UTEUZI WA MAKONDA WAPINGWA KILA KONA,WASOMI WALIA NA JK,WASEMA MAZITO SOMA HAPA KUJUA
Pichani ni Makonda picha na maktaba |
Wasomi, wanasiasa na
wanaharakati nchini, wamepokea kwa hisia tofauti uteuzi alioufanya na Rais
Jakaya Kikwete, wa wakuu wa wilaya wapya, huku baadhi wakikosoa uteuzi wa mkuu
mpya wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda na wengine wakiunga mkono.
Juzi Rais
Kikwete aliteua wakuu wa wilaya wapya 27, akiwamo Katibu wa Umoja wa Vijana wa
CCM (UVCCM) Uhamasishaji na Chipukizi, Makonda, kuwang’oa 19 na kuwahamisha 64.
Wakizungumza kwa
nyakati tofauti na Chanzo changu jana, badhi walisema Rais Kikwete amefanya
jambo la busara kuboresha utendaji kazi serikalini, lakini wakasema kumpa
Makonda wadhifa huo kunaweza kudhoofisha utendaji wa kazi katika wilaya
ya Kinondoni.
PRO. BAREGU
Aliyekuwa mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Prof. Mwesiga Baregu, alisema Makonda alituhumiwa kumfanyia fujo aliyekuwa
Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, lakini hakuna hatua zozote
zilizochukuliwa dhidi yake.
Kutokana na hali hiyo, alisema ni jambo la kushangaza kuona mtu
mwenye tuhuma za kufanya fujo anateuliwa kuwa mkuu wa wilaya, ambaye atakuwa
mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
“Hakuna uchunguzi wa polisi au kiusalama juu ya Makonda.
Kutochukuliwa hatua kunadhihirisha mambo aliyoyafanya aliagizwa,” alisema Prof.
Baregu.
Alisema uteuzi huo wa wakuu wa wilaya wapya unaweza ukawa kinga
kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujiimarisha katika uchaguzi mkuu na kura ya
maoni za katiba inayopendekezwa.
MUKOBA
Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Gratia Mukoba, alisema
Rais Kikwete amefanya kitendo kizuri kuteua wakuu wa wilaya, lakini akasema
kitendo cha kumpa Makonda ukuu wa wilaya ya Kinondoni siyo chema.
Alisema Makonda amepewa wilaya kubwa na hana uzoefu wowote wa
kuongoza wilaya, kwani hajawahi hata kuongoza kata.
Mukoba alisema yawezekana Rais Kikwete amemteua Makonda kutokana
na fujo anazozifanya, ikiwamo inayodaiwa kumfanyia Jaji Warioba.
“Sijawahi kumsikia akiongoza hata kata. Sana sana amewahi
kuongoza Tahliso (Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu). Mtoto mdogo
kama yule kumfanyia fujo mzee kama yule aliyeliletea sifa taifa na leo anakuwa
mkuu wa wilaya ni jambo la kushangaza sana,” alisema Mukoba.
DK. BANA
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson
Bana, alisema uteuzi wa wakuu wa wilaya ni mzuri, kwani rais ndiye mwenye
mamlaka ya uteuzi.
Alisema japokuwa muda ni mdogo uliobaki wa kiutendaji wa kazi
kwa wakuu hao wa wilaya wapya, changamoto kwao ni kuhakikisha mafanikio
yanapatikana kwa wakati.
Dk. Bana alisema nafasi ya ukuu wa wilaya ni ya kisiasa zaidi,
hivyo CCM wanajipanga kwa uchaguzi mkuu ujao.
KIJO-BISIMBA
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Hellen Kijo-Bisimba, alisema uteuzi huo wa wakuu wa wilaya wapya, CCM
wanaweka makada wao mapema ili kujipanga na uchaguzi mkuu pamoja na kura ya
maoni.
Alisema kulikuwa hakuna sababu ya Rais Kikwete kuweka wakuu
wapya wa wilaya wakati muda wa kumaliza uongozi wake umebaki mdogo.
RAIS TLS
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Charles
Rwechengura, alisema Rais Kikwete anapaswa kupongezwa kwa uteuzi huo, kwani
amefuata vigezo vya uteuzi wa wakuu wa wilaya, hivyo kumteua Makonda kuwa mkuu
wa wilaya siyo kosa.
“Kisheria iko ivi, kama Makonda alifikishwa mahakamani
akatuhumiwa kumfanyia fujo Jaji Warioba, basi ni makosa kuwa mkuu wa wilaya,
lakini kama hakushitakiwa popote haina shida,” alisema Rwechengura
MNYIKA
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
Tanzania Bara, John Mnyika, amesema mabadiliko ya wakuu wa wilaya ni mkakati wa
CCM kupitisha katiba inayopendekezwa kinyemela.
Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema uamuzi wa Rais
Kikwete kupangua safu hiyo una lengo la kuhujumu upinzani kuelekea uchaguzi
mkuu zaidi kuliko ufanisi wa utendaji wa serikali.
Katika taatifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema
kuhamishwa vituo kwa wakuu wengi wa wilaya miezi michache kabla ya kura ya
maoni ya katiba inayopendekezwa na uchaguzi mkuu, ni mkakati wa wakuu hao ambao
ni makada wa CCM kushinikiza Watanzania kupigia kura ya ndiyo katiba hiyo.
Alisema uteuzi huo unapaswa kuibua mjadala wa haja ya
kufuta vyeo vya wakuu wa wilaya kwa Watanzania.
Alisema Watanzania wanatakiwa kutoshiriki kupiga kura ya maoni
ya katiba inayopendekezwa kwa sababu imeendeleza mianya ya nafasi hizo kutumika
kwa siasa chafu za hujuma za CCM.
“Badala yake wananchi wajiandikishe kwa wingi kwa ajili ya
uchaguzi mkuu kupiga kura kuiondoa CCM madarakani ili katiba mpya ikamilishwe
na Rais mpya, serikali mpya, Bunge jipya na Bunge Maalumu jipya kwa kuzingatia
maoni ya wananchi,” alisema Mnyika.
Alisema mpango huo ni wa kuendeleza mianya ya nafasi hizo
kutumika kwa siasa chafu nchini.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni