MASIKINI MREMA"", UBUNGE WAKE SASA WAOTA MBAWA HUKO VUNJO. SOMA HAPA KUJUA ZAIDI
HALI ya kisiasa ya Mbunge wa Vunjo mkoani Kilimanjaro, Augustine Mrema, (TLP), imezidi kuwa mbaya baada ya ngome yake kuzidi kumeguka na kutangaza kumuunga mkono Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia katika uchaguzi mkuu mwakani.
Hivi karibuni wakati wa Bunge Maalum la Katiba mjini Dodoma, Mrema alikaririwa akilalamika kuwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), ambayo ni CHADEMA, CUF na NCCR Mageuzi, vimemtangazia vita kumpora jimbo hilo na kuomba CCM waende Vunjo kumsaidia.
Awali kabla hajalalamika katika bunge hilo, alifikisha kilio chake kwa Rais Jakaya Kikwete wakati wa mkutano wa viongozi wa Kituo cha Demokrasia (TCD), akidai Rais ndiye anampa kiburi Mbatia baada ya kumteua kuwa mbunge na kutaka amnyang’anye.
Wakati Mrema akiweweseka juu ya hatma yake ya kurejea bungeni mwakani, baadhi ya Madiwani wa TLP na Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametangaza kumuunga mkono Mbatia katika mbio za kugombea ubunge wa jimbo hilo 2015.
Madiwani hao, Meja mstaafu Jesse Makundi wa Kata ya Mwika Kaskazini, Yolanda Lyimo wa Kilema Kati wote TLP na Joachim Tesha wa Kirua Magharibi, walitangaza uamuzi huo kwa nyakati tofauti wakati Mbatia akiongoza harambee ya ujenzi wa maabara na bweni katika shule za Sekondari za Pakula, Kiluani na Mwika, ambako sh milioni 48 zilipatikana.
Akitangaza kumuunga mkono Mbatia, Meja Makundi ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Vunjo mwaka 2000-2005, ambaye ndiye aliyemuangusha Mbatia aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo wakati huo, alisema amefikia uamuzi huo kutokana na kutambua uwezo wa Mbatia katika uongozi.
Meja Makundi anayetajwa mmoja wa madiwani wenye nguvu na ambaye alikuwa ni tegemeo la kambi ya Mrema, alisema kwa sababu mwaka 2000, alipokea tochi ya kumulikia Wana Vunjo kutoka kwa Mbatia, basi ameona ni busara kuirudisha kwa aliyemkabidhi.
Kujitokeza kwa Meja Makundi kunafanya idadi ya viongozi wakubwa katika siasa za Jimbo la Vunjo waliojitokeza hadharani kumuunga mkono Mbatia kufikia wanne pamoja na Wenyeviti zaidi ya 10, akiwemo wa Kijiji cha Nduweni, Nemes Minja, ambaye aliwahi kuwa dereva wa Mrema.
“Leo nimefikia uamuzi ambao naamini ndio hitaji la Wana Vunjo, kwa kuwa Jimbo hili nililipokea kutoka kwa Mbatia, na kwa kuwa yeye ndiye aliyenikabidhi hii Tochi (anakabidhi Tochi kwa Mbatia), natamka hadharani kuwa Mbatia ndiyo chaguo langu, yeye ndio atakayemulika Wana Vunjo,” alisema Meja Makundi.
Awali, wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mikutano miwili tofauti, Diwani Yolanda na Diwani Tesha, walinukuliwawa wakidai kuwa uamuzi wa kumuunga mkono Mbatia ni uamuzi wa Mungu.
“Tunamuomba Mungu amuinue aweze kuwa Mbunge wetu, mimi ni Diwani wa TLP, nina Mbunge wangu, namuheshimu sana (Mrema), lakini namuomba Mungu amteue Mbatia chaguo letu Wana Vunjo, nafahamu wapo watakaonukuu maneno yangu lakini kama mbaya acha iwe mbaya,” alisema.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Tanzania Daima hivi karibuni, Mbatia ambaye ni Mbunge wa Kuteuliwa na Rais, amesema kitendo cha Mrema kulalamika kwamba yeye pamoja na viongozi wa UKAWA, kuwa wamemuingilia jimboni mwake ni sawa na kulalamikia kivuli.
Alisema malalamiko ya Mrema hayana msingi wowote na kumtaka aache kumchafua kwenye vyombo vya habari, huku akisisitiza kutokuwa tayari kujibizana naye, badala yake ataelekeza nguvu zake katika kuwatumikia wananchi wa Vunjo.
“Siko tayari kujibizana na mtu, kuna kazi kubwa mbele yetu, tuelekeze nguvu zetu kuwatumikia Wana Vunjo, mkutano wa Septemba ndio unaomtesa, nyinyi ni mashahidi tangu Septemba 6 sijafanya mkutano wowote, kulalamika kwake ni sawa na kulalamikia kivuli… kivuli chake kinamuhukumu, mimi siko tayari kumjibu,” alisema Mbatia.
Hakuna maoni
Chapisha Maoni