WANAFUNZI WA CHUO CHA IFM WAMUANGUKIA LOWASSA,WASEMA YAO SOMA HAPA KUJUA
Wanafunzi wa Chuo cha
Usimamizi wa Fedha (IFM) jijini Dar es Salaam wametangaza azma yao ya kumuunga
mkono Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa (pichani), iwapo ataamua kugombea
urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Wamesema wataanza kutekeleza azma yao hiyo kwa vitendo kwa
kumsindikiza atakapokwenda kuchukua fomu za kukiomba ridhaa chama chake ya
kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Kauli hiyo ilitolewa na Mbunge wa Bunge la Serikali ya Wanafunzi
wa Chuo hicho, Hafsa Masumai, kwa niaba ya wenzake, alipozungumza na waandishi
wa habari, jijini Dar es Salaam juzi.
Mkutano huo na wanahabari, ambao ulifanyika ndani ya eneo la
IFM, ulihudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa serikali ya wanafunzi na wanafunzi
wa chuo hicho.
Alisema wanamuunga mkono Lowassa kwa kuwa ni miongoni mwa
viongozi watetezi wa masuala ya elimu.
“Wanafunzi wamekuwa wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ambazo
zimekuwa sugu hata kutatuliwa na serikali, ikiwamo mikopo kwa wanafunzi wa
elimu ya juu,” alisema Masumai.
Aliongeza: “Tutamuunga mkono Lowassa, kwani ni kiongozi, ambaye
anaonekana kujali elimu na tunaamini anaweza kutatua matatizo haya, ambayo
yamekuwa yanatukabili kwa muda mrefu.”
Alisema Lowassa mbali na kuwa kiongozi aliyetetea elimu pia
amekuwa akisaidia vijana katika nyanja mbalimbali, ikiwamo kuwasaidia kwenye
vikundi vyao na kujikwamua dhidi ya makali ya maisha.
Masumai alisema kuachwa vijana hao vijiweni, kunaweza
kukawafanya wajiingize kwenye makundi ya ujambazi, uvutaji unga na sehemu za
hatari kwa maisha yao.
“Lowassa ni kiongozi wa pekee, ambaye anaweza kutusaidia vijana
na kututetea kielimu. Na sisi kama vijana, tutamuunga mkono na tutahakikisha
tunamsindikiza kuchukua fomu ya urais,” alisema Masumai.
Alisema endapo Lowassa atafanikiwa kupata nafasi hiyo, wanaamini
kuwa vijana watapata haki zao za msingi pamoja na kuboreshewa elimu katika
ngazi zote.
Kwa mujibu wa Masumai, vijana wamekuwa wakisahaulika kwenye
nafasi mbalimbali na kwamba, hilo lisipoangaliwa na kutiliwa mkazo na serikali
watakuja kupata makundi ya uhalifu.
Alisema makundi hayo yamekuwa yakifumbiwa macho bila kuangalia
njia ya kuwawezesha kwa ngazi mbalimbali.
“Sisi kama vijana tumeona umuhimu wa Lowassa katika kipindi cha
uongozi wake alipokuwa waziri mkuu. Hivyo, tuna imani hata akipata nafasi ya
urais, tuna hakika kuwa vijana tutapata haki zetu,” alisema Masumai.
Hata hivyo, wanafunzi hao hawakufafanua kama katiba ya serikali
yao ina kipengele kinachoruhusu viongozi kutangaza misimamo ya kuamua nani wa
kumuunga mkono katika chaguzi za kisiasa.
Lowassa ni miongoni mwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
ambaye anatajwa kujitosa katika kinyang’anyiro cha kuwania urais katika
uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Hata hivyo, hadi sasa Lowassa mwenyewe kwa kinywa chake
hajatangaza kama atawania urais katika uchaguzi huo.
Badala yake, mara zote, ambazo amekuwa akiulizwa kuhusiana na
hilo, amekuwa akijibu kwa kifupi kuwa: “Huwezi kuvuka daraja kabla
hujalifikia.”
Hadi sasa makada wa CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania
urais kupitia chama hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na
Mawasiliano, January Makamba; Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Mbunge wa
Nzega, Dk. Hamis Kigwangallah; Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda na Waziri wa
Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu.
Wanaotajwa kuwania nafasi hiyo ya juu kuliko zote nchini ni
Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William
Ngeleja.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe; Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na
mawaziri wakuu wastaafu, Lowassa na Frederick Sumaye.
Wanatajwa pia Spika wa Bunge, Anne Makinda; Waziri wa Katiba na
Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu),
Prof. Mark Mwandosya na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu),
Stephen Wasira.
Kati ya makada hao, sita waliwahi kuitwa na Kamati Ndogo
ya Nidhamu iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara,
Philip Mangula na kuwahoji kwa tuhuma za kuanza kampeni za uchaguzi mkuu ujao
kabla ya wakati.
Baada ya mahojiano hayo, Februari, mwaka jana, Kamati Kuu
(CC) ya CCM ilitangaza uamuzi mzito dhidi ya makada wake hao baada ya kutiwa
hatiani, kwa kuwafungia kugombea nafasi za uongozi ndani ya chama hicho kwa
miezi 12, huku pia wakiwa chini ya uangalizi. Siku za kifungo hicho
zilikamilika jana.
Makada hao ni pamoja na Sumaye, Lowassa, Membe, Wasira,
Ngeleja na Makamba, ambao wanakisubiri chama kutangaza hatma yao wakati wowote
kuanzia sasa baada ya kipindi cha uangalizi kupita.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni