SERIKALI YA KIKWETE INANUKA UFISADI TU,PAC,LAAC YAIBUA MADUDU KILA KONA ,SASA MAWAZIRI WENGINE KUJIUZULU,SOMA HAPA KUJUA
Pichani ni Rais Jakaya Kikwete picha na maktaba |
Ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma ulioibuliwa katika taarifa ya
mwaka ya Kamati za Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Bunge ya Hesabu
za Serikali za Mitaa (LAAC) umesababisha baadhi ya wabunge kutaka mawaziri
wang’oke.
Wakizungumza bungeni jana wakati wakichangia majadala uliohusu
taarifa za kamati hizo, wabunge hao walisema wamechoshwa na mijadala inayohusu
wizi na ubadhirifu wa fedha za umma kila mwaka na sasa wanataka hali hiyo
ibadilike ili Bunge lianze kujadili mikakati ya maendeleo.
Katika mchango wake, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ester Bulaya
alisema Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum hapaswi kubaki salama kutokana na
kuvunja katiba katika matumizi ya fedha za umma.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya PAC, waziri huyo ametumia fedha
zilizotengwa kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini na kuzitumia kwa matumizi
mengine, jambo ambalo ni kinyume cha sheria na katiba.
Aliliambia Bunge kuwa katiba ya Jamhuri ya Muungano, Ibara ya
135 na 136 inaelekeza kuwa fedha zote zinazokusanywa na serikali zinapaswa
kuingia kwenye mfuko mkuu wa Hazina isipokuwa zile ambazo zimeelekezwa na
sheria kutumika kwa matumizi maalum.
Alisema kuwa katiba hiyo pia inaelekeza kuwa fedha zilizotengwa
kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya matumizi maalum hazipaswi kutumika kwa ajili
ya mambo mengini zaidi ya yale yaliyokusudiwa.
“Bunge hili linatunga sheria, na kama viongozi lazima tuonyeshe
mfano wa kufuata sheria, leo hii tunazungumzia fedha ambazo zipo kwenye
ring fence, hazitakiwi kutumika kwa matumizi mengine, kwa mujibu wa sheria.
Waziri umevunja katiba ibara ya 135 na 136, ni Tanzania peke yake unabaki
salama….ukifanya mambo haya” alisema Bulaya.
Bulaya alisikitishwa na kitendo cha serikali kuchepusha fedha
ambazo zimetengwa kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kupeleka umeme vijijini ili
kuwakomboa wanawake wanateseka na vibatari kama njia pekee ya kupata mwanga kwa
maisha yao yote huko vijijini.
“Mmeshindwa kukata hela za chai, fedha za suti, za
sambusa, mnakata zinazokwenda kuacha tabia ya kutumia vibatari vijijini, kweli?
Halafu tuje hapa tuwapongeze? Mimi mbunge wa CCM ninayependa chama changu
kibaki madarakani siwezi kufanya hivyo,” alisema Bulaya.
“Taarifa zote hapa kila tukisoma ni wizi, wizi, wizi hatuwezi
kuvumilia, kama mnataka mbaki salama ni lazima muwabane watendaji wenu ili
mambo yaende vizuri,” alisisitiza.
Mbunge Mkanyageni Juma Habib Mnyaa (CUF) alisema kwa muda
mrefu Zanzibar imekuwa haipati mgawo wa fedha za kupeleka umeme vijijini wakati
Wazanzibari wanachangia upatikanaji wa fedha hizo.
Mnyaa alisema fedha kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini
zinapatikana baada ya kutozwa Shilingi 50 kwa lita ya mafuta na kwamba
mafuta ya Tanzania huagizwa kwa pamoja na fedha hizo hukatwa na TRA
wakati mafuta hayo yakiwa Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Zanzibar.
Alisema mafuta hayo yanapofika Zanzibar wananchi huuziwa kwa bei
ya juu wakilichangia na fedha ya umeme lakini hawajawahi kupelekewa umeme.
Mbali na hilo Mnyaa aliungana na wabunge wengine kupinga
ubadhirifu wa fedha za umma, akisema kuwa kiini cha upotevu wa fedha hizo ni
mikataba mibovu inayoingia serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Alitaka pamoja na mawaziri kuwajibishwa pia wale wote
walioshiriki kusaini mikataba mibovu kwa niaba ya Serikali pia wafiishwe
mahakamani kujibu tuhuma za kuiingizia serikali hasara na kusababisha matumizi
mabovu ya fedha za umma.
“Ikiwa hatutaisaidia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) kwa kuona wale wote walihusika na mikataba hii wafikishwe
mahakamani, Bunge tutakuwa hatujatenda haki, tupitishe maazimio kuwa mikataba
hii yenye utata wale wote waliohusika nayo washitakiwe,” alisema Mnyaa.
Alisema kuwa bila ya kufanya hivyo siku zote wabunge wataendelea
kupiga kelele bungeni na wahusika nao wataendelea kufanya uhalifu wao wakijua
kuwa hakuna hatua wanazochukuliwa.
Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema),
alisema kutokana na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma unaoendelea nchini,
taifa limekuwa sawa na chumba cha vijana wasio na makazi rasmi kiitwacho ‘geto’
ambako kila mmoja anafanya anavyotaka.
Alisema ili kurejesha misingi ya uadilifu ni lazima taifa lianze
kujenga utamaduni wa kuwajibishana bila kuoneana haya kwa wale wote
wanaoisababishia Serikali hasara au ubadhirifu wa rasilimali za umma.
Lema alisema kwa kuwa Bunge limemaliza kujadili sakata la Escrow
hivi karibuni, huenda wabunge wasione kuwa taarifa hizo zimebeba ufisadi mkubwa
kutokana na fedha zinazoonekana kupotea kuwa ndogo ikilinganishwa na zile za
Escrow.
Alisema lakini ukweli ni kwamba taarifa za kamati hizo
zinaonyesha kuna wizi na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma ambao hauwezi
kuvumilika.
“Kwa sababu hivi karibuni tumetoka kwenye wizi wa Shilingi
bilioni 300, Bunge halionekani kutetemeka sana kwa sababu ya wizi wa
Escrow,” alisema Lema.
Juzi jioni, Kamati tatu za Bunge ambazo ni ya Kudumu ya Hesabu
za Serikali, Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati ya Bajeti, ziliwasilisha
taarifa zake bungeni ambazo zilionyesha kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa wa fedha
katika taasisi mbalimbali za Serikali. Miongoni mwa taasisi zilizoguswa na
ubadhirifu huo ni pamoja na Mamlaka za Bandari Tanzania (TPA), Viwanja
vya Ndege (TAA), Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere wa Dar es Salaam na
halmashauri za wilaya na miji.
CHANZO: NIPASHE
Hakuna maoni
Chapisha Maoni