HABARI KUBWA, KASHFA NZITO MBUNGE WA CCM,ATESA WATU HOVYO SOMA HAPA KUJUA
MBUNGE wa Bukoba Vijijini, Jason Rweikiza
(CCM) (pichani)anatuhumiwa kutumikisha wafanyakazi katika shule yake ya Rweikiza English
Medium and Nursery School kwa kutokuwapo mikataba ya ajira.Anaandika Edson Kamukara … (endelea).
Kutokana na hilo,
wafanyakazi ambao ni pamoja na walimu wapatao 30, hawalipi kodi (PAYE),
hawachangii mafao ya pensheni katika mfuko wowote wa jamii; na wanawake
hawapati likizo ya uzazi.
Shule hii ipo eneo
la Kyetema-Mchangani, yapata kilometa 15 nje ya mji wa Bukoba, kwenye barabara
iendayo Biharamulo.
Rweikiza ni
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala ambaye wafanyakazi
wake wanadai “angekuwa anaelewa na kuthamini haki.”
Wafanyakazi hao, wasio na mikataba ya ajira, wasiolipa
kodi ya PAYE na wasiopata likizo ya uzazi; ndio wameiwezesha shule ya Rweikiza,
iliyoanzishwa mwaka 2010, kuwa na ufaulu wa juu katika matokeo ya mtihani wa
Darasa la Saba.
Katika matokeo ya
2014, shule hii imekuwa ya kwanza kati ya shule 145 za wilaya ya Bukoba Vijijini;
ikaibuka ya pili kati ya shule 909 za mkoa wa Kagera na ya 13 kitaifa kati ya
shule 15,867.
“Tunaogopa kudai haki
zetu kwa nguvu. Tutafukuzwa kazi. Lakini kubwa zaidi ni kutopata hata nafasi ya
kuzungumza na Rweikiza kuhoji unyanyasaji huu,” ameeleza mwalimu.
Mkuu wa shule
hiyo, Baraka Mwambinga anakiri Rweikiza kutokutana na wafanyakazi. Anasema
“…hajataka kukutana nao, ila simu yake iko wazi na namba yake wanaijua;
anayemhitaji anaweza kumpigia simu wakati wowote.”
Lakini Rweikiza
hakubaliani na madai hayo. Katika mahojiano na gazeti hili amesema, “NSSF na
Bima ya Afya wanazo. Wanapata likizo za uzazi na wanalipwa. Mishahara ni ya
kawaida – mikubwa na midogo – kutegemea kazi ya mtu, elimu, madaraka, uzoefu,
uwezo wa kulipa na mengineyo.”
Chanzo changu kimedokezwa
kuwa wafanyakazi wa shule ya Bukoba ndio pekee wenye malalamiko. Wenzao katika
shule tatu za Rweikiza za jijini Dar es Salaam “hawasikiki kudai chochote.”
Rweikiza
anamiliki pia shule za msingi na sekondari za St. Anne Maria, Sunshine na
Brilliant zilizopo Dar es Salaam.
“Hatuna mikataba ya
ajira. Makubaliano yanafanyika kwa mdomo. Mshahara wa chini hapa kwa mwezi ni
Sh. 200,000 na kima cha juu ni Sh. 350,000 kwa walimu,” ameeleza mwalimu
mwingine.
Amesema watumishi
wengine – wapishi, mweka fedha, mhasibu, madereva, walinzi, wafanya usafi na
matroni – nao wanalalamika kama walimu; lakini viwango vyao ni vya chini kuliko
vya walimu.
“Fikiria mtu anayepata
mshahara wa Sh. 100,000. Atoe nauli ya Sh. 2,000 kwa siku (sawa na sh. 60,000)
kwa mwezi… anabaki na nini? Rweikiza haruhusu mfanyakazi kupanda gari la shule.
Akibainika anafukuzwa kazi,” analalamika mfanyakazi.
Wafanyakazi wanaelewa
kuwa sheria ya ajira inataka mfanyakazi mjamzito apewe likizo ya uzazi ya miezi
mitatu na malipo; “…lakini hapa mzazi anapewa mwezi mmoja na ukiisha haruhusiwi
kuja na mtoto kazini, isipokuwa atakwenda kunyonyesha saa nane mchana.”
Lakini lini
wafanyakazi wamekutana na Rweikiza na mara ngapi kumweleza matatizo yao?
“Utaanzia wapi? Anakuja hapa. Anazunguka eneo lake lote; kisha anazungumza na
‘watu wake’ na kuondoka,” anaeleza mwalimu.
Taarifa za shuleni
hapo zinaeleza kuwa suala la kutolipa michango NSSF lilifichuka baada ya
watendaji wa shirika hilo kutembelea shule 28 Februari mwaka huu, na
kuwaelimisha wafanyakazi kutambua wajibu wa mwajiri kupeleka michango hiyo.
“Tulipigwa butwaa.
Tukauliza haki hizi tutazipataje ikiwa hatuna mikataba ya maandishi wala
vitambulisho vya kazi. Tuliwaeleza NSSF kwamba hata mishahara imeanza kupitia
benki Mei 2014; awali tulipokelea dirishani,” ameeleza mfanyakazi.
Kwenda kwa NSSF
shuleni Bukoba sasa kumeamsha watumishi. Kuna taarifa kuwa wanapanga kuiomba
serikali kuingilia kati ili wapate kile walichokwishapoteza na kuwekwa
utaratibu utakaowahakikishia haki.
Angalia hata hili, mfanyakazi
anaonesha kitanda katika bweni, “Idadi ya wanafunzi imeongezeka. Watoto
wanalazwa kitandani wawili-wawili. Ni rahisi hata kuambukizana magonjwa.”
Mwalimu mkuu wa
shule, Baraka Mwambinga ameiakiambia Chanzo changu, “…kuhusu NSSF, ni kweli
hazikuwa zikipelekwa; lakini hivi karibuni tumeanza kufanya utaratibu.”
Alipoulizwa iwapo
haoni ni kinyume cha taratibu za ajira, alisema “…unajua, awali shule ilianza
kama huduma kwa majirani wasio na uwezo wa kupeleka watoto katika shule za nje
za gharama kubwa. Sasa tumepanuka tunaboresha.”
Kuhusu wanafunzi kulazwa wawili-wawili kitanda
kimoja, Mwambinga alisita kidogo, kisha akasema madai ya wanafunzi “kulazwa
wawili-wawili siyo ya kweli. Tuna vitanda vya kutosha…hilo tatizo halipo.”
Kuhusu walimu,
Mwambinga amesema waliomweleza mwandishi kinachoitwa malipo duni kwa walimu,
walimwambia uongo. “…hapa walimu wanalipwa vizuri na kupata haki zao zote.”
Chanzo changu klipomtafuta
Rweikiza kwa simu hakupatikana; simu ilikuwa ikiita bila kupokelewa. Lakini
alipopelekewa ujumbe wa simu, alifunguka.
Akijibu malalamiko ya
wafanyakazi, Rweikiza aliandika sms, “…licha ya kuwa mimi ni mwanasheria
mwandamizi, ni mtu mwenye umri mkubwa, ni kiongozi mkuu wa kisiasa na kijamii.
Hakuna wanafunzi wanaolala wawili kitandani.”
Aliandika, “Hakuna
dhuluma nyingine au yoyote ile; hayo unayosema yangekuwa ya kweli au hata nusu
yake, shule isingekuwa bora kama ilivyo hadi inakuwa ya kwanza wilayani na
mkoani ya 11 kati ya shule 16,000 Tanzania nzima.”
“Wafanyakazi
wasingekuwa na ari ya kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa. Baadhi ya wafanyakazi
wanapewa nyumba za shule bure bila malipo. Wanapewa chakula cha mchana bure
bila malipo,” alieleza.
Katika majibu hayo kwa
njia ya sms, Rweikiza anasema kama wafanyakazi wangekuwa wanafanyiwa “dhuluma”
wasingekubali kuajiriwa au kuendelea kuajiriwa kwa sababu ni hiari yao na
hawashurutishwi.
“Pia wafanyakazi
wanaopata matokeo mazuri katika kazi zao wanalipwa bonasi kubwa-kubwa kulingana
na matokeo ya kazi zao,” amesema.
Uchunguzi wa Chanzo changu umebaini kuwa
wafanyakazi wanaopewa nyumba za shule bure ni walimu wanane tu; tena wanaotoka
Uganda. Hawa wanapewa pia chakula cha mchana bure.
Ada ya mwanafunzi wa
kutwa na wa bweni, wa madarasa ya awali katika shule yake, ikiwa ni pamoja na
usafiri, haizidi Sh. 1,300,000.
Ada kwa darasa la
kwanza hadi la saba zinatofautiana, lakini hazizidi Sh. 1,500,000 kwa mwaka kwa
kila mwanafunzi.
Chanzo ni
Gazeti la Mwanahalisi.oline
No comments
Post a Comment