UWEZO WA VYUO VIKUU KUCHUKUA WANAFUNZI WA SAYANSI BADO CHANGAMOTO KWA TANZANIA KUTIMIZA MALENGO YA EFA
Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi nchini Tanzania Mh. Dkt. Shukuru Kawambwa akifungua mkutano wa kimataifa wa kutathmini mafanikio na changamoto za utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Kimataifa wa Elimu kwa Wote-EFA uliofanyika jijini Dar Es Salaam ambapo amesema tangu mwaka 2000 Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuelekea kutimiza malengo ya Mpango huo ikiwa ni utashi wa kisiasa na kuwajibika vikisaidiwa na kujitolea kwa wadau wa sekta ya elimu pamoja na washirika wa maendeleo.(Picha na Zainul Mzige wa MOblog).
Tanzania imekuwa moja wapo ya nchi za kutolea mfano miongoni mwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara katika kutekeleza maazimio ya mpango wa Elimu kwa wote (EFA).Akihutubia wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kimataifa wa wadau wote wa elimu , Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Ufundi nchini Tanzania Mh. Dkt. Shukuru Kawambwa amesema Tanzania Bara na Visiwani imeweza kukaribia kufikia malengo ya mpango huo ikiwa ni pamoja na suala la wastani wa waalimu kwa wanafunzi.
Amesema kwamba kwa shule za msingi Tanzania Bara imefikia wastani wa wanafunzi 47 kwa mwalimu mmoja wakati Visiwani Zanzibar ni wastani wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 27. Mafanikio mengine yaliyopatikana chini ya mpango huo ni kuboresha wastani wa wanafunzi kwa darasa, ambapo kwa Tanzania Bara wastani umetoka kuwa wanafunzi 92 kwa darasa na sasa ni wanafunzi 65 huku Zanzibar wastani ukiwa ni wanafunzi 62 kwa darasa.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bi. Zulmira Rodrigues akizungumza wakati wa mkutano wa kimataifa wa kutathmini mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika kutekeleza malengo ya Mpango wa Kimataifa wa Elimu kwa Wote –EFA ulioshirikisha wadau wote wa sekta ya elimu uliofanyika jijini Dar Es Salaam. Amesema lengo kuu la mkutano huo ni kuiandaa Tanzania kuweza kushiriki kikamilifu katika mashauriano ya kiserikali baina nchi mbalimbali na kuhakikisha wadau wakuu wa elimu kitaifa wanapata taarifa juu ya mapendekezo ya agenda zitakazoanza mwaka 2015.
Awali Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Bi. Zulmira Rodrigues amesema ikumbukwe kwamba malengo nane (8) ya EFA yanachangia kufanikisha Malengo Makuu ya Maendeleo ya Millennia (MGDs) yaliyopitishwa mwaka 2000 kati ya nchi 189 na Taasisi za Mendeleo zinazoongoza Duniani.
Bi. Rodrigues amefafanua kuwa tunapoelekea mwaka 2015, Tanzania Bara na Visiwani zimeonyesha juhudi katika kupunguza tofauti kubwa zilizokuwepo kielimu ikiwa ni pamoja na kukabilia na changamoto zilizojitokeza na kuweza kuweka sera, mipango na utawala bora katia Nyanja za fedha , wadau, usimamizi na uwajibikaji.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni