Zinazobamba

WAZIRI MKUU PINDA APATA NUKSI NYINGINE KWENYE UTAWALA WAKE, SOMA HAPA KUJUA

Waziri Mkuu Mizengo Pinda
   
Wiki chache baada ya kunusurika kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya IPTL ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameingia matatani tena baada ya kutuhumiwa kuhusika kuharibu uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika juzi.

Wengine wanaoandaliwa maamuzi hayo, ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, baadhi ya wasiMamizi wa uchaguzI huo pamoja na Jeshi la Polisi.

Tuhuma hizo zilitolewa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kikisema kitafanya maamuzi dhidi ya Pinda kupitia Kamati Kuu katika kikao chake maalumu cha dharura kinachotarajiwa kufanyika wakati wowote, kuanzia sasa.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Tanzania Bara, John Mnyika, alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

Alisema uamuzi wa kuitisha kikao hicho cha kamati kuu, umefikiwa na viongozi wakuu wa Chadema na kwamba, kitafanyika mapema iwezekanavyo mara baada ya kupokea taarifa za matokeo ya uchaguzi huo, kazi ambayo alisema wanaendelea kuifanya.

“Kikao hiki cha kamati kuu kitafanya maamuzi mazito juu ya hatua za kuchukua kwa serikali, ambayo katika jambo hili inaongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kama waziri mwenye dhamana na Tamisemi na vyombo vyote vinavyohusika kuharibu uchaguzi,” alisema Mnyika.

Alisema hatua hizo zitaamuliwa na kikao hicho cha kamati kuu, ambacho kitajadili ajenda moja maalumu pekee ya uchaguzi huo, ndicho kitakachoeleza.

Mnyika alisema pamoja na kikao hicho cha kamati kuu kufanyika, Chadema wakiwa sehemu ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), watashiriki chaguzi za marudio zilizosogezwa mbele katika maeneo mbalimbali nchini kutokana na kuharibika na kwamba, kwa njia ya nguvu umma wataendelea kushinda.

Hivyo, alisema wanatarajia Pinda na serikali watarekebisha kwa haraka kasoro zote zilizojitokeza na kusababisha uchaguzi kuharibika.  Alisema hilo ni kutokana na uchaguzi huo kugeuka kuwa tishio la amani ya wananchi, ikiwamo baadhi kupigwa, kunyanyaswa, kuibiwa na wengine kuuawa. 

Alisema juzi Katibu Mkuu Tamisemi, Jumanne Sajini, alisema kwamba taratibu zote za uchaguzi zimekamilika kwenye halmashauri zote na kwamba, hakukuwa na tatizo, lakini alipohojiwa sababu za kuwapo kasoro, alisema zimesababishwa na wakurugenzi wa halmashauri.

Mnyika alisema pia jana Waziri Ghasia alizungumza na baadhi ya vyombo vya habari na kurudi kujaribu kuhamisha mzigo wa lawama za ubovu wa uchaguzi huo kwa wakurugenzi wa halmashauri. 

Hata hivyo, alisema kabla ya uchaguzi wa sasa, kulifanyika kikao kati ya serikali na vyama vya siasa mkoani Morogoro juu ya maandalizi ya uchaguzi huo na kwamba, katika kikao hicho yeye (Mnyika) aliwakilisha viongozi wakuu wa Chadema na kwamba, upande wa serikali uliwakilishwa na Waziri Ghasia.

Alisema wadau waliojadiliana katika kikao hicho, waliziona kasoro za uchaguzi kabla hazijatokea na pia waliona mgogoro uliokuwapo kati ya kauli ya Rais Jakaya Kikwete ya kusogeza uchaguzi huo mbele na ile ya kuendelea na maandalizi bila ya kuwa kamili.

Mnyika alisema pia waliona kasoro ya mapendekezo ya serikali ya kanuni za uchaguzi, ambazo alisema zimeleta matatizo makubwa kwenye uchaguzi katika maeneo mbalimbali nchini, lakini Waziri Ghasia kwa niaba ya waziri mkuu aliendelea kushikilia msimamo wa serikali wa kuandaa uchaguzi huo mbovu.

“Kwa hiyo, Waziri Hawa Ghasia pamoja na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, hawawezi kukwepa lawama na rai ya kutakiwa kuwajibika kutokana na kasoro, ambazo zimejitokeza kwenye uchaguzi huu,” alisema Mnyika.

Aliwataka wananchi kuendelea na maandalizi ya chaguzi hizo na kusubiria hatua, ambazo kamati kuu ya chama itaamua.
 
“Na visingizio vinavyotolewa na Waziri Hawa Ghasia na waziri mkuu au mtendaji mwingine yeyote wa Tamisemi, haviwezi kuhalalisha udhaifu, uzembe na matatizo ya hujuma ambayo yalipangwa kuanzia mwanzo, yakapingwa, lakini bado yakatekelezwa na sasa yameharibu uchaguzi katika taifa letu,” alisema Mnyika.

Aliongeza: “Kwa hiyo, tulisema pamoja na kuwa Waziri Hawa Ghasia amelizungumza leo (jana), tulijibu leo (jana). Kwamba, asikwepe lawama za kuwajibika yeye na waziri mkuu kutokana na haya.

“Na wasikwepe lawama pia ya mambo yote yanayotokea, iwe yanayofanywa na Jeshi la Polisi, iwe yanayofanywa na wasimamizi, kwa sababu dalili zilionyesha toka mwanzo kwamba mambo haya yaliandaliwa kufanyika.”

Kuhusu baadhi ya maeneo, ambayo wagombea wa vyama vinavyounda Ukawa kutoshirikiana, Mnyika alisema watafanya tathmini ili kurekebisha changamoto hiyo.

Hata hivyo, alisema ni maeneo machache, ambayo yamekumbwa na changamoto hiyo kulinganisha na maeneo mengi, ambayo ushirikiano baina ya vyama hivyo umetekelezwa.  Pinda alinusurika kuhusishwa katika kashfa ya akaunti hiyo baada ya kutetewa na wabunge wengi bungeni kwa madai kwamba, hakuhusika.

Alipata utetezi huo baada ya taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kumhusisha kwa maelezo kwamba alikuwa anajua kilichokuwa kikiendelea katika kashfa hiyo.

Kigezo kikubwa kilichotumiwa na PAC kumhusisha Pinda katika kashfa hiyo, ni kauli yake kwamba, fedha hizo hazikuwa za umma aliyoitoa bungeni.

 Bunge lilimvua rasmi kuhusika na kashfa hiyo baada ya kupitisha maazimio dhidi ya wote waliohusika katika kashfa hiyo, huku wakitajwa nyadhifa zao, bila kumtaja Pinda kwa namna yoyote ile.  

JOHN MREMA
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri na Bunge wa Chadema, John Mrema, alisema sababu zilizochangia kuharibu uchaguzi huo katika maeneo mengi ya Tanzania Bara ni pamoja na uzembe na hujuma.

Alidai hujuma hizo zimekuwa zikifanywa na serikali kwa kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM).Mrema alisema mpaka kufikia juzi majira ya jioni, katika maeneo mengi, vifaa vya uchaguzi vilikuwa havijafika na hivyo kusababisha uchaguzi kuahirishwa.

Alisema pia CCM kwa kushirikiana na baadhi ya wasimamizi wa uchaguzi walihusika katika kuvuruga uchaguzi huo.Alitoa mfano wa baadhi ya maeneo katika jiji la Dar es Salaam akisema kwamba, baadhi ya wagombea wa CCM na mawakala wao waliingia kwenye vituo na kuchukua masanduku ya kura na mengine kuyamwagia maji kwa makusudi na hivyo kuvuruga uchaguzi.

“Na mfano dhahiri, ni mtaa huu wa makao makuu ya chama. Uchaguzi ulikuwa unafanyika hapo upande wa polisi. Mgombea wa CCM na wapambe wake wakaingia kituoni,wakachukua yale maboksi, wakamwagia maji zile karatasi za kura, ikapelekea uchaguzi kuahirishwa,” alisema Mrema.

Alisema pia katika maeneo mengine, wagombea wa CCM walifanya hivyo hivyo, huku wasimamizi wakiwa wanawatazama na kwamba, suala hilo lilisababisha pia katika baadhi ya maeneo uchaguzi kuahirishwa.

Mrema alisema katika maeneo mengine, hadi kufikia jana mchana, matokeo ya uchaguzi yalikuwa bado hayajatangazwa kwa sababu masanduku ya kura yalikuwa yakishikiliwa katika vituo vya polisi, kinyume cha taratibu za kidemokrasia.

Mrema alisema hali hiyo ilisikika pia katika maeneo ya Kimara, Mbezi, Gongo la Mboto na Ukonga, jijini Dar es Salaam, ambako risasi za moto zilikuwa zikifyatuliwa.
 Alisema katika Wilaya ya Nzega, mkoani Tabora, mwanachama wa Chadema, aitwaye Batholomeo, akiwa analinda kura, alipigwa risasi na polisi na amefariki.

Alisema pia kuna masanduku ya kura yako kwenye vituo vya polisi, ambako yamelala katika vituo hivyo na kusema mifano iko mingi jijini Dar es Salaam na mikoani.

 “Kwa mfano, Dar es Salaam, serikali ya mtaa ya Mwenge-Nzasa maboksi ya kuhesabia kura mpaka sasa yako kituo cha polisi Mabatini. Hatujui huko polisi yalilindwa au kura zimeshabadilishwa usiku au nini kimetokea. Kimara, Mbezi Louis, maboksi yako kituo cha polisi Mbezi. Ukienda Bunda, maboksi yako kituo cha polisi Bunda,” alisema Mrema.

Alisema kama kunatokea vurugu, ni wajibu wa jeshi hilo kulinda vituo ili msimamizi pamoja na mawakala wahesabu kura na kutangaza matokeo na siyo vinginevyo.

Alisema katika maeneo mengine, kufikia jana asubuhi, wasimamizi walikuwa hawajarudi vituoni, hivyo aliitaka serikali kuhakikisha matokeo hayo yanatangazwa na kura hizo hazichakachuliwi kwa sababu wana uhakika watu wao wamezilinda.

KATA 127 HAZIKUFANYA UCHAGUZI
WILAYA tatu na Kata 127 nchini, hazijafanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa.Aidha, kuanzia mwaka 2019, uchaguzi huo utakuwa unaendeshwa na kusimamiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia, alisema sababu za kuahirishwa kwa uchaguzi huo ni kutokana na kasoro mbalimbali ikiwamo kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura vituoni.

Alisema kasoro nyingine ni karatasi ya kupigia kura katika nafasi ya mwenyekiti wa kijiji kuunganishwa na nafasi ya mwenyekiti wa kitongoji, nembo za vyama kuwekwa kwa mgombea wa chama kingine, majina ya wagombea kukosewa, kukosekana kwa majina ya wagombea, karatasi za kupigia kura kuwa chache kuliko idadi ya walioandikishwa na kukosekana kwa majina ya wapigakura.

“Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu uchaguzi umeahirishwa kwa sababu ya kuchanganya karatasi za kupigia kura mfano karatasi za Kata X kupelekwa kwenye Kata Y. Wilaya ya Kaliua uchaguzi umeahirishwa kwa sababu ya ucheleweshaji wa vifaa na kasoro katika karatasi za kupigia kura,” alisema.

Ghasia alisema Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga haijafanya uchaguzi kwa sababu ya ucheleweshaji wa vifaa na mchanganyiko wa majina.

Waziri Ghasia alisema watakaobainika kufanya uzembe na kusababisha dosari kwenye uchaguzi huo watachukuliwa hatua kali ikiwamo kukatwa mshahara, kushushwa cheo au kufukuzwa kazi. 

“Hii ni taarifa ya awali ya yaliyojitokeza, tumeitaka mikoa iwasilishe taarifa rasmi na kamilifu kuhusu kilichojitokeza katika Halmashauri. Wizara itachambua taarifa hizo ili kubaini wote waliosababisha kasoro ili wachukuliwe hatua stahiki,” alisema Ghasia.

 Hata hivyo, alisema Halmashauri 145 zimefanya uchaguzi huo bila dosari, Halmashauri 14 ndizo zenye kasoro kwenye baadhi ya maeneo na tatu hazijafanya kabisa na kuahidi kwamba uchaguzi huo utafanyika Jumapili ijayo.

 Halmashauri za Wilaya na idadi ya Kata ambazo zitarudia uchaguzi Jumapili ijayo kwenye mabano ni Rombo (4), Hanang' (8), Mbulu (4), Ulanga (8), Mvomero (1), Msalala (8), Busega (4), Itilima (1), Kwimba (18), Sengerema (28), Muheza (20), Bunda (1), Serengeti (13), Sumbawanga (8) na Temeke (4)

Hakuna maoni