WASAKA URAIS WA CCM.WAMALIZA VIFUNGO VYAO,NAPE ASEMA WASUBIRI RUNGU JINGINE,SOMA HAPA KUJUA
KIFUNGO cha miezi 12 walichopewa makada sita wa CCM kwa kukiuka kanuni na taratibu za chama hicho na kuanza kampeni za kuwania urais kabla ya wakati, kinamalizika ndani ya saa 24 na hatma yao kusubiri tathimini itakayofanywa na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo walitekeleza ipasavyo adhabu hiyo au la.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alithibitisha jana kuwa muda wa adhabu hiyo unaelekea ukingoni na kufafanua kuwa viongozi hao watafanyiwa tathmini na kamati ndogo ya maadili ili kubaini kama walitekeleza ipasavyo adhabu hiyo.
Makada hao walipewa adhabu hiyo ya onyo kali na Kamati Kuu Februari 18, mwaka jana baada ya kuthibitika kuanza kampeni za kutafuta kuteuliwa kugombea urais kabla ya wakati kinyume na kanuni za uongozi na maadili za CCM Toleo la Februari 2010, Ibara 6(7)(i).
Vilevile baada ya kuhojiwa, walithibitika kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na baadhi yao kufanya vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya jamii.
Kutokana na adhabu ya onyo kali makada hao kwa mwaka mzima walikuwa katika hali ya kuchunguzwa ili kuwasaidia katika jitihada za kujirekebisha.
Pia kamati ndogo ya udhibiti iliagizwa kuwachunguza na kuchukua hatua kwa wote waliohusika kwa namna moja au nyingine (mawakala na wapambe), kufanyika kwa vitendo hivyo vilivyovunja kanuni za chama.
Makada hao waliokuwa chini ya adhabu hiyo ni Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Kwa nyakati tofauti jana, makada hao walizungumza na Chanzo change na kueleza kuwa wanasubiri kauli ya chama hicho baada ya adhabu yao kumalizika.
Kauli ya Nape
Akizungumza na Chanzo changu jana Nape alisema, “Kanuni zetu zipo wazi. Adhabu ikimalizika itafanyika tathmini ili kubaini utekelezaji wa adhabu kwa wahusika.”
Hata hivyo, Nape alisema hakuna muda maalumu wa kufanya tathmini hiyo na kusisitiza kuwa inaweza kufanywa kwa siku moja, wiki au miezi, “Itategemea kazi yake itamaliza lini. Kamati ikimaliza kazi yake itawasilisha ripoti katika vikao vya juu vya chama.”
Nape alisisitiza kuwa adhabu kwa viongozi hao ilianza pale ambapo waliambiwa kuwa wamepewa adhabu, alipotakiwa kutaja tarehe ambayo walianza adhabu hiyo alisema kuwa haikumbuki, ila ilikuwa mwaka jana mwezi kama huu.
Kuna baadhi wameanza kupanga kufanya mikutano Februari 19 wakiamini kuwa adhabu inaisha Februari 18. Sijui tarehe hii wameitoa wapi,” alisema Nape.
Februari 13, mwaka huu Kamati Kuu ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete ilifanya kikao chake Kisiwandui, Zanzibar na kuagiza adhabu kali zichukuliwe dhidi ya wale watakaobainika kuwa walikiuka masharti ya adhabu waliyopewa.
Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula ambaye kamati anayoiongoza ndiyo iliyopewa kazi ya kufanya tathmini hiyo, alipotafutwa na gazeti hili jana alisema asingeweza kuzungumza chochote kwa kuwa alikuwa safarini.
Huenda baadhi yao wakakumbwa na rungu jingine kutokana na madai yaliyokuwa yakitolewa na wanachama wa chama hicho, kwamba baadhi yao waliendeleza kampeni za chini chini.
Kwa nyakati tofauti wagombea hao waliwahi kuzungumzia juu ya adhabu hizo huku Membe akisema adhabu hiyo ilikuwa mwafaka na kwamba laiti uamuzi huo usingefanywa mapema, “ingekuwa vurugu tupu”. “Sijui nchi hii ingekuwa wapi kama watu wangeachwa bila ya kuwekewa ‘gavana’,”
Sumaye ambaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1995 hadi 2005, mwezi mmoja baada ya kupewa adhabu hiyo alikata rufaa kuipinga. Hata hivyo, rufaa hiyo haijawahi kusikilizwa.
Kauli ya Sumaye
Akizungumza na Chanzo changu, Sumaye aliendelea kusisitiza kuwa licha ya kukata rufaa hajawahi kusikilizwa na alipoulizwa endapo kuna hatua zozote atakazochukua alisema anachosubiri sasa ni kauli ya chama juu ya adhabu aliyopewa.
“Mpaka sasa bado rufaa yangu haijasikilizwa. Kuhusu muda wa adhabu ni kweli kuwa unamalizika kesho ila siwezi kusema chochote kwa sababu chama ndiyo kinatakiwa kutoa tamko rasmi,” alisema.
Alisisitiza kuwa atakuwa na mengi ya kuzungumza baada ya kusikia msimamo wa chama chake juu ya adhabu hiyo.
Makamba
Kwa upande wake Makamba alisema, “Nafarijika kwamba kipindi cha uangalizi kimeisha. Naamini sikustahili adhabu niliyopewa lakini niliitii.”
Alisema kuwa kipindi hicho kilikuwa kigumu na kwamba wakati mwingine alilazimika kukataa mialiko ya shughuli za kijamii kwa hofu kwamba isije kutafsiriwa kwamba ni kampeni.
“Nilifadhaishwa na mambo mawili; kwanza baadhi ya makada walishiriki kwenye kikao cha kutupa adhabu kumbe na wenyewe wana nia ya kugombea. Pili, Wakati wengine tuko kwenye adhabu kuna makada wengine walikuwa wanafanya kampeni waziwazi, wanagawa pesa, wanafanya vikao na mambo mengine yaliyokatazwa,”
“Matumaini yangu ni kwamba hawa nao, bila kujali nyadhifa zao, wataadhibiwa ili kujenga misingi ya haki na usawa ndani ya chama chetu.”
Makamba ambaye tayari ametangaza nia ya kugombea urais alisema nyakati zijazo wana-CCM wanaotaka uongozi waruhusiwe kutangaza nia zao mapema ili waweze kuchambuliwa na kuonekana wanaofaa na wasiofaa.
“Kugombea nafasi kubwa hakupaswi kufanywa kwa kificho na mafumbo kama vile tunatafuta mchawi maarufu miongoni mwetu. Lakini pia ni vyema kwamba wale wanaobainika kutumia pesa au siasa ya kibaguzi wafutwe kabisa uanachama bila woga wala kusitasita,” alisema.
Ngeleja
Mbunge huyo wa Sengerema alisema, “Binafsi naona kama bado adhabu haijaisha na ninalazimika kuendelea kutekeleza maagizo ya chama,”
Alifafanua kuwa pale ambapo CCM itatoa maelekeo baada ya kufanya tathimini ya adhabu waliyopewa ndiyo utakuwa muda mwafaka wa kuzungumzia suala hilo.
“Chama kitatoa tamko rasmi na hilo ndiyo linalosubiriwa ili kujua hatua zaidi. Kifupi ni kwamba sikuwahi kwenda kinyume na maagizo ya chama,” alisema.
Lowassa
Mbunge huyo wa Monduli simu yake iliita bila kupokewa lakini msaidizi wa Lowassa, Aboubakar Liongo alikiambia Chanzo changu kwamba kiongozi huyo hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo na kusisitiza kuwa wanaopaswa kuulizwa ni CCM.
Chanzo
Ni Gazeti la Mwananchi
Hakuna maoni
Chapisha Maoni