LOWASSA AZIDI GEUKWA NDANI YA CCM,MIKAKATI YA KUMUONDOA YABAINIKA TU,SOMA HAPA KUJUA
Pichani wa kwanza kulia ni Edward Lowassa akiwa na Waziri mkuu mstaafu Fredrck Sumaye picha na Maktaba |
Taarifa
kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa, huenda akaenguliwa iwapo atatangaza
nia na kuchukua fomu kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimezidi
kushika kasi.
Lowassa hajatangaza kuwania nafasi hiyo
ya juu kabisa katika utumishi wa umma nchini, lakini harakati zake za siasa
pamoja na watu wake wa karibu zinaonesha kuwa Mbunge huyo wa Monduli kwa zaidi
ya miaka 20, huenda akawa mgombea.
Umeundwa pia mtandao unaosambaza taarifa
kuwa Lowassa anaumwa, ukitaraji kuwa umma utafika mahala utaamini maneno hayo,
ambayo yamesemwa mara kadhaa, na Lowassa akajitokeza hadharani akiwa mwenye
siha njema.
Mmoja wa viongozi wa CCM, amekileza
chanzo chetu kwamba Mwenyekiti
wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, yuko njiapanda kutokana na shinikizo la kuchuja
wagombea Aprili, mwaka huu akiwamo Lowassa.
Mtoa taarifa amesema hatari kubwa iko kwa
vigogo watatu ambao baadhi yao wametangaza nia. Vigogo au makada hao kwa sasa
wanapigiwa chapuo waingie hatua ya tatu bora ndani ya CCM, na hapo ndipo
wanapopambana Lowassa asifikie.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. Mohamed Gharib Bilal, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Bernard Membe, na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye tayari
ametangaza ‘kimyakimya’, nao wanatajwa kumtesa Rais Kikwete.
“Hili linamuumiza kichwa Mwenyekiti (Rais
Kikwete). Kwa kweli yuko njiapanda. Watu anaofanya nao kazi anawatosaje? Yeye
mwenyewe halisemi hili ovyo. Ni gumu na linalosumbua kichwa,” anasema mtoa
habari na kuongeza.
“Kuna mashinikizo ya kuwafikiria
anaofanya nao kazi kwa sasa, Makamu wa Rais amefanya naye kazi kwa kipindi
chote cha miaka mitano; Waziri Mkuu atamtosa vipi, rafiki yake Membe atamtoa
vipi?” anahoji mtoa taarifa.
“Hawa ni lazima wapite, kwa sababu
taarifa zinasema kama Lowassa akipenya tu ndani ya tatu bora, ujue atateuliwa.
Mbinu hapa ni kufanya asifike huko,” anasema mtoa taarifa huyo aliyeomba
kuhifadhiwa jina.
Lowassa hajatangaza kuwania nafasi hiyo,
ila karibu kila kona ya nchi hii mazungumzo ya wananchi wa kawaida wanasema
wazi kuwa wangetaka Lowassa apewe usukani aweze kunyoosha mambo yaliyopinda
kutokana na falsafa yake ya kufanya uamuzi mgumu kwa wakati bila kuremba.
Bernard Membe kwa upande wake, ingawa
ametangaza tayari kutogombea ubunge katika Jimbo la Mtama, ambapo Katibu wa
Uenezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye, amejipanga kugombea jimbo hilo, kuhusu
urais, anasema hadi sasa “hajaoteshwa.”
Makamu wa Rais, Dk. Bilal mwishoni mwa
mwaka jana wakati Rais Kikwete anaumwa alikutana na wahariri kwa chakula cha
jioni nyumbani kwake, na wahariri walipomhoji iwapo atagombea urais, maana
wakati huo alikuwa Kaimu Rais, Rais Kikwete alipokuwa Marekani kwa matibabu,
wasaidizi wake walijibu kwa niaba yake kuwa hawajasikia neno la aina hiyo
kutoka kwake. Yeye hakujibu neno hilo, badala yake akapiga picha na wahariri
wakatawanyika.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, yeye
alipohojiwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) iwapo ana nia ya
kugombea urais, alimjibu Salim Kikeke, ambaye ni Mtangazaji wa BBC kuwa yeye
bado anatangaza “kimyakimya.”
Mbinu nyingine inayopendekezwa
kutumiwa kukata jina la Lowassa ni kuendelezwa kwa adhabu dhidi ya kada huyo
pamoja na makada wengine watano ambao mwaka mmoja uliopita, waliadhibiwa na
chama kutokana na kasi ya kuonesha nia ya kuwania urais.
Makada wengine walioadhibiwa na Lowassa
ni Membe, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais
(Uhusiano), Stephen Wasira, Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January
Makamba, na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Licha ya makada hao kufungiwa mwaka
mmoja kuanzia Februari 18, mwaka jana kutojishughulisha na shughuli za kisiasa
kwa kuwa zingewapa kura ya turufu katika kuwania uongozi wa nchi, baadhi yao hawakujali
kwani waliendelea kutangazani nia.
Viongozi
hao waliadhibiwa na Kamati Ndogo Maalum ya Nidhamu iliyowatia hatiani kwa kosa
la kuanza kampeni mapema. Kamati hiyo iliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM,
Philip Mangula.
Hata hivyo, Makamba, Wasira na Sumaye
wameendelea na shughuli za kijamii bila hofu, huku wengine wakijitokeza akiwamo
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba; Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Asiye na Wizara Maalum, Profesa Mark
Mwandosya, na Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mtoa taarifa anasema tahadhari
kubwa ya Rais Kikwete ipo katika kutengeneza uhusiano na diplomasia ndani ya
chama kwamba baada ya uteuzi kusiwe na mgawanyiko aina yoyote.
Mtoa habari ambaye ametoka kwenye
vikao vya CCM huko Zanzibar amesema kwa nia ya kujenga uaminifu kwenye chama na
Serikali, anasema Rais Kikwete anapata taabu kutokana na Lowassa kuwa na sifa
mbili kwake.
Kwanza Rais Kikwete anawaza uhusiano
kati yake na Lowassa walioutangaza kwamba “hawakukutana barabarani”, na pili
nguvu ya ushawishi na Lowassa kuungwa mkono na wanachama wengi na hata nje ya
chama. Licha ya Lowassa kutotangaza nia, lakini waliotangaza nia, kauli zao
zinaonesha kutaka kupambana na mbunge huyo ambaye CCM ilifikia hatua ya kumpunguza
kasi yeye na makada wenzake watano mwaka jana.
Taarifa zinasema kwa mara ya kwanza
wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, alikubali kupewa Makamu Rais aliyekuwa
Mgombea Mwenza, Dk. Mohamed Shein lakini akapinga kuletewa Waziri Mkuu. Nafasi
hiyo alimpa kada mwenzake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mbunge wa Monduli
Lowassa ambaye alikitumikia cheo hicho kwa miaka miwili na mwezi mmoja kabla ya
kujiuzulu akateuliwa Pinda.
Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM
ameiambia Chanzo chetu kuwa chama hakina mpango wa kumtimua
mwanachama yeyote kama inavyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Lakini akasisitiza, “CCM itakuwa
makini sana na mgombea atakayeteuliwa. Katika hili la urais na uchaguzi wa
wabunge na madiwani, chama kiko makini sana katika haya. Sawa.”
Mchakato wa uchaguzi ndani ya CCM
unatarajiwa kukamilishwa Aprili, mwaka huu. Hii ina maana mwezi Machi utakuwa
mwezi wa mikikimikiki. Wagombea watarajiwa karibu wote hawakuwa tayari
kulizungumzia hili, wakiiambia Chanzo chetu kuwa wakati haujawafika
Chanzo
ni Gazeti la Jamhuri
Hakuna maoni
Chapisha Maoni