bajeti iliyopita haijatekelezwa. Mwaka jana Miradi ya
maendeleo ilitegwa trilioni sita, zimetoka trilioni mbili. Deni la taifa
linaongezeka kutoka trilioni 18 hadi 19. Bajeti ya mwaka huu ni ngumu na haina
matumaini.”
Chanzo
ni Gazeti la Mwanahalisi.oline
No comments
Post a Comment