SERIKALI YA KIKWETE YAWEKWA MIFUKONI MWA BOSI WA IPTL,SASA AAMUA KUIVIMBIA TRA,SOMA HAPA KUJUA
Pichani ni Mmiliki wa IPTL, Seith |
Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WAKATI
ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ikionyesha
Kampuni ya Power Solution Limited (PAP) ilikwepa kodi ya Sh bilioni 8.68,
kampuni hiyo imekimbilia Bodi ya Rufaa ya Kodi kupinga hatua ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA) kuondoa hati za awali za kuthibitisha ulipaji wa kodi.
PAP ambayo inadaiwa kulipwa visivyo
halali Sh bilioni 306 zilizokuwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, ombi lake
lilikubaliwa na bodi hiyo ambayo imemzuia kwa muda Kamishna Mkuu wa TRA kuondoa
hati zake zinazothibitisha ulipwaji wa kodi wakati wa mchakato wa kununua hisa
za Kampuni ya IPTL.
Uamuzi huo ulitolewa Novemba 26 na
Katibu wa bodi hiyo, Respicius Mwijage, baada ya kusikiliza maombi ya zuio la
muda yaliyowasilishwa na PAP na IPTL dhidi ya Kamishna Mkuu wa TRA na Msajili
wa Makampuni nchini (Brela).
Madai ya msingi ya PAP ni kutaka
kuendelea kutambulika kama kodi waliyolipa ni halali na kupinga uamuzi wa TRA
kuondoa hati zake hizo.
Katika kutaka zuio la muda, wadai hao
waliitaka bodi hiyo iwazuie walalamikiwa, mawakala wao, waajiri wao au mtu
yeyote atakayefanya kazi kwa niaba yao kuondoa hati za kuthibitisha kulipwa kwa
kodi ya ongezeko la mtaji kuhusu uuzwaji wa hisa za IPTL.
Katika maombi hayo, wadai walizitaja
hati hizo kuwa ni namba 0049656 na 0049657 ambazo zilitolewa kwa ajili ya
uuzaji wa hisa kutoka Kampuni ya Mechmar na Piper Links Investment na kati ya
Piper Links na PAP.
Walitaka hati hizo zizuiwe
kuondolewa kwa namna yoyote hadi rufaa waliyofungua kupinga kuondolewa
itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.
Kampuni
hiyo pia inaiomba bodi itoe amri ya muda kwamba hali ilivyo sasa iendelee kuwa
hivyo hadi rufaa yao itakaposikilizwa.
Madai hayo yaliambatana na hati ya
kiapo iliyoapwa na Manraj Bharya ambaye ni Mkurugenzi wa PAP na Parthiban
Chandrasakaran ambao wanadai katika kiapo kwamba PAP ilishanunua hisa zote za
IPTL.
Hati hiyo ya kiapo inadai Novemba 19
Kamishna wa TRA alitoa taarifa kwa IPTL akionyesha nia ya kuondoa hati hizo
zinazothibitisha kuwa kampuni hiyo ililipa kodi.
Inadaiwa sababu za kuondoa hati hizo
ni kutokana na mkataba feki wa makubaliano ya mauzo ya hisa hizo kwa makampuni
husika ambapo kodi iliyolipwa inaonekana ilikuwa ndogo.
Wadai hao waliiomba mahakama kutoa
zuio la muda kwani isipofanya hivyo wataingia kwenye hasara ambayo haiwezi
kulipika.
Hata hivyo, Katibu Mwijage alitoa amri
ya muda kwamba hali ibaki kama ilivyo sasa na kwamba nia ya kuondoa hati za
kuthibitisha ulipaji wa kodi iliyotolewa na TRA kupitia barua ya Novemba 19
mwaka huu ikielekezwa BRELA, isimamishwe hadi maombi yatakaposikilizwa.
Aliamuru maombi ya kuwazuia TRA na
BRELA kuondoa hati za ulipaji kodi yasikilizwe Desemba 10.
RIPOTI YA
CAG NA KODI ILIYOKWEPWA
Kwa mujibu
wa ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Septemba 9,
2012 Kampuni ya Mechmar iliuza hisa saba kwa Piper Links ilizokuwa inamiliki
katika Kampuni ya IPTL kwa bei ya dola za Marekani milioni 6.
Hata
hivyo, taarifa zilizowasilishwa TRA kwa ajili ya kukokotoa kiasi cha kodi ya
ongezeko la mtaji ambacho Mechmar ilitakiwa kulipa, zinaonyesha hisa hizo
zimeuzwa kwa Sh milioni 6 za Kitanzania badala ya dola za Marekani.
Kutokana na udanganyifu huo, kodi ya
ongezeko la mtaji iliyolipwa ni Sh 596,500 badala ya Sh 1,919,988,800
iliyopaswa kulipwa.
Kwa upande wa ushuru wa stempu, Mechmar
ilipaswa kulipa Sh milioni 96 na siyo Sh 60,000 ilizolipa.
“Jumla ya kodi iliyopotea kwa maana ya
kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu ni Sh 2,015,988,800,” inasema
taarifa ya PAC.
Inasema hisa hizo kutoka Kampuni ya
Piper Links kwenda PAP, ziliuzwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 20,
lakini taarifa zilizopelekwa TRA zilionyesha hisa hizo zimeuzwa kwa dola za
Marekani 300,000.
“Kwa mantiki hiyo, taarifa ya CAG
inaonyesha Piper Links ilitozwa na kulipa kodi ya ongezeko la mtaji Sh 47,940,000
na Sh 4,800,000 kama ushuru wa stempu (stamp duty),” ilisema ripoti hiyo.
Katika mahojiano, Kamishna Mkuu wa
TRA aliifahamisha kamati kuwa kwa gharama ya dola za Marekani milioni 20, kiasi
cha kodi ya ongezeko la mtaji kilichotakiwa kulipwa ni Sh 6,399,977,600 na si
Sh 47,988,800, na kwa upande wa ushuru wa stempu kiasi kilichotakiwa kulipwa ni
Sh 320,000,000 na si Sh 4,800,000.
“Kwa maana hiyo, jumla ya kodi
iliyopotea kwa maana ya kodi ya ongezeko la mtaji na ushuru wa stempu ni Sh
6,667,188,800.
“Jumla ya kodi iliyopotea kutokana na
uuzaji wa hisa za Mechmar kwenda Piper Links na za Piper Links kwenda PAP ni Sh
8,683,177,600,” inasema taarifa ya PAC.
Ikulu,
Bunge zarushiana mpira
Wakati hayo yakiendelea, Katibu wa
Bunge, Dk. Thomas Kashililah, amesema chombo hicho hakiwezi kupeleka maazimio
yake serikalini kwani Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ndiye mtendaji mkuu wa
shughuli za Serikali bungeni, alishayapokea na kuyatolea ufafanuzi siku ya
kuahirisha Bunge.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku
chache tangu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kueleza kwamba ofisi
yake haijapokea rasmi maazimio ya Bunge.
“Ninavyojua ni kwamba Bunge litaleta
rasmi mapendekezo hayo serikalini,” alisema Balozi Sefue.
Akizungumza na Chanzo changu jana, Dk.
Kashililah alisema maazimio yalitolewa bungeni na kujibiwa na Waziri Mkuu,
hivyo inamaanisha kwamba tayari yalishafika serikalini.
“Maazimio yalitolewa bungeni na
baadaye Waziri Mkuu kuyatolea ufafanuzi, inamaanisha kuwa tayari yameshaifikia
Serikali kwa kuwa yeye ndiye mtendaji mkuu wa Serikali bungeni,” alisema Dk.
Kashililah.
Maazimio ya Bunge yameitaka mamlaka
ya uteuzi kuwawajibisha wote waliotajwa kuhusika na kashfa ya Escrow
Hakuna maoni
Chapisha Maoni